Habari

‘Kinara’ wa wizi wa magari kortini

ERNEST Sambuo maarufu kama White na wenzake wanne, jana walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, kujibu kesi mbili za wizi wa magari mawili tofauti.

Regina Kumba


ERNEST Sambuo maarufu kama White na wenzake wanne, jana walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, kujibu kesi mbili za wizi wa magari mawili tofauti. Inadaiwa kuwa kesi moja inahusu wizi wa gari moja kwa kutumia silaha. White alikuwa akitafutwa tangu aliyekuwa Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa nchini, Imran Kombe auawe na polisi waliomfananisha naye.


Watuhumiwa wengine katika kesi hiyo ni Aston Lyatuu (31), Emmanuel Clement (33), Kitoi Ndosi (22) na Filbert Joseph (20). Watuhumiwa wote, isipokuwa Ndosi katika kesi yao ya kwanza iliyoko mbele ya Hakimu Mkazi Addy Lyamuya, wanadaiwa kuwa waliiba gari aina ya Toyota Corolla yenye thamani ya Sh 5,000,000.


Mwendesha Mashitaka Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Charles Kenyella alidai kuwa watuhumiwa walitenda kosa hilo Januari 20 mwaka huu, saa mbili usiku katika maeneo ya Mikocheni B, Dar es Salaam. Ilidaiwa kuwa gari hilo lilikuwa mali ya Bernard Membe na ili kufanikisha wizi huo walimtishia kwa bastola kichwani, Ally Kassim.


Watuhumiwa walikana shtaka hilo na Kenyella aliomba kesi iahirishwe kwa vile upelelezi haujakamilika. Aliiomba watuhumiwa wanyimwe dhamana, kwa vile kosa hilo halina dhamana chini ya kifungu cha sheria ya mwaka 1985. Hakimu alikubaliana na ombi hilo. Katika kesi nyingine iliyoko mbele ya Hakimu Ezron Mwankenja ambayo inawahusu watuhumiwa wote, ilidaiwa kuwa walitenda kosa hilo Julai 15, mwaka huu saa 4:50 asubuhi katika eneo la Sea Cliff Village Masaki, Dar es Salaam.


Watuhumiwa walidaiwa kuiba Toyota Land Cruiser yenye thamani ya dola za Marekani 55,000, mali ya Kampuni ya China Hennan International Cooperation Group. Kenyella pia aliomba watuhumiwa wasipewe dhamana kama ilivyokuwa kwa shtaka la kwanza ambalo halina dhamana. Alidai kuwa kuwapa watuhumiwa hao dhamana kutaharibu upelelezi, kwa sababu bado watuhumiwa wengine wanaendelea kutafutwa kutokana na mtandao wa wizi wa magari kuwa mkubwa.


Mtuhumiwa Emmanuel alidaiwa kuwa na kesi nyingine katika mahakama hiyo ambayo alihukumiwa kifungo cha miaka 15 na viboko sita baada ya kukutwa na hatia ya kupora ingawa hakuwapo wakati wa hukumu. Ilidaiwa kuwa alitoroka baada ya kudhaminiwa. Mtuhumiwa huyo pia ana kesi nyingine ya uhujumu uchumi mahakamani hapo akidaiwa kukutwa na bastola. Kesi hiyo itafikishwa mahakamani Agosti 29, mwaka huu. Kesi nyingine ziliahirishwa hadi Agosti 14, mwaka huu.


Souce: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents