Habari

Kinyang’anyiro CCM wagombea waanza kumwaga rushwa

MBIO za kuelekea uchaguzi katika Chama Cha Mapinduzi (CCM), zimeanza kuingia katika sura mpya baada ya baadhi ya wagombea wanaowania nafasi mbalimbali za uongozi katika chama hicho mkoani Dar es Salaam, kutoa rushwa hadharani kwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu

Na Muhibu Said


MBIO za kuelekea uchaguzi katika Chama Cha Mapinduzi (CCM), zimeanza kuingia katika sura mpya baada ya baadhi ya wagombea wanaowania nafasi mbalimbali za uongozi katika chama hicho mkoani Dar es Salaam, kutoa rushwa hadharani kwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu, ili kuwashawishi wawapigie kura katika uchaguzi huo.


Rushwa ambayo imeshuhudiwa ikitolewa na wagombea hao (majina tunayo) kwa wajumbe hao, ni pamoja na chakula, vinywaji na fedha taslimu.


Vigogo hao ambao baadhi yao wana nyadhifa kubwa serikalini na katika chama, wameshuhudiwa juzi katika maeneo tofauti jijini Dar es Salaam wakiwahonga wajumbe hao.


Baadhi ya wajumbe ambao hawakutaka kutaja majina yao, walilithibitishia Mwananchi kunufaika na ‘takrima’ waliyodai kupewa na vigogo hao.


Wagombea hao walitoa ‘takrima’ hiyo katika maeneo ya Kigamboni, Ilala, Kimara na wengine katika maeneo ya Tabata, jijini Dar es Salaam.


Mgombea mmoja aliwakusanya baadhi ya wajumbe katika baa moja iliyopo Tabata na kuanza kuwakirimu wajumbe hao kwa chakula, vinywaji na fedha taslimu Jumamosi wiki iliyopita.


Baadhi ya watu walioshuhudia tukio hilo walisema kigogo huyo (jina tunalo), anadaiwa kumwaga takrima kwa wajumbe hao, kuanzia saa 6:00 mchana hadi 12:00 jioni katika baa hiyo.


“Haikuwa mchezo. Watu walikula, wakanywa kama hawana akili. Ni chereko chereko ndizo zilizotawala jana (juzi) hapa,” alisema mmoja wa wahudumu wa kike alipozungumza na Mwananchi katika baa hiyo jana mchana.


Wakati kigogo huyo akielezewa hivyo, kigogo mwingine wa CCM, alishuhudiwa akimwaga ‘takrima’ katika maeneo ya Kigamboni Jumamosi kuanzia mchana hadi jioni katika baa moja.


Mgombea huyo ambaye ni kiongozi mwandamizi katika chama hicho, anadaiwa kumwaga pilau, vinywaji na fedha taslimu.


Wakati hayo yakiendelea jijini Dar es Salaam, kinyang’anyiro cha kuwania nafasi mbalimbali za ungozi ndani ya CCM inazidi kushika kasi katika mikoa mbalimbali nchini, huku baadhi ya wagombea wakidaiwa kuanza kampeni kwa nguvu.


Wilayani Geita mkoani Mwanza, mgawanyiko mkubwa umeanza kuikumba CCM kufuatia vigogo kadhaa wa chama hicho, walioangushwa katika uchaguzi mkuu wa wabunge mwaka 2005 kuanzisha makundi na kuanza kujipanga kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 2010 kwa kupanga safu zao za uongozi katika ngazi mbalimbali.


Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hii baadhi ya vigogo wenye majina makubwa miongoni mwao wakiwemo wale walioangushwa katika uchaguzi wa wabunge wa mwaka juzi, wamekuwa wakishiriki kikamilifu katika kuhakikisha wanapanga safu zao za uongozi na kuhakikisha kwamba watu wao wanashinda katika chaguzi zinazoendelea ndani ya CCM.


Vigogo hao wamekuwa wakionekana huku na kule wakihaha kuhakikisha kwamba, watu wao wanashinda ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kushinda katika uchaguzi wa mwaka 2010, huku mara nyingine wakitumia fedha nyingi kujaribu kuwashawishi wananchama wa chama hicho kugoma kufanya uchaguzi pale ambapo wanaona kwamba watu wao waliowaandaa majina yao hayakurudishwa.


Wakati huo huo, Samson Chacha kutoka Tarime anaripoti kuwa, Idadi ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Mara wanaowania kuchukua fomu za kugombea uongozi katika chama hicho ngazi mbalimbali imezidi kuongezeka.


Habari zilizolifikia gazeti hili mwishoni mwa wiki zinasema kuwa wakati Enock Mwita Chambiri amechukua fomu hizo kutetea wadhifa wake wa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Christopher Mwita na Gachuma wamechukua fomu hizo kutaka kumnyang’anya wadhifa huo.


Wengine waliochukua fomu hizo ni Abiud Maregesi. Waliochukua fomu hizo kugombea ujumbe wa NEC ni Mbunge wa Musoma mjini, Vedastus Mathayo, Kisyeri Chambiri aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Tarime, Thobias Rayah na Isack Chacha ambaye ni Diwani wa Kata ya Bweri- Musoma.


Rumanyika Kyombo anayetetea kiti hicho na Hafidhi wamechukua fomu kugombea kiti cha mweka hazina wa mkoa na Mwandishi wa habari, Maximillian Ngessi, Juma James na Magoti Emmanuel wamechukua fomu hizo kugombea nafasi ya katibu mwenezi wa mkoa.


Wengine waliochukua fomu za uenyekiti wilaya ya Tarime ni Thobias Rayah anayetetea kiti hicho, Mseti Mwita Nyaronyo, Peter Wangwe Keba aliyekuwa mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Tarime.


Waliochukua fomu za uenezi Wilaya ya Tarime ni Mairo Marwa anayetetea kiti hicho, Samwel Kiboye ambaye ni Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Tarime, Christopher Samwel Chomete, Dock Kisare aliyekuwa diwani wa NCCR Mageuzi aliyehamia CCM hivi karibuni, Yakob Chongore (kada wa chama) na Wankyo Kisyeri Chambiri.


Aliyechukua fomu ya kuwania uweka hazina wilaya ya Tarime ni John Gimunta anayetetea kiti hicho kwa mara nyingine. Wagombea wote wanatakiwa kurudisha fomu hizo Juni 5, mwaka huu katika ofisi husika za CCM.


Naye Shija Felician anaripoti kutoka Shinyanga kuwa, mkoani Shinyanga waliochukuwa fomu jana kuwania ujumbe wa NEC ni diwani kata ya Isaka Jared Mwanzia kupitia vijana, na Mbunge wa Msalala, Ezekiel Maige. 


Naye Midraji Ibrahim, anaripoti kuwa, staili ya uchukuaji fomu hasa kwa kundi la wanamtandao, kuwania ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuchukua fomu kwenye mikoa mingine, umeendelea baada ya Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Diodorus Kamala kuchukulia fomu Morogoro.


Dk Kamala ambaye ni mjumbe wa NEC-CCM kwa kundi la vijana, alisema atarajesha fomu hizo Mkoa wa Kagera na anawania nafasi hiyo kupitia viti 20 bara. Alikabidhiwa fomu hizo jana na Katibu wa CCM Mkoa wa Morogoro, Mary Chatanda.


Utaratibu kama huo pia ulitumiwa na Mbunge wa Chalinze, Ramadhan Maneno ambaye baada ya kuchukulia fomu hizo Kibaha kama alivyofanya mwaka 2002, alichukulia wilayani Kisarawe.


Maneno ambaye ni Mjumbe wa NEC-CCM, katika uchaguzi wa mwaka 2002, alimwangusha kada mkongwe wa chama hicho, Paul Sozigwa.


Akizungumza baada ya kukabidhiwa fomu hizo jana na Katibu Msaidizi wa CCM Wilaya ya Kisarawe, Said Bakari, Maneno alisema lengo la kuchukulia fomu Kisarawe ni kutambua kwamba wilaya zote za Mkoa wa Pwani zinamhusu kama mjumbe wa NEC-CCM mkoa.


Pia, Paul Kirigini anayewania ujumbe wa NEC kupitia kundi la vijana alichukua fomu hizo jana Mkoa wa Dar es Salaam na kusema kwamba atazirejesha Mkoa wa Mara.


Kirigini ambaye ni mfanyakazi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), alisema lengo la kuwania nafasi hiyo ni kuitikia wito wa viongozi wa CCM kwa wanachama wenye sifa kuwania uongozi.


Alisema licha ya kuitikia wito huo, pia anataka kuimarisha demokrasia na kuongeza uwakilishi wa vijana kwenye vikao vya maamuzi ya chama.


Source: Mwananchi

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents