Kipanya chaua saba

WATU saba wamekufa papo hapo na wengine 11 kujeruhiwa katika ajali mbaya ya basi dogo aina ya Toyota Hiace ‘kipanya’, lililokuwa likisafiri kutoka Tukuyu mjini, Wilaya ya Rungwe kuelekea Kyela

na Christopher Nyenyembe, Kyela




WATU saba wamekufa papo hapo na wengine 11 kujeruhiwa katika ajali mbaya ya basi dogo aina ya Toyota Hiace ‘kipanya’, lililokuwa likisafiri kutoka Tukuyu mjini, Wilaya ya Rungwe kuelekea Kyela. Basi hilo lilipinduka na kutumbukia bondeni katika eneo la Stamico.

Ajali hiyo ilitokea juzi usiku majira ya saa 2.00, ikilihusisha gari hilo lenye namba za usajili T 123 ABR.

Polisi tayari wamemtia mbaroni dereva wa gari hilo, Ambikile Seti (29), ambaye amelazwa katika Hospitali ya Makandana Rungwe pamoja na majeruhi wengine.

Abiria waliofariki katika ajali hiyo ni pamoja na Emi Mwamoto (33) mkazi wa Chunya mwanafunzi wa chuo cha uuguzi Chunya na Agness Mgogo, ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Ipinda Kyela.

Marehemu mwingine ametambuliwa kuwa ni Mkuu wa Shule ya Sekondari Ngonga, Ikupa Mwandoloma (44), Bupe Mwaikasu (42) mkazi wa Mbugani wilayani Kyela na Donald Henry (27), mkazi wa Tukuyu.

Marehemu wengine bado hawajatambuliwa kutokana na miili yao kuharibika vibaya huku majeruhi, ambao wamelazwa katika Hospitali ya Makandana, wakitajwa kuwa ni Suma Mwankenja, Leonard Andolile, Innocent Mwangaza, Janeth Mwanjoka, Lucy Sanga na Happy Mwakatobe.

Majeruhi aliyenusurika na kulazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kyela, Hussein Hassan (38) mkazi wa Ndandalo, alisema kuwa ajali hiyo ilitokea kutokana na mwendo mkali wa basi hilo dogo.

Alisema ni dhahiri kuwa kutokana na mwendo huo mkali, basi hilo lilimshinda dereva baada ya kukosa breki na lilipofika katika eneo la Stamico, kwenye kona kali, ndipo lilipoacha njia na kutumbukia bondeni.

Mbali ya majeruhi huyo, mwingine aliyelazwa katika hospitali hiyo ni Mary Mwamwembe (18), mkazi wa Ndandalo na majeruhi mwingine ambaye inadaiwa kuwa katika hali mbali akiwa hajitambui kwa mujibu wa maelezo ya wauguzi wa hospitali hiyo.

Miili sita ya watu waliofariki katika ajali hiyo, imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kyela na mwingine katika Hospitali ya Makandana.

Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Mashimba Mashimba, aliyefika eneo la ajali hiyo muda mfupi baada ya kutokea, alielezea hali ya kutisha aliyoikuta katika eneo la ajali.

Alisema kuwa, baadhi ya miili ya abiria waliokuwemo katika basi hilo dogo iliharibika vibaya, huku mingine ikiwa imetupwa bondeni na mingine kung’ang’ania juu ya miti ilipotupwa nje kutoka kwenye gari hilo.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, Suleiman Kova, akizungumza kwa njia ya simu kutoka mjini Mbeya, alisema kuwa ajali hiyo imesababishwa na uzembe mkubwa wa dereva huyo, ambaye alijua wazi kuwa gari lake halikuwa na breki, lakini akaliendesha kwa mwendo wa kasi.

Kova alisema kuwa kutokea kwa ajali hiyo kumerudisha nyuma jitihada za polisi mkoani humu, za kupunguza ajali za barabarani na kwamba jeshi hilo linalaani vikali uzembe huo uliopoteza maisha ya watu na mali zao.

“Dereva huyu alitakiwa achukue tahadhari baada ya kugundua kuwa gari lake ni bovu, halina breki, lakini hakuweza kutii kelele za abiria hao waliomtaka asimame… alizidi kuwapa matumaini kuwa mambo yatakuwa shwari,” alisema Kamanda Kova.


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents