Kisasa, Kaburu Wagaragazwa TFF

KATIBU Mkuu wa Yanga, Lucas Kisasa ameangushwa katika mchujo wa kupata wawakilishi wa klabu wanaowania wadhifa wa makamu wa pili wa rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

KATIBU Mkuu wa Yanga, Lucas Kisasa ameangushwa katika mchujo wa kupata wawakilishi wa klabu wanaowania wadhifa wa makamu wa pili wa rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Kisasa aliyekuwa akiwania nafasi moja kati ya mbili pamoja na Damas Ndumbalo, Godfrey Nyange ‘Kaburu’ na Ramadhan Nassib alishindwa kupita katika mchujo huo baada ya kuambulia kura moja.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Henry Tandau aliwataja waliopita katika uchaguzi huo mdogo uliofanyika jijini Dar es Salaam jana kuwa ni wakili Ndumbalo aliyepata kura nane na Ramadhani Nassib, pia akipata kura nane huku Kaburu akiungana na Kisasa kutupwa.
Katika nafasi ya uwakilishi wa klabu za Ligi Kuu kwenye Kamati ya Utendaji ya TFF ambapo wagombea walikuwa watatu, waliopita ni Wallace Karia aliyepata kura 11 na Abdul Sauko aliyepata kura nane wakimwacha Mohammed Nassoro aliyeshindwa kwa kupata kura tano.
Tandau alisema majina ya wagombea waliopita katika mchujo huo wa jana yatapelekwa katika uchaguzi mkuu wa TFF, Desemba 14 kwa ajili ya kupigiwa kura.
Akizungumza baada ya uchaguzi huo kumalizika, Ndumbaro aliwashukuru wenyeviti wa klabu za ligi kuu kwa kumpa heshima kubwa na kuongeza kuwa anatarajia ushindani utakuwa mkali zaidi kutokana na mpinzani wake naye kuwa na sera nzuri.
Naye Nassib pamoja na kuwashukuru wenyeviti wa klabu hizo kwa kuonyesha kuwa na imani naye na kwamba anastahili kuwepo kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi huo wa TFF, lakini alieleza kuwa sasa anajipanga upya ili kuhakikisha anatwaa nafasi ya makamu wa pili wa rais katika uchaguzi huo.
Wakati huo huo, Mulamu Ng’hambi aliyerejeshwa na kamati ya rufaa baada ya awali kuenguliwa na kamati ya uchaguzi kwa kutohudhuria usaili, amepitishwa jana katika usaili mdogo na hivyo kuwa mgombea wa nafasi ya ujumbe anayewakilisha klabu za Kanda ya Dodoma na Singida.
Nafasi ya makamu wa pili wa rais ilikuwa ikishikiliwa na Jamal Bayser, aliyechukua nafasi ya Ismail Aden Rage ambaye alifungwa jela kutokana na kesi ya matumizi mabaya ya fedha na mali za kilichokuwa Chama cha Soka Tanzania (FAT), wakati ule akiwa Katibu Mkuu.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents