Habari

Kisima cha gesi Mtwara hatarini, serikali yaanza kuchukua hatua

Serikali imeahidi kuchukuliwa kwa hatua za haraka za kudhibiti athari za mmomonyoko wa ardhi katika kisima cha gesi asilia, kilichopo kijiji cha Msimbati kwenye kisiwa cha Mnazi Bay mkoani hapa kwa kujengea ukuta, kutokana na kuongezeka kwa kina cha bahari katika eneo hilo.

Hayo yalibainishwa jana na Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani baada ya kutembelea kisima hicho kwa lengo la kujionea na kujiridhisha athari ya mmomonyoko huo. Alisema, wakati wowote kisima hicho kinaweza kujaa maji ya bahari na kusababisha nchi kukosa nishati hiyo, hivyo ni vema wataalamu wakaangalia namna ya kujenga ukuta ili kunusuru athari hiyo isitokee.

Hili ni jambo la dharura tusisubiri tatizo litukumbe ndipo tuanze kuhangaika. Mara nyingi huwa tunachelewa kuchukua hatua. Gesi tunayoitegemea kwa sasa hivi kwenye kuzalisha nishati ni hii hapa, sasa ikifikia hatua maji yakajaa na kukisomba kisiwa hiki tutakuwa wageni wa nani? “Anzeni sasa kufanya utaratibu wa kujenga ukuta kwa sababu mtafika mahala mtakosa hata mahali pa kuweka ukuta, kwani maji yakishafika huku haitawezekana kufanya chochote.

Ni bora tuanze sasa wakati bado ni mapema kuliko kuchelewa kukatokea madhara makubwa,” alisema Dk Kalemani. Alizitaka mamlaka zinazohusika na usimamizi wa kisima hicho, kukutana mara moja na kuweka mbinu za kuanza kujenga ukuta huo. “Ujio wangu hapa leo ni katika kuhakikisha kuwa kisima hiki kinabakia kuwa salama ili kuiwezesha nchi kuendelea kupata nishati itokanayo na gesi asilia.

Ni lazima wote wanaowajibika na usimamizi wa kisima hiki wakae chini na kujipanga kwa kila mmoja kutimiza wajibu wake itakiwavyo,” alisema Dk Kalemani. Naibu Mkurugenzi wa Kampuni ya Maurel & Prom inayojihusisha na uchimbaji wa gesi hiyo ya asilia katika kisima hicho, Elius Kilembo alisema athari kama hiyo ya tishio la kisima hicho kusombwa na maji, iliwahi kutokea mwaka 2015.

Lakini, alisema madhara yaliishia umbali wa mita 150 kutoka eneo la bahari hadi kwenye kisima hicho, lakini sasa upo uwezekano wa madhara kufika jirani zaidi. Alisema, mwaka 2017 pia athari hiyo iliwahi kutokea, lakini haikuleta athari yoyote. Lakini, mwaka huu ni vema hatua za haraka zichukuliwe, kabla ya kutokea kwa madhara yaliyoanza kujitokeza.

Hapa pana kina kirefu sana usione hivi yaani panapotokea athari kama hii ni muda mfupi sana madhara yanatokea, kwa hiyo serikali iangalie namna ya kudhibiti hili tatizo, isingoje mpaka madhara kutokea,” alisema. Mkazi wa kijiji hicho, Juma Maarufu alisema ni vema serikali ikachukua hatua ya kuangalia namna ya kuhamisha kisima hicho kutokana na madhara yatakayojitokeza kuwa makubwa, endapo kisima hicho cha gesi asilia kitasombwa na maji.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents