Habari

Kiswahili chapendekezwa kuwa lugha rasmi ya mawasiliano katika nchi za SADC

Kamati ya Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) leo Agosti14 wamekubaliana na kuifanya lugha ya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya nne ya jumuiya hiyo huku wakieleza kuwa kwa sasa wanasubiri baraka za wakuu wa nchi hizo ili ianze kutumika.

Akizungumza mara baada ya kikao cha mawaziri wa SADC , Mwenyekiti wa kamati ya baraza hilo la mawaziri wa SADC ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje na uUhirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi amesema baada ya baraza la mawaziri kukaa kwa siku mbili wametoka na mapendekezo 107 ambayo yatapelekwa kwa wakuu wa nchi kwa ajili ya majadiliano yatakayofanyika Agosti 17 na 18 mwaka huu.

“Mkutano wa mawaziri hautoi maamuzi bali uamuzi utatolewa na wakuu wa nchi baada ya kukaa katika kikao cha siku mbili, moja ya pendekezo kubwa na lenye kuleta heshima kwa watanzania ni kuichagua lugha ya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya nne ambayo itatumika katika ngazi mbalimbali ikiwemo katika vikao vya baraza la mawaziri, vikao vya wakuu wa nchi, hotuba mbalimbali na baadaye kutafsiriwa katika nyaraka mbalimbali” ameeleza Kabudi.

Pia amesema katika mapendekezo hayo ambayo yamejikita katika kauli mbiu ya mazingira wezeshi ya biashara na ukuaji wa viwanda ndani ya jumuiya wanachama kwa muda wa mwaka mmoja uenyekiti utakaoongozwa na Rais. Dkt. JohnJoseph Magufuli utahakikisha biashara inakua katika ukanda wa SADC.

“Tupo chini sana katika masuala ya umiliki wa biashara tunamiliki asilimia20 pekee huku asilimia 80 tukizitumia kununua bidhaa kutoka nje hali inayokosesha ajira kwa vijana wetu” ameeleza.

Aidha amesema kuwa kwa muda wa mwaka mmoja wa uenyekiti Tanzania itahakikisha asilimia 60 ya vijana ambalo ndilo kundi kubwa linapata ajira aidha kwa kujiajiri au kuajiriwa na hiyo ni kwa kuhakikisha biashara zinafanywa kwa kuhusisha nchi zote wanachama na pia watahakikisha wanashirikiana katika kuhakikisha Zimbabwe inaindolewa vikwazo walivyowekewa na baadhi ya nchi na hiyo ni baada ya nchi hiyo kufanya uchaguzi na kubadilisha mifumo mbalimbali hivyo hakuna sababu ya kuwekewa vikwazo ambavyo huwaumiza wananchi.

Mapendekezo hayo 107 yatajadiliwa na kufanyiwa maamuzi katika kikao Cha wakuu wa nchi na Serikali kitakachofanyika Agosti 17 na 18 mwaka huu.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents