Technology

Kiwanda kikubwa zaidi cha kutengeneza simu barani Afrika, Chazinduliwa nchini Rwanda ‘Simu zitauzwa kwa mkopo’

Kampuni ya Mara Group yenye makazi yake Mjini Dubai, imefungua kiwanda kikubwa cha teknolojia ya juu ya kutengeneza simu katika ukanda wa kiuchumi jijini Kigali, nchini Rwanda.

Kiwanda hicho ambacho kilizinduliwa jana Oktoba 7, 2019 na Rais wa Rwanda, Paul Kagame kina uwezo wa kuzalisha simu milioni 2 kwa mwaka.

Mmiliki wa kiwanda hicho, Ashish Thakkar amesema kiwanda hicho kinakusudia kutengeneza simu zenye ubora wa juu zitakazouzwa kwa bei nafuu ili kuwezesha lengo la kuboresha ukuaji wa matumizi ya simu janja barani Afrika.

Tumetambua kuwa ili kuleta matokeo chanya kwenye jamii zetu za bara la Afrika na katika masoko yanayokua kwa kasi. Tunahitaji kuwa na simu zenye ubora wa juu, zinazopatikana kwa bei nafuu. Hapo ndipo tulipopata wazo la kuanzisha kiwanda cha Mara Phones,” amesema Thakkar wakati wa ufunguzi.

Kiwanda cha Mara Phones kitaanza kuzalisha aina mbili za simu ambazo ni Mara X na Mara Z. Simu zote zitauzwa chini ya $200 sawa na Tsh. 460,000, Imeelezwa kuwa simu hizo zitakuwa na betri inayoweza kudumu na chaji muda mrefu na uwezo mkubwa wa kuhifadhi taarifa.

View image on Twitter

Kampuni hiyo pia imeingia ubia na taasisi za kifedha na mitandao ya simu nchini humo, ambapo mnunuaji wa simu anaweza kukopa na kuanza kulipa kidogo kidogo kwa hadi miaka miwili.

Kampuni ya Mara Group imesema kiwanda hicho ndiyo kikubwa zaidi Afrika na chenye teknolojia ya juu zaidi barani Afrika.

Mwanzilishi wa kampuni hiyo, Thakkar amesema viwanda vingi vilivyopo Afrika si vya kutengeneza simu, bali kuunganisha (assembling plants), lakini walichofungua nchini Rwanda ni kiwanda cha kutengeneza simu.

Tawi lingine la Mara Phones linatarajiwa kufunguliwa mwishoni mwa mwezi huu nchini Afrika Kusini.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents