Michezo

Kocha wa Azam FC, Aristica Cioaba afungiwa

Kocha wa Azam FC, Aristica Cioaba amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la kuwafuata waamuzi na kuwalalamikia kwa kurusha mikono akionyesha kutoridhika na maamuzi yao.

Cioaba , alifanya hivyo kwenye mechi namba 69 ya ligi kuu ya Vodacom dhidi ya Ruvu Shooting iliyofanyika Novemba 4, 2017 kwenye Uwanja wa Azam Complex na adhabu hiyo imezingatia kanuni ya 40(1) ya ligi kuu kuhusu udhibiti wa Makocha

Kanuni: 40 Udhibiti kwa Makocha

Kocha (coach) yeyote atakayefanya jambo lolote kati ya haya yafuatayo ataadhibiwa kwa mujibu wa kanuni  hii.

(1) Akimshambulia mwamuzi, mchezaji au kiongozi yeyote, kwa maneno au vitendo,  kabla, wakati au baada ya mchezo, atatozwa faini isiyopungua sh. 500,000 (lakitano) na kufungiwa michezo isiyopungua mitatu (3), bila ya kujali adhabu yoyote iliyotolewa na mwamuzi kiwanjani.

(2) Akitoa kauli au ishara inayoashiria au kushawishi shari kabla, wakati au baada ya mchezo atatozwa faini isiyopungua sh. 500,000 (laki tano) na kufungiwa michezo isiyopungua mitatu (3).

(3) Akibainika kuwa anadai hongo au amepokea/ametoa hongo au kuhusika na matendo yoyote yanayoashiria hongo ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa ya mpango wa hongo inayotia mashaka, kutoa taarifa ya mchezo isiyo sahihi kwa makusudi atafungiwa maisha.

(4) Akijishirikisha na vitendo vyovyote vile vinavyoashiria imani za uchawi au ushirikina atatozwa faini isiyozidi isiyopungua sh. 500,000 (laki tano) na kufungiwa michezo isiyopungua mitatu (3).

(5) Akifanya kitendo chochote ambacho ni kinyume cha maadili ya taaluma ya ukocha wa mpira wa miguu kama vile kuhudhuria kikao cha maandalizi ya awali ya mchezo au kusimamia benchi la ufundi katika mchezo akiwa amelewa atafungiwa kipindi kisichopungua mwaka mmoja au/na faini ya sh. 500,000 (laki tano).

(6) Akibainika kughushi saini ya mchezaji au kufanya tendo lolote kwa lengo la kukamilisha zoezi la usajili kwa udanganyifu atafutwa katika orodha ya waalimu, leseni yake itatwaliwa na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

(7) Akibainika kusababisha timu kutofika uwanjani na kukosa mchezo, baada ya kuhudhuria kikao cha maandalizi, atatozwa faini ya sh. 1,000,000 (milioni moja) na kufungiwa kwa kipindi kisichopungua miezi kumi na mbili (12).

(8) Akibainika kusababisha au kuhamasisha vurugu au kugomea mpaka kupelekea mchezo kuvunjika atafungiwa kwa kipindi kisichopungua miezi kumi na miwili na faini ya sh. 1,000,000 (milioni moja).

(9) Akithibitika kutoa shutuma, kejeli au kushambulia mwamuzi wa mchezo, msimamizi, Bodi ya Ligi Kuu au TFF kwenye vyombo vya habari atafungiwa kushiriki mechi tatu mpaka sita na/au kutozwa faini ya sh. 1,000,000 (milionimoja).

(10) Akithibitika kumchezesha mchezaji ambaye ni batili kiusajili au ambaye usajili wake haujathibitishwa na TFF atafungiwa kwa kipindi cha mwaka mmoja na faini ya sh. 500,000 (laki tano).

(11) Kocha atakayetolewa na mwamuzi kwenye mchezo wa Ligi Kuu (ordered off) atafungiwa kuiongoza timu yake kwenye vyumba vya kuvalia na benchi la ufundi katika michezo isiyopungua miwili (2) inayofuatia ya timu yake na faini ya sh.500,000 (laki tano).

(12) Kocha atakayekataa kuhojiwa na vyombo vya habari kwenye mchezo wa Ligi Kuu baada ya kutakiwa kufanya hivyo na maofisa wa mchezo atafungiwa kuiongoza timu yake kwenye vyumba vya kuvalia na benchi la ufundi la timu yake katika michezo miwili (2) inayofuata na/au kutozwa faini ya sh. 500,000 (laki tano).

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents