Michezo

Kocha wa Manchester United Ole Gunnar afunguka “Pogba anastahili Unahodha”

Kocha wa Manchester United Mnorway, Ole Gunnar Solskjaer amefunka kuhusu ubora wa Kiungo wa klabu hiyo, Mfaransa Paul Pogba na kusemaKiungo huyo” Ana sifa za kuwa nahodha wa Manchester United”.

Ikumbukwe Pogba aliwahi kuwa nahodha msaidizi wa United kabla ya kocha Jose Mourinho kumvua wadhifa huo mwanzoni mwa msimu.

Kiungo huyo mwenye miaka 25 alivaa kitambaa cha unahodha msimu huu katika mechi tatu wakati Antonio Valencia alipokuwa majeruhi. Hata hivyo alivuliwa madaraka hayo mwezi Spetemba.

“Namjua kijana huyu (Pogba) kwa muda sasa na ni kiongozi,” amesema Solskjaer, ambaye alimfunza Pogba akiwa kinda kati ya miaka ya 2008 na 2010.

“Ana ushawishi mkubwa mbele za watu. Anajali na uchu wa mafanikio.

Maisha ya Pogba nje ya uwanja yamekuwa yakisimangwa sana, sawa na namna anavyotembea kwa madaha kabla ya kupiga mikwaju ya penalti msimu huu.

Lakini masimango hayo yanaonekana kugonga mwamba, na kiwango chake mchezoni kimeimarika maradufu toka Solskaer alipochukua mikoba ya Mourinho aliyetimuliwa kazi mwezi Disemba.

Katika mechi sita chini ya Solskjaer Pogba amefunga magoli matano na kupiga pasi za mwisho zilizozaa magoli manne.

“Paul ana mbwembwe nyingi pia, lakini hivyo ndivyo alivyo,” amesema Solskjaer.

“Mitandao ya kijamii ni sehemu ya maisha tunayoyaishi kwa sasa. Ndiyo jamii ya leo. Tuna kanuni kadhaa lakini sina tatizo na mitadao.”

Mustakabali wa nahodha Valencia katika uga wa Old Trafford ni finyu, na tangu mwezi Septemba amecheza mechi moja tu ya Ligi ya Premia.

Wakati Valencia akiwa nje, na Pogba kuvuliwa madaraka, Mourinho alimkabidhi mikoba ya uongozi Ashley Young na Solskjaer hana mpango kwa sasa kufanya mabadiliko.

“Yeye (Young) ni aina ya mwisho ya kizazi cha manahodha wa kizamani,” amesema Solskjaer. “Ni muhimu kutokuogopa kusimama mbele ya wachezaji wenzako na kuwakosoa pale inapobidi.”

By Ally Juma.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents