Habari

Kortini Dar akihusishwa mihadarati nchini China

MKAZI mmoja wa jijini Dar es Salaam, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akihusishwa na kifo cha mtu mwingine aliyekufa baada ya mihadarati aliyomeza, kupasukia tumboni.

na Asha Bani


MKAZI mmoja wa jijini Dar es Salaam, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akihusishwa na kifo cha mtu mwingine aliyekufa baada ya mihadarati aliyomeza, kupasukia tumboni.



Mtu huyo alifikishwa mahakamani hapo jana na akasomewa mashitaka mawili yanayohusu biashara hiyo haramu ya dawa za kulevya.



Mtuhumiwa huyo aliyetajwa kwa jina la Ali Khatibu Shikuba (37), mkazi wa Mbezi jijini Dar es Salaam, alisomewa mashitaka ya mauaji ya kukusudia pamoja na kutoroka akiwa chini ya ulinzi wa polisi.



Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Hezron Mwankenja, Mwendesha Mashitaka, Inspekta wa Polisi, Boniface Edwin alidai kuwa, mnamo Septemba 4, mwaka jana, mshitakiwa alimuua kwa makusudi, Kheto Brown Kheto, wakiwa nchini China.



Alidai kuwa, mtuhumiwa alimtuma Kheto asafirishe dawa hizo kutoka China na kuzileta nchini kwa kuzimeza tumboni. Hata hivyo, zilipasuka zikiwa tumboni na kumsababishia mauti.



Katika shitaka jingine, Mwendesha Mashitaka Edwin, alidai kuwa, baada ya tukio hilo, mshitakiwa alikamatwa na Polisi wa China na akawekwa chini ya ulinzi katika nyumba ya wageni ya Xiushian Lou namba 3007.



Hata hivyo, kwa kutumia ujanja, mtuhumiwa alifanikiwa kuwatoroka polisi na kutokomea kusikojulikana.



Tangu siku hiyo, mtuhumiwa hakuonekana tena mpaka alipokamatwa na D/A Inspekta Jumanne Kim, Machi 30 mwaka huu, majira ya saa 1:00 usiku huko Magomeni.



Mshitakiwa hakutakiwa kujibu lolote kwa sababu mahakama hiyo haina uwezo kisheria kusikiliza kesi za mauaji.



Ndugu na jamaa kadhaa wa mtuhumiwa, walikusanyika mahakamani hapo, huku baadhi yao wakibubujikwa na machozi na wengine kuangua vilio wakati wote mtuhumiwa alipokuwa anasomewa mashitaka.



Vilio hivyo vilizidi wakati mtuhumiwa huyo anaondolewa mahakamani hapo kupelekwa rumande.



Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents