Kubenea atoboa siri ya kumwagiwa tindikali

Mhariri wa gazeti la MwanaHalisi na Mseto Bw. Saed Kubenea amelihusisha tukio la kuvamiwa na kumwagiwa tindikili kuwa linatokana na kazi zake pamoja na msimamo wa gazeti

Saed Kubenea


 


Na Grace Michael




MHARIRI wa gazeti la MwanaHalisi na Mseto Bw. Saed Kubenea amelihusisha tukio la kuvamiwa na kumwagiwa tindikili kuwa linatokana na kazi zake pamoja na msimamo wa gazeti.

Bw. Kubenea aliyasema hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati akitoa ushahidi wake kuhusiana na tukio lililofanyika ofisini kwake la kuvamiwa na kumwagiwa tindikali pamoja na kujeruhiwa kwa sime.

Alidai kuwa alikuwa akipata barua za vitisho kutoka kwa watu mbalimbali pamoja na mawakili wanaowatetea viongozi wanaodaiwa kuwa ni mafisadi lakini yeye amekuwa akijibu kupitia gazeti lake.

“Tukio hili ninalihusisha moja kwa moja na kazi zangu kwani ndani ya miaka miwili nimeweza kufichukua maovu mengi ndani ya jamii hasa ya viongozi hivyo hata tukio hili nadhani limetokana na hayo,” alidai Bw. Kubenea.

Mbali na barua hizo za vitisho pia aliiambia mahakama kuwa alikuwa akipokea ujumbe mfupi wa simu za mkononi ambao hakuweza kuusoma lakini mahakama iliutaka upande wa mashitaka kwenda katika kampuni ya simu na kuchapisha ujumbe huo ili uweze kusomwa mahakamani hapo Mei 19 mwaka huu.

Alisema kuwa Januari 5 mwaka huu akiwa ofisini kwake saa 2.00 usiku ghafla alisikia mlango ukisukumwa kwa nguvu na alipokwenda kufungua alikutana na mtu aliyemwamuru kukaa chini lakini alikaidi amri hiyo.

“Baada ya kuniambia nikae chini na amenifuata mimi nilirudisha mlango haraka na kuingia ndani lakini walifanikiwa kufungua mlango huo na kuingia vijana watatu ambao walianza mashambulizi hadi kunimwagia maji maji ambayo yanilifanya nipoteze uwezo wa kuona kutokana na macho kuingiwa na maji hayo,” alisema Bw. Kubenea.

Alisema kuwa katika purukushani hizo, Mhariri mwenzake, Bw. Ndimara Tegabwage alifanikiwa kuwazidi nguvu waliokuwa wamevamia na kutoka nao nje ya ofisi ambapo walikimbia.

Baada ya kukimbia kwa wavamizi hao, walikwenda hospitali iliyopo Kinondoni na walifanikiwa kutoa taarifa hizo katika Kituo cha Polisi Oysterbay na askari walifika hospitalini hapo na kuwashauri kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Alidai kuwa kutokana na madhara ambayo aliyapata kwa kumwagia kemikali alilazimika kwenda India kwa matibabu zaidi.

Kesi hiyo ina jumla ya washitakiwa sita ambao baadhi yao wako rumande kutokana na kushindwa kutimiza masharti ya dhamama.

Washitakiwa katika kesi hiyo ni, Bw. Alex Anyemike, Bw. Hashimu Mdoe, Bw. Augustino Kimario, Bw. Hamisi Almasi, Bw. Alfred Benard na Bw. Frednand Msekwa ambao wanadaiwa Januari 5 mwaka huu, Kinondoni katika ofisi za Gazeti la MwanaHalisi na Mseto waliwajeruhi, Bw. Saed Kubenea na Ndimara Tegambwage.

Inadaiwa Bw. Kubenea alijeruhiwa kwa sime katika shavu na kumwagiwa kemikali na Bw. Tegambwage alikatwa kwa sime kisogoni.


 


Source: Majira


 

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents