Burudani

Kwanini Hollywood inaenda Uganda au Kenya kufanya kazi na si kuja Tanzania? Tumeziangalia sababu

Mara ya mwisho kusikia msanii mkubwa wa Marekani amekuja Tanzania na kufanyia video yake huku ni Oktoba 2007. John Legend alisafiri hadi visiwani Zanzibar kwenda kushoot video ya wimbo wake Show Me.

Tangu hapo, sijasikia tena msanii mwenye ukubwa wa Legend kuja Tanzania kwa mradi wa aina hiyo. Wenzetu Kenya na Uganda, hali iko tofauti. Ni juzi tu, Disney walikuwa Uganda kutengeneza filamu ya binti bingwa wa mchezo wa chess wa nchini humu, Phiona iitwayo Queen of Katwe ambayo Lupita Nyong’o aliigiza.

Lakini pia hivi karibuni rapper French Montana alienda nchini humo kushoot video ya wimbo wake Unforgettable aliomshirikisha muimbaji wa kundi la Rae Sremmurd, Swae Lee.

Huku Tanzania tunapata ugeni wa mastaa wanaokuja kutalii tu akiwemo Will Smith ambaye alikuja mwezi uliopita na kutembelea mbuga ya wanyama ya Serengeti. Huku hawaji kufanya kazi, wanakuja kula bata na kuondoka. Kwanini wakati kwa mujibu wa Rais wa shirikisho la filamu Tanzania, TAFF, Simon Mwakifamba, nchi yetu ni ya pili kwa mandhari nzuri za filamu?

“Ya kwanza ni Brazil, ya pili ni Tanzania, ina mazingira mazuri sana ya sinema. Kama ni wa pili duniani basi kwa Afrika ni wa kwanza kwakuwa na mazingira bora ya kisinema,” Mwakifamba ameiambia Bongo5.

Mwakifamba amesema watu wengi wangependa kuja kufanya filamu zao Tanzania lakini kinachokwamisha ni nchi kutokuwa na sera ya filamu, ambayo kwa mujibu wake ni muhimu sana pamoja na urasimu mkubwa uliopo.

Amesema mwekezaji wa filamu anapokuwa na nia ya kufanya kazi Tanzania huuliza apewe sera ya filamu inavyosema, lakini kwakuwa haipo hushindwa kuendelea na mpango wake.

“Akiona hivyo anajua kuwa biashara anayotaka kuifanya, haina ulinzi wa kile anachotaka kuwekeza pale, na hiyo inamfanya aondoke.” Anasema hiyo imetengeneza mwanya wa nchi jirani ikiwemo Kenya kunufaika.

“Wakenya wanayo tayari sera ya filamu. Kwahiyo unakuta wanapokelewa Kenya baadaye wanaingia Tanzania kutumia tu location, lakini kwa kutumia mgongo wa Kenya au Uganda.”

Ameongeza kuwa watengenezaji wa filamu nchini Marekani kwa sasa wanahitaji mandhari mpya kwaajili ya kazi zao na Tanzania imejaaliwa vivutio vingi lakini hakuna mazingira rafiki na wezeshi ya kuwavutia. Kuja kwao anasema, kungeitangaza nchini, kuingiza fedha za kigeni lakini pia tasnia ya nyumbani kuiba utaalamu toka kwao.

Mwakifamba amedai kuwa kikwazo kingine kilichopo Tanzania ni urasimu uliopo ukilinganisha na Uganda ambako wametengeneza mazingira rahisi sana. Amesema urasimu umekuwa changamoto kubwa hata kwenye kufanya video za muziki, kitu ambacho kimewafanya wasanii kukimbilia Afrika Kusini ambako hakuna mlolongo mrefu wa kupata vitu na mandhari.

Ametoa mfano kuwa yeye mwenyewe alikuwa na mradi wake na alienda Makumbusho ya taifa kuomba kutumia kitu toka kwao akini walimkatalia licha ya kuwa tayari kulipia na kuwaeleza kuwa kazi yake ingeitangaza Tanzania.

“Hata ule uzalendo sasa unapungua sababu mazingira yaliyowekwa kuna urasimu sana Tanzania kwenye masuala ya location. Hata filamu zetu ndio maana zinakosa uhalisia, ukitaka mahakama ni mtihani kupata, ukitaka gereza ni mtihani kupata, ukisema uvae sare za jeshi la polisi ni mtihani. Bongo pana kazi sana,” amesisitiza.

Hata hivyo Mwakifamba amesema wapo kwenye mchakato wa kuwa na sera ya filamu ambayo inaweza kuwa tayari mwaka huu.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents