Habari

LHRC yazindua kitabu cha uhuru wa kujieleza na kukusanyika Tanzania

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimezindua kitabu kidogo cha uchambuzi wa sheria zinazohusu uhuru wa kujieleza na uhuru wa kukusanyika nchini Tanzania.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinayofuraha kuzindua kitabu kidogo cha uchambuzi wa sheria zinazohusu uhuru wa kujieleza na uhuru wa kukusanyika nchini Tanzania. Kitabu hiki kimechambua Sheria ya Makosa ya Mtandaoni ya mwaka 2015, Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari ya mwaka 2016, Sheria ya Jeshi la Polisi na Huduma Saidizi ya mwaka, 2002 na Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa ya mwaka 2016. Ikumbukwe kwamba, sheria hizi ni miongoni mwa sheria zenye vifungu vinavyokandamiza uhuru wa kujieleza kama ilivyoelezwa na kuchambuliwa katika kitabu hiki.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimefanya uchambuzi wa sheria hizi kwa kuzingatia misingi ya uhuru wa kujieleza na kukusanyika kama iliyoainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977, Mikataba ya Kimataifa ikiwemo Azimio la Ulimwengu la Haki za Binadamu, 1948, Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na za Kisiasa, 1966 pamoja na Mkataba wa Kikanda wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu, 1981. Pia, kitabu kimezingatia mifano ya kuigwa kutoka katika sheria za nchi mbalimbali zinahusiana na uhuru wa kujieleza kama vile, Kenya, Uganda, Nigeria, Malawi na Uingereza. Kwa mfano, Katiba ya Jamhuri ya Ghana imeweka Sura maalamu ya Uhuru wa Vyombo vya Habari, mathalan ibara ya 162(4) ya Katiba ya Jamhuri ya Ghana, 1992 inaainisha kwamba, wahariri wa magazeti na taasisi nyingine za utangazaji hazitoingiliwa au kudhibitiwa na Serikali au kuadhibiwa au kusumbuliwa kwa maoni ya kihariri watakayoyatoa, mawazo yao au maudhui katika machapisho watakayoyatoa. Hivyo, ibara hii ni mfano mzuri wa kuigwa nchini Tanzania kuhakikisha Tasnia ya habari inalindwa pasipo kuingiliwa uhuru wake na serikali kama ilivyoainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Ghana, 1992.

Kitabu hiki kitakuwa msaada mkubwa kwa wachambuzi wa sheria, wanafunzi, wadau wa sekta ya habari, Asasi za Kiraia, watafiti wa sheria na Jamii nzima kwa ujumla. Hivyo, Kituo kinatoa wito na kuwaalika, mamlaka za Serikali, wadau binafsi pamoja na taasisi mbalimbali kupata nakala ya kitabu hiki bure na kusoma ili kukuza uelewa mpana juu ya dhana ya uhuru wa kujieleza na uhuru wa kukusanyika. Pia kwa wadau walio mbali na Dar es Salaam au watakaoshindwa kufika katika ofisi zetu hapa Dar es salaam wanaweza kupata kitabu hiki kupitia tovuti ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ambayo ni www.humanrights.or.tz.
Katika kukuza uhuru wa kujieleza nchini, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimefurahi pia kupata usajili rasmi wa kuzalisha na kusambaza jarida linalojulikana kama Mlinzi wa Haki na leo jarida hilo limezinduliwa rasmi na kupatikana kupitia mitandao ya kijamii.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinaamini kuwa uhuru wa kujieleza na uhuru wa kukusanyika ni msingi mkuu wa maendeleo katika jamii yoyote ile. Tunatoa rai kwa mamlaka za Serikali, taasisi za dini, asasi za kiraia na jamii kwa ujumla kukuza na kulinda uhuru wa kujieleza na uhuru wa kukusanyika nchini.

Bi. Anna Henga (Wakili)
Mkurugenzi Mtendaji
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents