Soka saa 24!

Lini wasanii wataanza kusherehekea idadi ya album walizouza kama wanavyosherehea views za Youtube?

Huko nyuma, ni wasanii wachache sana walikuwa na uwezo wa kufikisha views milioni moja kwenye mtandao wa Youtube kwa hata kipindi cha mwezi mzima.

Si mchezo ati.. Kwa msanii kama Diamond au Alikiba kutokana na nguvu zao na kuwa na kundi kubwa la mashabiki nyuma, views milioni moja waliweza kuzifikia ndani ya muda mfupi. Mfano, Salome ya Diamond ilifikisha views milioni 1 ndani ya siku mbili.

Lakini sasa mambo yameanza kubadilika kidogo. Darassa na Mwana FA wamefikisha views milioni 1 ndani ya wiki mbili kwa nyimbo zao Muziki na Dume Suruali. Si kitu cha mchezo mchezo. Kupata views nyingi ni ishara ya ukubwa na wasanii wana haki ya kushangilia.

Na ni ishara kwamba muziki wa Tanzania una nguvu sana. Na ndio maana utashangaa kuwa Salome ya Diamond ambayo leo hii ina views zaidi ya milioni 10 tangu itoke, ndio video ya muziki iliyoangaliwa zaidi nchini Kenya. Yaani imeizidi hadi Work ya Rihanna na Drake. Ni jambo kubwa sana hili.

Lakini najiuliza tu hapa, vipi siku moja wasanii wa Tanzania wakaanza kusherehekea idadi ya nakala za album walizouza kama wanavyosherehea views leo? Kwa Marekani na nchi zilizoendelea, nakala za album wanazouza ndio kitu wanachosherehekea, na actually ndio kigezo kinachotumika kupanga nyimbo kwenye chati za Billboard, sio views za Youtube.

Kwa wasanii wakubwa wa huko, views za Youtube si kitu wanachoshangilia hata! Ni kitu cha kawaida mno!
Kwao, msanii akiuza kopi milioni moja (platinum) za album yake, kitu ambacho nao si rahisi tu, ni habari njema anayoweza kushare na mashabiki wake kwenye mitandao ya kijamii.

Huwezi kuona Drake akifurahia video yake kufikisha views milioni 100 Youtube, bali utaona akifurahia album yake kuuza nakala milioni kadhaa kama ambavyo juzi alisherehekea album yake Views kupata platinum nne.

Kwenye muziki, album ndio hatua ya juu zaidi ambayo msanii anapaswa kuifikia. Utaheshimika zaidi kwa idadi ya album ambazo umeuza, na sio kwa views ambazo video yako imevutia. Ni kwasababu, zipo video za hovyo hovyo tu kwenye mtandao huo ambazo ni views za hatari.

Album! album! album! ndio kipimo cha ujuzi au ubovu wa msanii, tukubali au tukatae. Hivyo, pamoja na visingizio vyote, ili muziki wetu ukue zaidi, lazima watu waanze tena kutoa album. Hapo ndipo tutakuwa na kipimo halisi cha ukubwa wa wasanii wetu.

Badala ya kuona wakiendelea kufurahia views, tunataka tuone wakifurahia kuuza walau kopi 10,000 au 5,000 tu za album zao katika wiki ya kwanza. Inawezekana, kama wakiamua.

Related Articles

Back to top button
Bongo5

FREE
VIEW