Habari

Lowassa nje kamati za Bunge

SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Samuel Sitta, amemwacha nje ya kamati za kudumu za Bunge hilo, Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, kwa madai ya kutojaza fomu.

na Irene Mark

 

 

 

SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Samuel Sitta, amemwacha nje ya kamati za kudumu za Bunge hilo, Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, kwa madai ya kutojaza fomu. Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima umebaini kwamba, Lowassa ni miongoni mwa wabunge wasio na madaraka serikalini kwa sasa, ambao wameachwa nje ya kamati zote 17 zilizotangazwa na Spika Sitta wiki iliyopita.

 

Taarifa ambazo gazeti hili limezipata kutoka ndani ya Bunge zinaeleza kuwa kwa kawaida wabunge wote wasio mawaziri wanapaswa kuwa wajumbe katika moja ya kamati hizo za kudumu na kabla ya kufanya hivyo hutakiwa kuomba kwa kujaza fomu maalumu.

 

Kwa mujibu wa habari hizo, kujaza au kutojaza fomu kwa mbunge bado hakuwezi kumzuia spika kumtea mbunge katika kamati yoyote ambayo anaamini mhusika atafaa kutokana na uzoefu au utaalamu alionao katika eneo husika.

 

Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu jana jioni, kuhusu kutokuwamo kwa Lowassa katika orodha ya wajumbe wanaounda kamati hizo za Bunge, Sitta alisema wakati wabunge wengine wanajaza fomu hizo, Lowassa alikuwa waziri mkuu, hivyo hakutakiwa kujaza.

 

“Ni kwa sababu wakati wabunge wengine wanajaza fomu katika mkutano ule za kuomba kuwa wajumbe wa kamati mbalimbali, yeye (Lowassa) alikuwa waziri mkuu hivyo hakustahili kuzijaza.

 

…Sasa, yalipotokea ghafla akajiuzulu, akaenda jimboni kwake, hakuweza kujaza. Baada ya hapo aliporudi Bunge nalo likawa limemaliza muda wake.

 

Mmmh, hakuna tatizo lakini anaweza kujaza wakati wa mkutano ujao,” alisema Sitta na kumaliza mazungumzo hayo kwa kukata simu.

 

Aidha, Februari 7, mwaka huu wakati wa kikao cha Bunge, Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, alitangaza kujiuzulu baada ya Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge iliyopewa dhamana ya kuchunguza mkataba tata wa kuzalisha umeme wa Kampuni ya Richmond Development uliodaiwa kugubikwa na vitendo vya rushwa na ufisadi, Dk. Harrison Mwakyembe, kumtaka awajibike.

 

Lowassa, alijiuzulu katika nafasi ya uwaziri mkuu baada ya kuhusishwa na kashfa ya ufisadi kwenye mkataba dhalimu unaliolisababishia taifa hasara ya sh bilioni 172.9.

 

Kutokana na mkataba huo, taifa linaendelea kupata hasara ya sh milioni 152 kila siku kwa kuilipa Kampuni ya Dowans Holdings iliyorithi mkataba huo, mapema mwaka jana.

 

Kwa mujibu wa kanuni za Bunge, waziri yeyote haruhusiwi kuwa mjumbe wa kamati za Bunge, kwa kuwa ni mwakilishi wa Serikali.

 

Hata hivyo wakati, Sitta akisema hayo, baadhi ya waliokuwa mawaziri waliotangaza kujiuzulu pamoja na Lowassa ambao ni Nazir Karamagi na Ibrahim Msabaha, wamo kwenye kamati mbalimbali za Bunge hilo.

 

Kama hiyo haitoshi, mbali ya hao wabunge wengine kadhaa waliokuwa mawaziri kabla ya mabadiliko ya hivi karibuni na baadaye wakaachwa nje ya Baraza jipya la Mawaziri lililoteuliwa Februari 12 mwaka huu, wamo ndani ya kamati za kudumu za Bunge ambazo leo zinatarajia kuchagua wenyeviti wake.

 

Baadhi yao na kamati zao kwenye mabano ni Kingunge Ngombale-Mwiru (Kanuni za Bunge), Anthony Diallo (Fedha na Uchumi), Nazir Karamagi, Basil Mramba, Joseph Mungai na Bakari Mwapachu (Viwanda na Biashara).

 

Wengine ni Dk. Ibrahim Msabaha (Ulinzi na Usalama), Zakia Meghji (Ardhi, Maliasili na Mazingira), Charles Mlingwa (Kilimo, Mifugo na Maji), Daniel Nswanzugwanko (Nishati na Madini), Zabein Mhita na Juma Ngasongwa (Hesabu za Serikali za Mitaa).

 

Kuwamo kwa wabunge hao, kunaifanya hoja ya Sitta kusema kuwa Lowassa hakupata fursa ya kujaza fomu hizo kuibua maswali.

 

Hata hivyo habari zinaeleza kwamba, Lowassa mwenyewe pamoja na kuwa na muda wa kutosha kujaza fomu, hakufanya hivyo, huku Spika Sitta ambaye kimsingi anayo mamlaka ya kumteua katika moja ya kamati naye akiamua kuliacha kando jina la waziri mkuu huyo aliyejiuzulu.

 

Wakati hilo likitokea kwa Lowassa, taarifa nyingine zinaonyesha kuwa tayari kumeibuka mvutano mkubwa wa kimakundi katika uteuzi wa wenyeviti wa kamati hizo.

 

Kuanza kutumika kwa kanuni mpya za Bunge kifungu cha 111 (10) kinachoainisha kwamba, kamati tatu za Bunge zinatakiwa kutoa wenyeviti wake katika kambi ya upinzani, kumeanza kuleta wasiwasi wa kuibuka kwa mgawanyiko.

 

Katika hali hiyo, baadhi ya wabunge wa kambi ya upinzani leo wanatarajia kuchuana vikali kuwania nafasi ya uenyekiti wa kamati tatu za Bunge ambazo ni Hesabu za Serikali, Hesabu za Mashirika ya Umma na ile ya Hesabu za Serikali za Mitaa.

 

Kamati inayoelezwa kuwa na upinzani mkali kwa upande wa nafasi hiyo ni ile ya Hesabu za Mashirika ya Umma, ambapo Mwadini Jecha na Mwanawetu Zarafi (wote wa CUF), Halima Mdee na Kabwe Zitto (CHADEMA), watachuana.

 

Habari ambazo Tanzania Daima ilizipata jana jioni zinaeleza kuwa, wakati tayari Zitto alikuwa ameshaanza kuonyesha dalili za kushinda, mwenzake Jecha naye alionekana kutoa upinzani mkali kwake.

 

Katika Kamati ya Hesabu za Serikali, watakaochuana ni John Cheyo (UDP), Seveline Mwijage na Muhammmad Sanya (CUF) wakati CHADEMA ikiwakilishwa na Mhonga Said.

 

Aidha, Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa inawakilishwa na Ania Chaurembo (CUF), Grace Kiwelu na Dk. Willibrod Slaa (CHADEMA).

 

Kuundwa kwa kamati mpya za Bunge kunatokana na mabadiliko ya kanuni, hivyo hata kuwapo kwa waliokuwa mawaziri kwenye baadhi ya kamati hizo kumesababishwa na kuvunjika kwa Baraza la Mawaziri.

 

 

 

 

 

Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents