Habari

Lukuvi kula sahani moja na maafisa waliouza eneo la makaburi Dar

Waziri wa ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi, William Lukuvi, ameamua kubatilisha hati tatu za viwanja ambavyo vimetolewa na watumishi wasio waaminifu wa serikali katika eneo la Kinyerezi jijini Dar es Salaam, lililokuwa likitumika kwa ajili ya makaburi na kuuzwa kinyume cha sheria.

lukuvi_0_o-1

Ameyasema hayo jijini Dar wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema kuwa watumishi hao wamediriki kuuza makaburi ambayo yametumiwa tangu mwaka 1962 na kwa sasa yapo zaidi ya mia tano.

Amedai watu hao hawana hofu ya Mungu hivyo kufukuzwa ni halali yao.

“Watumishi wa wizara ya ardhi wameipima ardhi na kuigawa na kujimilikisha, na nimeshuhudia kwamba eneo lile kimsingi lilipangwa kama eneo la mazishi, baadaye kwa namna ambayo haijulikani limepewa viwanja namba 213,215,217 block D Kinyerezi na likamilikishwa kwa watu, na nimeshuhudia kwamba hata wakati linamilikishwa lilikuwa na makaburi tayari ambayo yamezika watu zaidi ya mia tano,” alisema.

“Nimesoma mwenyewe pale kaburi la kwanza ni la mwaka 1962, hili jambo halivumiliki na serikali ya awamu ya tano haiwezi kuvumilia jambo hili,” alionya Lukuvi.

“Kuona kwamba baadhi ya maafisa ardhi wamefikia kiwango sasa kuyauza maeneo ambayo yamezikwa binadamu, hawa watu wamefikia hali ambayo hata Mungu hawamuogopi. Kwahiyo baada ya kuona kero kwa wananchi nimeamua kumuagiza kamishna wa kanda ya Dar es Salaam, afanye identification kwa maana kwamba viwanja vile vifutwe leo na viondolewe kwenye daftari la viwanja vilivyosajiliwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwasababu vilikuwa batili kuanzia siku ya kwanza vilivyotolewa.”

“Lakini pili nimemuagiza kamishna anitamkie kwenye orodha ya kwenye faili, nani alihusika katika kupima, nani alihusika kuvipa namba viwanja akijua kabisa linaonyesha yale ni makaburi na site pale kama alipima aliona ni makaburi, aliyehusika kugawa vile viwanja mpaka kuidhinisha hati nataka kuwaona,” alifafanua.

“Hawa ni watu wasio muogopa Mungu kama serikali lazima wafukuzwe, ni kufuatilia kujua kwamba ni watu gani waliohusika, pia wale waliomilikishwa viwanja hivi waje hapa ofisini, nataka nizungumze kama watanzania kwa upuuzi waliofanya pale. Nadhani hawaogopi kuna maiti 1000 unamilikishwa na bado unasema nitaondoa maiti wale, unasema uchimbue maiti pale ukazike mahali pengine lazima ni watu ambao hawana ubinadamu! Kwahiyo naomba waje ili nizungumze nao. Lakini kwa ufupi ni kwamba viwanja vile vitolewe, na nimeagiza kwamba lile eneo lirudi, muhimu kabisa ni eneo la huduma ya mazishi watu wanafikiri maeneo kama hayo si maeneo, binadamu wote tunaishi katika mazingira haya lakini mwisho wetu lazima tutazikwa.”

BY: EMMY MWAIPOPO

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents