Maambukizi ya ukimwi nchini yapungua

Asilimia 93 ya Watanzania hawajaambukizwa virusi vya ukimwi na kwamba jitihada zaidi zinaelekezwa katika kuwajali asilimia saba ya wale ambao tayari wameshaambukizwa virusi hivyo ili waweze kupata huduma zinazostahili

Na Job Ndomba

Asilimia 93 ya Watanzania hawajaambukizwa virusi vya ukimwi na kwamba jitihada zaidi zinaelekezwa katika kuwajali asilimia saba ya wale ambao tayari wameshaambukizwa virusi hivyo ili waweze kupata huduma zinazostahili na hatimaye kuwapunguzia makali ya ugonjwa huo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge), Bw. Philip Marmo, amesema hali ya maambukizi ya virusi vya ukimwi nchini inazidi kupungua na kutia moyo.

“Serikali inatarajia kutoa takwimu mpya ya maambukizi ya ukimwi. Lakini kwa sasa, asilimia 93 ya Watanzania hawajaambukizwa na tunafanya jitihada za dhati za kuijali asilimia saba ya Watanzania wanaoishi na virusi vya ukimwi,“ akasema Bw.Marmo.

Bw. Marmo amesema udhibiti wa ukimwi ni changamoto kubwa ambayo inahitaji ushirikishwaji wa kila sekta na vikundi mbalimbali ili jamii iweze kujitambua kuhusu janga la Ukimwi.

Amesema takwimu za ukimwi nchini za mwaka 2007/2008 zitatolewa na viongozi wa juu Serikalini na tayari zimeshakamilika.

Aidha, amesema kuwa Tanzania bila ukimwi inawezekana, kwani tayari kuna mipango ya kuhakikisha watoto wote wanaozaliwa Tanzania wanazaliwa bila ukimwi na hivyo kuwa na kizazi kipya kisichokuwa na maambukizi.

Ameongeza kuwa jitihada za kupunguza zaidi kiasi cha maambukizi nchini pamoja na jitihada za kuwalinda hao asilimia 93 wasiokuwa na maambukizi ya virusi vya ukimwi ili wasiambukizwe.

Sanjari na hayo Bw. Marmo amesema kuwa Serikali itahakikisha kuwa dawa za kupunguza makali ya ukimwi ‘ARVs’ zinamfikia kila mmoja anayezihitaji.

Amesema hadi kufikia Februari 2008 taarifa zinaonesha kuwa Watanzania 143,451 walikuwa wakipata dawa za kupunguza makali ya ukimwi.

Hata hivyo imesema kuwa itaendelea na jitihada za kuongeza vituo vya kupimia ukimwi VCT ili huduma hiyo iwe jirani zaidi na wananchi.

Aidha amesema kuwa Serikali itahakikisha kwa kila namna fedha zinazotolewa kwa ajili ya masuala ya Ukimwi inazdhibitiwa ipasavyo na ikiwezezakana itamtumia mdhibiti mkuu wa hesabu za Serikali kufanya ukaguzi.

Bw. Marmo ameongeza kuwa jamii itoe taarifa Serikalini iwapo itabaini kuwepo kwa ubadhilifu wa fedha katika taasisi zinazoshughulika na udhibiti wa ukimwi.


 


Source: Alasiri

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents