Habari

Mabilioni yapotea kwenye mavuno ya magogo, asali

SERIKALI imekuwa ikipoteza jumla ya Dola za Marekani milioni 58 (sawa na Sh bilioni 86) kwa mwaka kutokana na makusanyo ya chini ya kiwango ya mapato ya misitu na nyuki kwenye halmashauri mbali mbali nchini, wabunge wameelezwa.

Halima Mlacha, Dodoma


SERIKALI imekuwa ikipoteza jumla ya Dola za Marekani milioni 58 (sawa na Sh bilioni 86) kwa mwaka kutokana na makusanyo ya chini ya kiwango ya mapato ya misitu na nyuki kwenye halmashauri mbali mbali nchini, wabunge wameelezwa.


Kwa mujibu wa utafiti huru ulioidhinishwa na Wizara ya Maliasili na Utalii, uliofanywa kwa kushirikiana na Mtandao wa Kufuatilia Masuala ya Misitu na Wanyama (TRAFFIC), upungufu huo umetokana na mazao hayo kuuzwa kwa bei ya chini ikilinganishwa na soko la kimataifa.


Akiwasilisha ripoti ya utafiti huo jana mbele ya wabunge, Naibu Mkurugenzi wa mtandao huo, Simon Milledge, alisema pia upotevu huo umetokana na kutokuwapo kwa taarifa sahihi za mizigo ya magogo wakati wa kutozwa ushuru.


“Hali hii imesababisha nchi kukusanya asilimia 10 tu ya mapato ambayo ingeliyapata kutokana na kuuza mbao na mazao ya misitu nchi za nje,” alisema Milledge.


Alisema pamoja na hayo pia tatizo la uvunaji holela wa misitu na mazao yake limekuwa likichangia kwa kiasi kikubwa upungufu wa makusanyo chini ya kiwango hali ambayo pia imekuwa haiwanufaishi wananchi wa eneo husika.


“Wananchi wamekuwa hawana mamlaka na raslimali walizo nazo na mbaya zaidi wamekuwa wakilipwa kiwango cha Sh 1,000 hadi 1,800 kwa kazi ya ukataji magogo na miti,” alisema.
Alisema kwa mujibu wa utafiti huo, mapungufu katika utawala yameainishwa na wadau wengi kama kikwazo kikubwa katika utekelezwaji wa sheria na sera za Idara ya Misitu. Alisema wamebaini kuwa aina 27 ya miti yenye sifa za kutoa mbao nzuri za biashara ilikuwa inakatwa katika maeneo ya ukanda wa Pwani kusini mwa Tanzania, baadhi ya miti hiyo ni mpangapanga, mkuruti, msekeseke, mninga, mkongo, mhama na mtondolo.
Wakichangia maoni yao juu ya utafiti huo, baadhi ya wabunge walimpongeza Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe kwa kuchukua hatua za mwanzo za kurekebisha tatizo hilo la misitu katika idara husika.


Mbunge wa Lulindi, Sulemani Kumchaya (CCM), alisema pamoja na hatua hizo za Maghembe kuna haja ya wizara husika kuunda mikakati thabiti ya kuhakikisha kuwa sheria za misitu zinafuatwa.


“Katika kulitekeleza hili tunakuomba Waziri wewe ndio uwe msimamizi mkubwa na tunakuomba pia uanze kufanya mabadiliko ya kiutendaji katika idara hii,” alisema Kumchaya.
Alisema ni lazima uundwe mpango mahsusi wa kuwaondoa watendaji wote wenye vichwa vikubwa na wanaoendekeza rushwa hali ambayo inawanyima haki wananchi na kuliletea taifa hasara. “Tutakulinda tunajua uwezo unao profesa,” aliongeza.
Akitoa mchango wake mbunge wa Tabora Mjini Siraju Kaboyonga (CCM), alimtaka Maghembe kusimamisha uuzwaji wa magogo nje ya nchi na badala yake uanzishwe utaratibu wa kuanzisha viwanda vya mazao ya misitu nchini.


Pia alitaka utaratibu wa zamani wa kusafirisha mazao ya biashara nje ya nchi ambao ulikuwa ukishirikisha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) urejeshwe.


Kwa upande wake Maghembe alisema misitu ina mchango mkubwa kwa maisha ya binadamu ikiwa ni pamoja na kuwa chanzo cha hali ya hewa salama.
Alisema kukatwa hovyo kwake ni hasara kubwa na hatari kwa maisha ya binadamu na ndio maana hivi karibuni kumekuwapo na vimbunga vya ajabu ambavyo vimeleta madhara makubwa.


“Sasa nawaambia hivi pamoja na kulalamikia kupanda kwa bei ya magogo tunaanzisha operesheni kubwa ya kuwakamata wanaovuna magogo na kukata misitu hovyo, kuwachukulia hatua na kuwatoza faini na idadi ya fedha tutawatajia,” alisema Maghembe.


Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents