Machale yamcheza Kandoro

Bw/ Abbas KandoroMkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Abas Kandoro, amestushwa na “usanii” wa mikataba ya ujenzi wa barabara kadhaa za manispaa za Jiji lake na kueleza kuwa kuanzia sasa ataripoti kwenye Taasisi ya kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Abas Kandoro, amestushwa na “usanii” wa mikataba ya ujenzi wa barabara kadhaa za manispaa za Jiji lake na kueleza kuwa kuanzia sasa ataripoti kwenye Taasisi ya kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini, TAKUKURU ili ichunguze mikataba hiyo baina ya Manispaa na makandarasi wanaopata tenda hizo.

 

Aidha, Kandoro amesema ana hofu juu ya usahihi wa mikataba hiyo kutokana na viwango duni vya ujenzi wa barabara, tofauti na viwango vinavyostahili ambapo akasema hali hiyo husababisha upotevu wa fedha nyingi huku ujenzi ukiwa mbovu.

 

Bw. Kandoro ameyasema hayo wakati alipokuwa akizungumza na Wajumbe wa Kikao cha Bodi ya barabara Mkoa wa Dar , kilichoandaliwa na TANROADS na ambacho kilikuwa kikijadili uboreshaji wa miundombinu ya Jiji.

 

Mkuu huyo wa Mkoa alifikia hatua hiyo kutokana na kustushwa na kitendo kilichofanywa na Halmashauri ya Ilala kwa kumpa tenda ya ujenzi wa barabara ya Mtaa wa Lindi na Gerezani Mkandarasi mmoja pasipo kuandikishiana mkataba wowote ule kwa kazi hiyo.

 

Bw. Kandoro akasema mkandarasi huyo amepewa tenda ya kufanya kazi, lakini hakuna sehemu ya mkataba uliosainiwa kati yake na Manispaa.

 

“Je, malipo ya mkandarasi huyu yakoje? Nadhani kuna ubabaishaji umepita hapo,“ akasema Bw. Kandoro.

 

Akaongeza kuwa licha ya mkandarasi huyo kufanya kazi bila mkataba, pia barabara hizo hazina viwango vya kuridhisha ambapo mpaka sasa, zimeshakuwa na mashimo wakati hata mwaka hazijamaliza tangu zikamilike.

 

“Inawezekana pia kwamba kuna uzembe unaofanywa na wahandisi wetu kwa kukubali kuburuzwa na makandarasi wao ama kukaa ofisini na si kuwajibika katika sehemu zao za kazi… au fedha hizo zinatafunwa. Yote yanawezekana,“ akasema Mkuu huyo.

 

Akasema anashtushwa na taarifa zinazotolewa kuhusu utendaji kazi wa wakandarasi kwa kuonesha barabara nyingi zimejengwa, lakini barabara zote ni mbovu na kamwe hazidumu.

 

Naye Mbunge wa Jimbo la Temeke Bw. Abbas Mtemvu, aliomba wajumbe wa kikao hicho kumsimamisha kazi mara moja mkandarasi ambaye alipewa tenda ya kujenga barabara ya Tandika Devis Corner kutokiana na kitendo chake cha kutomaliza kazi kwa haraka.

 

Bw. Mtemvu akasema kuwa kazi inayofanywa na mkandarasi huyo hairidhishi na amekuwa akitumia muda mwingi katika ujenzi huo na hadi sasa hakuna maendeleo ya maana.

 

“Cha kusikitisha zaidi tulipofika katika eneo lake la ufanyaji kazi na baadhi ya wajumbe, mkandarasi huyo alitukimbia kwa kujua hana cha kutueleza… hata alipokuwa akipigiwa simu, hakutaka kupokea kwa kuogopa maswali yetu,“ akasema Bw. Mtemvu .

 

 

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents