Habari

Macho na masikio ya waumini wa KKKT yahamia mkoani Arusha

Macho na masikio ya waumini wote wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), yamehamia mkoani Arusha ambako kesho Agosti 23, 2019 wanatarajia kupata Mkuu wa Kanisa hilo atakayeliongoza kwa kipindi cha miaka minne ijayo.

Mkutano Mkuu wa kanisa hilo, ulianza juzi katika Chuo Kikuu cha kanisa hilo cha Makumira mkoani Arusha.

Licha ya kuwa Askofu Dkt. Fredrick Shoo, ambaye kwa sasa ndiye mkuu wa kanisa hilo, Anapewa nafasi kubwa ya kumalizia miaka mingine minne ya kipindi cha pili, bado kuna upinzani mkubwa kutokea kwa wagombea wenzake.

Baadhi ya maaskofu wanaotajwa kuchuana na Dkt. Shoo ni Askofu Dayosisi ya Kaskazini Magharibi, Dkt. Abednego Keshomshahara, Askofu wa Dayosisi ya Iringa, Blaston Gavile na Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dkt. Alex Malasusa.

Dkt. Shoo alichaguliwa Agosti 2015 baada ya kuwashinda maaskofu wenzake wawili ambao ni Dkt. Stephen Munga wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki na Askofu Charles Mjema wa Dayosisi ya Pare.

Kwenye uchaguzi huo, Dkt. Shoo alipata kura 153, huku Dkt. Munga akipata kura 67, ikiwa ni baada ya kurudiwa mara tatu kutokana na mshindi kutopata zaidi ya theluthi mbili ya kura zote.

Katika kanuni za uchaguzi za KKKT zinasema kuwa mshindi atapatikana kwa kupata kura zisizopungua theluthi mbili ya zote zilizopigwa na iwapo mshindi hatapatikana katika duru la kwanza, majina mawili yaliyopata kura nyingi ndiyo yatakayopigiwa tena kura.

Kiongozi wa Kanisa akimaliza muhula wake wa kwanza wa miaka minne, hupewa nafasi nyingine ya kumaliza muhula wa pili wa miaka minne.

Akizungumzia uchaguzi huo, Jana Agosti 21, 2019 Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini Kati, Dkt. Solomon Masangwa, asema wajumbe wanapaswa kumuomba Mungu awape kiongozi anayependeza moyo wa Mungu.

“Bado hatujafikia ajenda ya uchaguzi, ila wajumbe wa mkutano tunapaswa kumuomba Mungu atupe kiongozi anayeupendeza moyo wa Mungu, Kuupendeza moyo wa Mungu ni kuwa na upendo kwa watu wake na ukombozi kwa watu wake, Mungu hapendi tupotee lakini tufikie ustawi mzuri kiroho, kiuchumi, kimwili, kisiasa pamoja na kijamii,” amesema Dkt. Masangwa.

Juzi wakati wa ufunguzi wa mkutano huo wa 20, Dkt. Shoo aliwataka Wakristo kutenda kwa upendo na kuacha kuwahukumu wengine ikiwamo kuwafanyia kile wasichopenda wao kufanyiwa zinazozuia Wakristo wasiishi imani yao ipasavyo. Hivyo aliwataka wasiyumbishwe bali wawe imara kuishuhudia imani na kuwa huru katika Yesu aliyewaita.

Lengo la Mkutano Mkuu wa 20 ni kuangalia jinsi talivyoenda pamoja na jinsi tutakavyoendelea mbele pamoja. Kanisa ni mahali watu wanaweza kuona neema ya Mungu na kuishi kwa umoja katika kulichunga kundi, kuaminiana na kusaidiana hata katika tofauti zetu za kieneo, mapokeo, na misimamo. Suluhisho la migogoro ni kupendana, kushauriana ili kusonga mbele. Waefeso 4 inasema wala tusimpe ibilisi nafasi. Tuenende kama wito tulioitiwa ulivyo katika upendo na umoja katika kifungo cha amani.“amesema Dkt.Shoo na kusisitiza.

Niwaombe viongozi na washarika kwa ujumla kuwa makini na mafundisho potofu kutoka kwa yeyote, bali kudumu katika kweli ya Mungu na tusiwe watumwa wa ukanda na siasa, bali tuwe imara kutenda lililo jema bila kulipa kisasi,“alisema Askofu Shoo.

Chanzo: Gazeti Mtanzania

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents