Burudani

Madawa ya Kulevya yanavyoiondoa sifa ya wasanii kuwa vioo vya jamii

Kuna kauli inayosema ‘msanii ni kioo cha jamii’ lakini kwa sasa imeanza kubadilika na kuonekana ni kama matatizo kwa jamii. Kwa sasa wasanii wetu wa Bongo na mastaa wengine wanakumbwa zaidi na kashfa ya utumiaji wa madawa ya kulevya.

Japo wengi wamekuwa wakitumia kwa kujificha lakini hutakiwi kusahau, mficha maradhi kifo humuumbua. Tumeona kilichotokea kwa Chid Benz, Ray C, Nando, Ferooz na sasa jipya limeibuka kwa Young Dee baada ya kukiri kuachana na matumizi hayo miezi michache iliyopita lakini sasa amedaiwa kurudia tena.

Watu wamekuwa wakilaumu kwa hiki kinachotokea lakini ukweli ni kuwa ukitaka kuachana na matumizi hayo ni lazima kuwe na utayari kutoka moyoni wa mtumiaji mwenyewe bila ya kulazimishwa na mtu yoyote, hapo ndipo jambo hilo litakuwa rahisi kufanikiwa na kulimaliza kwa mtumiaji ila vinginevyo ‘utakuwa unampigia mbuzi giter’.

Shukrani za dhati ziwaendee wadau mbalimbali waliojitolea kuwasaidia baadhi ya wasanii kutoka kwenye janga hilo akiwemo Rais mstaafu kakaya Kiwete, Kalapina, Ruge Mutahaba, Babu Tale, Maximillian Rioba, Witness aka Kibonge Mwepesi na wengine wengi

Hakuna aliyetegemea kusikia hata kwa kuona leo hii Ferooz akitumia madawa ya kulevya kwakuwa alikuwa ni mmoja kati ya wasanii waliojitengenezea heshima kubwa nchini kutokana na nyimbo zake zenye ujumbe ikiwemo ‘Starehe’ ambayo ilimgusa mpaka Rais mstaafu Benjamin Mkapa. Lakini leo ni mmoja kati ya wasanii anayewatoa machozi mashabiki kwa kuwa miongoni mwa watumiaji wa madawa ya kulevya – hakika mganga hajigangi.

Ni imani yangu kubwa muda si mrefu tutasikia tena kuna msanii mwingine ameibuka anatumia ‘unga’ kwa kuwa wengi wao wamekuwa wakitumia kwa siri lakini ikumbukwe kuwa tunatakiwa kujifunza kutoka na makosa ya wengine kwa kile tunachokiona, ‘ukiona mwenzako ananyolewa basi wewe tia maji’.

Tumuombe Mungu awasaidie kuwaonyesha njia nzuri na kuwatoa wasanii wetu wote waliopo kwenye giza nene la utumiaji wa madawa ya kulevya kwa kuwarudisha kwenye hali zao kama za mwanzo na kuwafunga wengine wasiotumia wasiweze kuingia kwenye janga hilo zito.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents