Habari

Maelezo ya Mhe. Zitto mbele ya Kamati ya Bunge

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe amefikishwa mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwaajili ya kuhojiwa kwa kutoa kauli za kulidhalilisha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Haya ndio baadhi ya maelezo aliyoyatoa Mhe. Zitto katika kamati hiyo:

Part 1:
Uhuru Wangu wa Maoni Ulilenga Kulinda Uhuru, Haki, Hadhi na Heshima ya Bunge [Maelezo ya ndugu Kabwe Z. Ruyagwa Zitto (Mb), mbele ya Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge]. Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati,
Mnano tarehe 13 Septemba, 2017 nilipata wito wa kufika mbele ya Kamati yako kutoa ushahidi wa masuala mbalimbali. Nilipata wito husika saa nane na dakika 40 mchana, nikitakiwa kufika mbele ya kamati yako, hapa Dodoma saa saba mchana siku hiyo hiyo.
Nililetewa wito huo na RCO Mkoa wa Kigoma nikiwa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani la Manispaa ya Kigoma Ujiji. Sikuweza kufika, isingewezekana katika mazingira hayo niwe na uwezo wa kusafiri kutoka Kigoma na kufika mbele ya kamati yako hapa Dodoma. Kwanza muda ulishapita, lakini hata taratibu za kiusafiri pamoja na umbali kati ya Kigoma na Dodoma hazikuwezesha Jambo hilo.
Siku iliyofuata nilipata ajali, ambapo nyumba yangu iliwaka moto wakati nikiwa njiani kwenda Nairobi kumuona mbunge mwenzetu mgonjwa, ndugu Tundu Lissu. Jana tarehe Septemba 20, 2017 nikiwa natokea Kigoma ili kuja kwenye Kamati nilikamatwa na Polisi ili kufikishwa mbele ya Kamati yako.
Leo nimefika mbele yenu na nitajibu wito wenu kama ifuatavyo:
A: Kwamba maoni yangu kwenye mtandao wa Twitter kuwa “Bunge siku hizi ni Idara ya Tawi la Utawala” yanadhalilisha Mhimili Wa Bunge.
Maneno hayo ni ya kwangu na nimeyatoa kama raia wa Tanzania. Ninaamini kwa dhati kuwa Bunge la Kumi na Moja limekuwa likifanya kazi kwa kuingiliwa na Serikali chini ya ndugu Rais John Pombe Magufuli.
Maneno na vitendo vya Rais yanaashiria kuwa Bunge halina Uhuru wake, na mimi kama Mbunge nina wajibu wa kuonyesha kutopendezwa kwangu na hali hiyo. Nina mifano kumi (10) kuthibitisha maelezo yangu hayo kama ifuatavyo:
1. Kuzuiwa kwa “Bunge Live” kwa kisingizio cha kupunguza gharama za uendeshaji wa mhimili wa Bunge, wakati Mikutano yote ya mhimili wa Serikali, hasa ya Rais ikirushwa live (mubashara) ni dalili ya wazi ya kufifisha sauti ya Bunge na kupandisha sauti ya serikali. Hata vituo binafsi ambavyo vilipanga kurusha bunge Live bila malipo (na hivyo kutokuwa na gharama) vilizuiwa, lakini vinarusha Live mikutano ya Rais.

Part two.
2. Kitendo cha Uongozi wa Bunge kurudisha serikalini shilingi Bilioni 6 bila ridhaa ya wabunge kwa kisingizio kwamba zimebaki kutokana na kubana matumizi. Hii ni dalili ya wazi ya Bunge “kujipendekeza” kwa serikali. Wakati Uongozi wa Bunge ukirejesha kiwango hicho cha Fedha, kuna taarifa kwamba kamati nyingi za Bunge zinashindwa kutekeleza wajibu wake kwa sababu ya ukata.
3. Maelekezo ya mhimili wa Serikali kwa mhimili wa Bunge, kupitia maagizo ya Rais Magufuli kwa Spika Ndugai kuwa “Awashughulikie wabunge” (kwa kuwafukuza bungeni) aliowaita “waropokaji” ili waje wazungumze nje ya Bunge na yeye Rais (Serikali) apate nafasi ya kuwashughulikia. Kauli hii ya Rais aliyoitoa wakati akipokea Ripoti ya Prof. Osoro kuhusu Mikataba ya Madini, Juni 12, 2017 inaonyesha picha iliyo dhahiri kuwa Bunge linapokea Maelekezo kutoka Serikalini ya kuwadhibiti wabunge hasa wanaoiwajibisha serikali. Na hatuwahi kuliona Bunge likiyakana maelekezo hayo ya Rais kwa Spika.
4. Kitendo cha Bunge kuhariri hotuba za kambi ya upinzani kwa kushinikiza kuondolewa kwa vipengele vinavyoikosoa Serikali. Mathalani, Wakati wa Bunge la Bajeti, hotuba ya Msemaji wa Kambi ya upinzani wa Wizara ya Mambo ya Ndani, ndugu Godbless Lema, iliamriwa kuondolewa maneno yanayohusu kashfa ya Mkataba wa Lugumi, kumhusisha Rais na kuuzwa kwa nyumba za Serikali, Mauaji ya wanasiasa, pamoja na Bunge kulinda wahalifu.
5. Kauli ya Rais Magufuli ya Novemba 4, 2016 akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari kuwa “mzizi wa mhimili wa serikali ni mrefu zaidi kuliko mihimili mingine” mara baada ya kuulizwa juu ya matumizi ya Serikali Nje ya Bajeti iliyoidhinishwa na bunge, unaonyesha dhahiri fikra ya Rais na Serikali yake juu ya ukuu wa mhimili wa Serikali dhidi ya Bunge.
6. Kitendo cha Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Tanzanite na Almasi kusomwa nje ya Bunge na kuwasilishwa kwa Waziri Mkuu na Rais bila kuwasilishwa na kujadiliwa Bungeni ili kuwekewa azimio la Bunge. Kitendo hiki kinaifanya Kamati hiyo kuonekana kuwa ya Serikali badala ya Kamati ya Bunge.

Part Three;
7. Kauli ya Rais kuwa Spika alimpigia simu kumuuliza juu wajumbe wa kuwaweka kwenye Kamati za Bunge za Tanzanite na Almasi inaonyesha dhahiri kuwa Spika anafanya kazi kwa maelekezo ya Rais. Na Bunge na Spika hawajawahi kuikana kauli hii ya Rais.
8. Kwa mara ya kwanza kwenye Historia ya Nchi yetu tumeshuhudia Mbunge akishambuliwa kwa risasi wakati Mkutano wa Bunge ukiwa unaendelea. Haijapata kutokea katika historia ya Bunge letu, Wabunge kukamatwa hovyo mbele ya mageti ya Bunge na kusafirishwa usiku usiku bila hata Spika kujulishwa kama taratibu za Mabunge ya Jumuiya ya Madola zinavyotaka. Kitendo cha ‘Watu Wasiojulikana’ kummiminia risasi zaidi ya thelathini Mbunge wa Singida Mashariki, ndugu Tundu Lissu, wakati akitokea Bungeni, tena kwenye makazi yake, ambayo kwa mujibu wa sheria ni sehemu ya Bunge, ni dharau ya hali ya juu kwa Mhimili huu. Ni tukio linalolenga kuliziba mdomo Bunge. Makala yangu ya Nani alitaka kumwua Tundu Lissu (kwa lugha ya Kiingereza) naiambatanisha katika maelezo yangu haya.
9. Kitendo cha Serikali kutowasilisha ‘Taarifa za Utendaji wa Robo Mwaka’ kwenye Kamati ya Bunge ya Bajeti kama inavyotakiwa kwa mujibu wa Sheria ya Bajeti ya mwaka 2014 ni dharau kubwa kwa Mhimili wa Bunge. Ni dharau zaidi kwamba Serikali ilileta Muswada wa sheria kuondoa kifungu kinacholazimisha Waziri wa Fedha kutoa Taarifa hizo, na Bunge kupitisha kuwa Sheria, hivyo kuondoa kabisa Uwajibikaji wa kibajeti wa Serikali ndani ya Bunge, hivyo kudunisha hadhi ya bunge.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents