Habari

Maeneo 14 ya Dar yaliyoathirika zaidi na mvua zinazoendelea kunyesha

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda ametoa tahadhari kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya Dar es salaam.

Ofisi ya mkuu huyo imetoa taarifa hii…

Kutokana na hali ya hewa iliyopo hivi sasa na tahadhari ziliyotolewa mara kwa mara na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kuwa kutakuwa na mvua na upepo mkali katika maeneo yote ya Mkoa wa Dar es Salaam na maeneo mengine ya ukanda wa Pwani, Tumeshuhudia jinsi hali hiyo ilivyotokea kwa maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam kufurika na maji na kusababisha adha kubwa ikiwa ni pamoja na baadhi ya watu kuzihama nyumba zao kwa kujaa maji na maeneo mengine miundo mbinu ya barabara kuharibika na kusababisha msongamano wa magari na kero kubwa kwa wananchi.

Maeneo yaliyofurika ni pamoja na eneo la Jangwani, Magogoni Kigamboni, Ilala Kata ya Mchikichini, Kipunguni, Viwege, Majohe, Kata ya Tabata Madona, Temeke Shule ya Sekondari Kibasila, Kinondoni Kata ya Kigogo, Tandale, Bunju eneo la Basihaya, Mwananyamala Mitaa ya Bwawani, Kambangwa, Msisiri ‘A’, Mbezi darajani na Katikati ya Jiji.

Serikali inaendela kuchukua hatua kurekebisha athari zilizojitokeza ili kuwaondolea adha wanachi kwa kuhakikisha mifereji iliyoziba inazibuliwa, kuweka madaraja ya muda pale madaraja yalipoharibiwa na maji, na kurekebisha barabara ili wananchi waweze kuendelea na shughuli zao. Sambamba na hilo nawataka Wananchi kuzingatia taratibu na kanuni za afya kwa kutozibua na kutiririsha majitaka katika mifereji na mikondo ya maji kwani hali hiyo inawezasababisha milipuko ya maradhi ambayo ni hatari sana kwa Maisha na afya zetu.

Ndugu Wananchi,

Wito wa Serikali kwa wakazi wote waishio mabondeni na maeneo mengine hatarishi kuhama katika maeneo hayo kutokana na athari za mvua hizi zinazoendelea zinazoweza kusababisha madhara makubwa kwao ikiwemo mafuriko, kuangukiwa na nyumba, miti au kusombwa na maji.Aidha, Kamati ya Maafa ya Mkoa kushirikiana na Kamati zote za Maafa za Wilaya kuratibu ipasavyo suala hili kwa kuweka utaratibu wa kuwataka wakazi waliopo maeneo hatarishi kuhama maeneo hayo ili kuepuka majanga ya mvua yanayoweza kujitokeza.

Mwisho, Ndugu wananchi tuendelee kufuatilia taarifa katika vyombo mbalimbali vya habari ambapo Serikali tutaendela kutoa taarifa kutokana na hali ya Mvua itakavyo endelea ili kuweza kujiokoa na madhara makubwa zaidi na pale utakapokuwa na tatizo kubwa zaidi usisite kutoa taarifa kwa Mamlaka husika.

PAUL C. MAKONDA
MKUU WA MKOA – DAR ES SALAAM
13 May 2019

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents