Siasa

‘Mafisadi wa EPA sawa na magaidi’

MKUU wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP) Said Mwema, amewafananisha watuhumiwa wa ufisadi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), sawa na watuhumiwa wa ugaidi ambao wanaweza kuilipua nchi.

Na Ramadhan Semtawa

 

 

 

MKUU wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP) Said Mwema, amewafananisha watuhumiwa wa ufisadi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), sawa na watuhumiwa wa ugaidi ambao wanaweza kuilipua nchi.

 

 

 

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana kuhusu mchakato unaoendelea katika urejeshaji wa fedha za umma zaidi ya Sh133 bilioni zilizoibwa EPA, Mwema ambaye ni mjumbe wa Timu Maalumu ya Rais ya kusimamia mchakato huo, alisema watu hao wanaweza kuilipua nchi iwapo watafuatwa kwa pupa.

 

 

 

IGP Mwema alisema timu inafahamu kwa kina jinsi Watanzania wanavyokerwa na kuhoji vipi, watuhumiwa hawakamatwi kitu ambacho hata wao (timu) kinawaumiza roho.

 

 

 

Alisema kuna mashaka makubwa miongoni mwa Watanzania kwamba, watu waliotajwa katika ufisadi huo wanapita mijini huku wakitamba, lakini hawakamatwi hali ambayo inawafanya wananchi wahoji kazi ya timu hiyo.

 

 

 

“Kuna mashaka makubwa, watu waliotajwa wanaonekana kupita mijini, wanatamba, watu sasa wanahoji hii timu kazi yake nini? Hili jambo linawakera wengi na sisi pia tunajisikia hivyo hivyo,” alisema IGP Mwema na kuongeza:

 

 

 

“Tunaambiwa tunawaogopa, hata sisi inatusikitisha kwanini hatuwakamati, kila mtu anajua na kila mtu anataka wakamatwe, lakini hili suala linahitaji upelelezi wa hali ya juu kwa kuwa linagusa watu wengi na maeneo mengi”.

 

 

 

Akisisitiza kuwa hata magaidi wanapoteka ndege na vikosi vikiwemo vya jeshi la ulinzi na polisi vikiwazingira, hawashambulii bali hufanya nao mazungumzo ili wasije wakawalipua mateka.

 

 

 

“Hata sisi tunaficha majina, si kwamba tunataka kula nao bali ni kwasababu ya suala lenyewe lilivyo nyeti na linahitaji umakini,” alisema.

 

 

 

Kwa msisitizo, Mwema alienda mbali zaidi baada ya kula kiapo mbele ya wahariri na waandishi waliofika katika mkutano huo, akisema ni bora afukuzwe wadhifa huo wa IGP kuliko kuambiwa amekula fedha na mafisadi.

 

 

 

Mwema akizidi kuonyesha uzito na unyeti wa mchakato huo, alisema roho zinawaenda mbio wakisikia wananchi wakihoji kama fedha hizo zitarudishwa na kukamatwa watuhumiwa.

 

 

 

“Wengine tukiambiwa hili roho zinaenda mbio, mimi nasema bora nifukuzwe U-IGP kuliko kuambiwa nimekula na mafisadi,” alisema.

 

 

 

Alisema ni kweli waliotajwa, wapo mijini na hawajakamatwa lakini akafafanua kwamba, kuna njia mbili za kushughulikia makosa ya jinai ambazo ni kukamata kabla ya upelelezi au kupeleleza baada ya kukamata.

 

 

 

“Kuna wengine wenye kandambili wanakamatwa na kufikishwa mahakamani, lakini wenye vitambi na magari ya kifahari hawakamatwi,” alisema na kuongeza:

 

 

 

“Naomba nitoe mfano mmoja, mheshimiwa Ditopile aliwahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi na anaheshimika sana katika nchi hii, lakini tulimkamata kabla ya upelelezi, kwa hiyo sasa tunapeleleza halafu tutakamata, kwani unaweza kukamata kabla, kisha ukapeleleza au kupeleleza halafu ukamate,” alifafanua.

 

 

 

Usiri watawala ziliko fedha

 

 

 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Timu hiyo, Johnson Mwanyika, tofauti na IGP Mwema yeye kama kawaida hakuwa na jipya la kueleza badala yake alishindwa kutoa majibu ya msingi ya maswali ambayo yamekuwa yakiulizwa.

 

 

 

Mwanyika akionekana dhahiri kushindwa kujieleza huku akijikanyaga katika kauli zake, alisema hadi sasa fedha hizo zinarejeshwa katika akaunti maalumu ambayo alisita kusema imefunguliwa wapi.

 

 

 

Huku akionekana kukosa taarifa mpya za kutoa kwa vyombo vya habari, Mwanyika alishindwa kueleza kwa dhati kiasi cha fedha kilichokusanywa hadi jana badala yake alikisia kwamba ilitarajiwa kuwa Sh60 bilioni.

 

 

 

Hata hiyo taarifa ya Mwanyika imepingana na iliyotolewa jana na Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambayo ilisema zilikuwa zimekusanywa Sh64 bilioni.

 

 

 

Alirudia maneno yake ya kusihi Watanzania kuwa na subira huku akishindwa kueleza pia kwamba, katika fedha hizo thamani ya mali ni kiasi gani na fedha taslimu.

 

 

 

“Tathimini ya thamani ya mali ndiyo inaendelea kufanyika, lakini tunajua kuna mali kama nyumba ziko nje, tutazichunguza kuona kama zina uhusiano tutazikamata,” alisema.

 

 

 

Kuhusu Daud Ballali kama amekwisha hojiwa au kama kuna uwezekano wa kumleta nchini, alisema hadi sasa uchunguzi umejikita kurejeshwa kwa fedha na kusisitiza iwapo atabainika kuhusika atarejeshwa nchini hapo baadaye.

 

 

 

Mwanyika alipoulizwa vipi anasita kutaja majina ya makampuni ambayo hadi sasa yamekwisha rejesha fedha kati ya 22, wakati tayari Katibu Mkuu Kiongozi aliyataja katika tamko la serikali, alijibu: “Hatuwezi kutaja, tunachofanya sasa ni kuhakikisha kuwa fedha zinarejeshwa kwanza”.

 

 

 

Kuitishwa kwa mkutano wa jana ni ishara kwamba, joto la ufisadi katika EPA limepanda huku shinikizo la wanaharakati likionekana dhahiri kuitikisa timu hiyo na serikali kwa ujumla.

 

 

 

Tayari wanaharakati wamepaza sauti wakiinyoshea kidole timu hiyo iliyoundwa na Rais Jakaya Kikwete, mapema Januari wakihoji utaratibu wa kisheria wa kushindwa kukamata watuhumiwa wa ufisadi wanaorejesha fedha hizo, badala yake wanaachiwa huru.

 

 

 

Ufisadi katika EPA akaunti ambayo ilifunguliwa wakati wa Ujamaa kuziba pengo la ukosefu wa bidhaa uliotokana na ukosefu wa fedha za kigeni, ulijitokeza katika kipindi cha mwaka 2005/06, baada ya ukaguzi wa kimataifa chini ya Kampuni ya Ernst&Young.

 

 

 

Kabla ya Arnst&Young, tayari Kampuni ya Deloitte&Touche ilikwisha anza ukaguzi na kubaini ufisadi huo hasa Sh40 bilioni ambazo zililipwa kwa Kampuni ya Kagoda Agriculture, lakini ghafla mkataba wake na BoT ukasitishwa.

 

 

 

Baada ya kubainika ufisadi huo, Rais Kikwete alitengua mkataba wa Ballali na kuteua gavana mpya huku akiunda timu hiyo na kuipa kazi mbili, kuhakikisha fedha zinarudi na watuhumiwa wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

 

 

 

CCM yapongeza

 

 

 

Wakati Mwenyekiti wa Timu ya Rais ya Uchunguzi wa Fedha za Akaunti ya Malipo ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Johnson Mwanyika akisema fedha zilizorejeshwa ni Sh60 bilioni, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimesema fedha za akaunti hiyo zilizokwisharejeshwa hadi jana zilikuwa ni Sh64 bilioni.

 

 

 

CCM ilieleza hayo kupitia taarifa yake iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana kuhusu kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho (CC) Taifa, kilichojadili mambo mbalimbali, ikiwamo suala hilo katika kikao chake, kilichofanyika chini ya uenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete, jijini Dar es Salaam juzi.

 

 

 

“Timu hiyo inaendelea kuzibana kampuni husika kurejesha fedha zilizochukuliwa kwa njia haramu. Hadi sasa timu imefanikisha kurejeshwa kwa jumla ya Sh64 bilioni,” ilieleza taarifa hiyo iliyosainiwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi wa CCM, Kapteni John Chiligati.

 

 

 

Taarifa ya hiyo ilisema kuwa timu hiyo inaendelea kuwabainisha wanahisa wote wa makampuni yaliyochukua fedha hizo kwa njia za udanganyifu na hasa wahusika wakuu wa uchukuaji wa fedha hizo.

 

 

 

Hata hivyo, Kamati Kuu iliipongeza timu hiyo kwa kazi nzuri inayoifanya hadi kufikia sasa na kuitaka iendelee na jitihada za kuhakikisha fedha zote zinarudi na wahusika wakuu wanabainishwa ili sheria ichukue mkondo wake.

 

 

 

Mwanyika wakati akizungumza na waandishi wa habari jana alisema kuwa hadi kufikia jana asubuhi, timu yake ilikuwa imekusanya jumla ya Sh60 bilioni kutoka kwa watu waliochukua fedha hizo.

 

 

 

Hali hiyo ya kutolewa idadi tofauti kati ya timu na Kamati Kuu ya CCM ambacho ndicho chombo cha juu cha maamuzi ya chama tawala, inatia wasiwasi kuhusu ukusanyaji wa fedha hizo.

 

 

 

Source: Mwananchi

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents