Magaidi wamkosa Bush

WATU wanne, wawili wakiwa ni Waarabu, walikamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi mkali wa polisi baada ya kukamatwa wakihusishwa na tuhuma za ugaidi.

na Happiness Katabazi na Kulwa Karedia

 

 

 

WATU wanne, wawili wakiwa ni Waarabu, walikamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi mkali wa polisi baada ya kukamatwa wakihusishwa na tuhuma za ugaidi.

 

 

 

Tukio la kukamatwa kwa watu hao wanne katika mikoa ya Dar es Salaam na Arusha, kulikotokea siku chache kabla ya kuwasili nchini kwa Rais wa Marekani, George Bush, kumethibitishwa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna wa Polisi, Robert Manumba.

 

 

 

Kamishna Manumba alisema, watuhumiwa wawili kati ya hao, ambao wana asili ya Kiarabu, walikamatwa Dar es Salaam wakati wengine wawili walikutwa Arusha.

 

 

 

Manumba alisema Jeshi la Polisi liliwakamata watuhumiwa hao baada ya makachero wake kufanya upelelezi wa kina kutokana na kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema zilizokuwa zikiwahusisha na vitendo vya kigaidi.

 

 

 

“Ninachofahamu mimi, watuhumiwa hawa wamekamatwa na makachero wa Jeshi la Polisi kwa tuhuma za ugaidi ila ni mapema mno kusema kwamba walikuwa wamepanga kufanya ugaidi kwenye ujio wa Rais Bush hapa nchini.

 

 

 

“Tulipata taarifa hizi kutoka wa wananchi wenye nia njema, tukatuma vijana wetu ambao walifanya kazi hiyo kwa makini mno na kufanikiwa kuwakamata watu hao, tumewahoji kila mmoja ili kupata undani… kuna mambo wametueleza, mambo mengi,” alisema DCI.

 

 

 

Alisema watuhumiwa hao walikamatwa baada ya msako mkali kuendeshwa kutokana na taarifa hizo za raia wema.

 

 

 

Kamishna Manumba alisema kuwa, wawili kati ya watuhumiwa hao walikamatwa siku chache kabla ya kuwasili nchini kwa Rais Bush wa Marekani.

 

 

 

“Hawa tumewakamata kabla ya ujio wa Rais Bush, sasa maelezo yao ndiyo yanayotusaidia kutambua walikuwa na nia gani, kwa namna moja au nyingine hatuwezi kuwahusisha moja kwa moja na ziara ya kiongozi huyo aliyekuwepo hapa nchini kwa siku nne,” alisema DCI.

 

 

 

Bush alimaliza ziara yake ya siku nne jana na hakukuwa na tukio lolote la kuhatarisha amani lililoripotiwa wakati wa ziara yake, ambayo aliifanya katika mikoa ya Dar es Salaam na Arusha.

 

 

 

Manumba alisema, bado ni mapema mno kuzungumzia suala hilo, lakini polisi wako katika hali ya mapambano mazito dhidi ya ugaidi kutokana na Tanzania kuonja machungu ya ugaidi Agosti mwaka 1998 wakati ofisi za Ubalozi wa Marekani zilipolipuliwa na magaidi wa kundi la al-Qaeda.

 

 

 

“Uzoefu unaonyesha kwamba nchi nyingi ambazo zimekuwa zikilengwa na mikasa hii ni Marekani na Ulaya, sasa sisi kwa kweli tunasema kwamba, zoezi hili ni endelevu. Kila siku ya Mungu tunajipanga na kujilinda ili kuepukana na matatizo ambayo yanaweza kutokea,” alisema DCI Manumba.

 

 

 

Manumba alisema hali ya mapambano dhidi ya ugaidi inaendelea kwa nguvu zote ili kuhakikisha Tanzania inakuwa salama siku zote.

 

 

 

DCI alisema kuwa baada ya mahojiano, watuhumiwa watatu waliachiwa, lakini hadi jana, polisi walikuwa bado wanamshikilia mtuhumiwa mmoja kwa mahojiano zaidi mkoani Dar es Salaam, ambaye anaonekana kutotoa ushirikiano zaidi tangu alipotiwa mikononi.

 

 

 

“Baada ya kuwahoji wote, baadhi yao tumewaachia baada ya kuonekana hawana hatia, lakini kuna mmoja tunaendelea kumhoji zaidi kwa vile tunadhani bado kuna mambo zaidi ambayo tunaamini anaweza kutusaidia,” alisema DCI.

 

 

 

Pamoja na kuieleza hali halisi Tanzania Daima, DCI hakuwa tayari kutaja majina ya watuhumiwa hao kwa kile alichodai kuwa kwa ajili ya masuala ya usalama.

 

 

 

Habari hizi zinakuja baada ya kuwapo kwa taarifa nyingine kutoka mkoani Arusha zinazoeleza kuwa, watu kadhaa ambao ni waumini wa Kiislamu, walitiwa mbaroni na polisi siku kadhaa kabla Rais Bush ajatua mkoani humo, wakituhumiwa kupanga maandamano ya kupinga ziara hiyo.

 

 

 

 

 

Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents