Habari

Magari 8 yagongana, matatu yamfunika muuza magazeti

Ajali Ubungo (Picha na Kulwa Mwaibale)Kijana mmoja muuza magazeti amekufa papo hapo baada ya kufunikwa na magari zaidi ya matatu kati ya nane yaliyopata ajali baada ya Fuso kukatika breki, tukio hilo lilitokea jana jijini Dar es Salaam maeneo ya Ubungo

Ajali Ubungo (Picha na Kulwa Mwaibale)


 


Na Anneth Kagenda



Kijana mmoja muuza magazeti amekufa papo hapo baada ya kufunikwa na magari zaidi ya matatu kati ya nane yaliyopata ajali baada ya Fuso kukatika breki.

Tukio hilo lilitokea jana jijini Dar es Salaam maeneo ya Ubungo Maji saa 6:34 mchana baada ya Fuso hilo lenye namba za usajili T 655 AFW lililokuwa limebeba vitunguu kukatika breki.

Hata hivyo, kijana huyo jina lake halikuweza kupatikana mara moja wala umri wake.

Fuso hilo lilisababisha ajali nyingine ya magari nane yaliyokuwa kwenye foleni yakitokea maeneo ya Kimara.

Akielezea tukio hilo, dereva wa gari daladala lenye namba za usajili 47495 ZNZ, Bw. Idd Mchopanga, alisema akiwa kwenye foleni alisikia watu wakipiga kelele za “tunakufa!“ kabla hajafikiwa na baada ya muda mfupi gari lake lilivamiwa na gari iliyokuwa nyuma yake.

“Awali sikujua ajali hiyo ilitokana na nini, ila nilishangaa kuona tayari navamiwa, na mimi nilijitahidi kutoka kwenye gari ili kuona kama nitaweza kunusuru maisha yangu,“ alisema Bw. Mchopanga.

Bw. Mchopanga alipata majeraha madogo kwenye mwili wake ikiwa ni pamoja na kuchubuka uso.

Kwa upande wake, dereva wa daladala ambalo halikuweza kusomeka namba kwa vile liliharibika vibaya, Bw. Akhibal Badru, alisema kuwa gari hilo lilikuwa likiendeshwa na baba yake (hakuwepo).

Alisema kuwa wao hawakujeruhiwa japokuwa kwa wakati huo walikuwa wakijisikia vibaya kwa ajili ya mshtuko na kwamba ajali hiyo ilisababishwa na mwendo wa kasi.

Magari mengine ni teksi yenye namba T 230 AMY, hiace daladala yenye namba T 985 AFG na mengine ambayo hayakuweza kutambulika namba zake kwa vile yalikuwa yameharibika vibaya.

Aidha shuhuda mmoja, Bw. Kharisto Pivato, aliyekuwa eneo la tukio alisema kuwa Fuso hilo lilikatika breki tangu likiwa Kimara lakini lilikuja kuishiwa nguvu zaidi lilipofika Ubungo kitendo kilichosababisha kutokea kwa ajali hizo zote.

“Japokuwa dereva hajaonekana lakini alijua mapema kuwa gari hiyo ilikuwa haina breki sasa kilichomfanya ailete mpaka huku ni nini,“ Alisema shuhuda huyo akishangaa.

Inasemekana dereva wa Fuso hilo alikimbia kutokana na kugundua kusababisha ajali hiyo kwa uzembe wa hali ya juu.


 


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents