Habari

Magari yenye mwanga mkali yapigwa marufuku

Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani imesema itaanza kukamata magari yote ambayo yamewekwa taa zenye mwanga mkali (spotlights) kwa kuwa uwekaji wa taa hizo, ni kinyume na sheria ya usalama barabarani.

Kauli hiyo imetolewa na Kamanda wa Kikosi hicho, Naibu Kamisha Mohammed Mpinga wakati akizungumza na gazeti la habarileo ofisi kwake jijini Dar es Salaam, ambapo alisema ukamataji wa magari hayo utaanza rasmi wiki ijayo.

Mpinga alisema wameshatoa maelekezo kwa askari wa usalama barabarani, kuhakikisha wanakamata magari, pikipiki na malori makubwa ambayo yamewekwa taa hizo.

“Ziko taa za aina fulani zinazowekwa kwenye magari na hata ukitembea usiku utaona mwingine ameweka taa moja mwingine anaweka nyingi sana, kiasi ambacho zimeleta matatizo kwa madereva wengine,” alisema Kamanda Mpinga.

Aidha, alisema kwenye barabara kuu kuna mtindo wa madereva wa magari makubwa, kuweka taa kubwa ambazo zinawekwa juu na kumulika mwanga mkali, kiasi ambacho dereva anayemulikwa anapata upofu wa muda na kushindwa kudhibiti chombo chake.

Kamanda Mpinga alisema kuwa walishatoa muda wa kutosha kwa wamiliki wote wa magari, walioweka taa hizo kuziondoa, hivyo kwa sasa wataanza kuwachukulia hatua wote ambao watakuwa hawajaziondoa.

Alifafanua kuwa uwekaji wa taa hizo ni kinyume cha Sheria ya Usalama Barabarani Kifungu cha 39 Sura ya 168, ambacho kinaeleza matumizi ya taa. Mpinga pia alisema magari yatakayokamatwa ni yale ambayo yameongezewa taa hizo.

BY: Emmy Mwaipopo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents