Habari

‘Magazeti ya udaku yafungiwe’

WABUNGE wamemtaka Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo kuyafungia magazeti yote ya udaku yanayochapisha picha za ngono pamoja na kukamata CD za video za filamu za ngono zinazouzwa mitaani.

Maulid Ahmed, Dodoma


WABUNGE wamemtaka Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo kuyafungia magazeti yote ya udaku yanayochapisha picha za ngono pamoja na kukamata CD za video za filamu za ngono zinazouzwa mitaani.


Wakichangia makadirio na matumizi ya fedha ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2007/2008 jana, wamemtaka Waziri huyo kutumia mamlaka aliyopewa kisheria kuwachukulia hatua watu hao wanaochapisha picha hizo ambazo ni kinyume na maadili.


Akitoa mchango wake, Mbunge wa Newala, George Mkuchika (CCM) alisema, “Waziri nafahamu una uwezo, tumia nafasi yako kufungia magazeti yanayoandika uchafu, yanachapisha picha za uchi… Tanzania ni nchi ya kistaarabu, hao wanaharibu watoto wetu.”


Mbunge wa Viti Maalumu, Magdalena Sakaya (CUF) aliitaka wizara hiyo inayoongozwa na Muhammed Seif Khatib, kuchukua hatua za haraka kuyafungia magazeti yanayochapisha picha za ngono na kuongeza, “mtu analewa pombe picha yake inawekwa gazetini, picha za uchi nazo zinawekwa gazetini, serikali inanyamaza kwa nini inayaacha magazeti haya?”


Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu (CCM), alisema, “ukipita kila kwenye mataa ya barabarani, utaona kunauzwa CD za pilau na biriani (ngono), wakamatwe wote haraka
wanaouza CD za ngono, watoto wetu wananunua na kujifungia vyumbani wanaangalia.”


Akisoma maoni ya Kambi ya Upinzani, Mwanawetu Said Zarafi alisema asilimia 70 ya waandishi wa habari nchini hawajaajiriwa na wanalipwa kati ya Sh 1,000 hadi Sh 10,000 kwa habari moja, hivyo kumtaka Waziri kuweka utaratibu unakaotumiwa na wamiliki wa
vyombo vya habari kuhakikisha masilahi yao yanalingana na taaluma yenyewe.


Akiwasilisha makadirio na matumizi ya wizara hiyo, Waziri Khatib alisema Wizara yake
inaendelea na mchakato wa kutayarisha muswada wa sheria utakaotoa uhuru mkubwa wa habari na kurekebisha au kufuta sheria za vyombo vya habari zilizopitwa na wakati zinazolalamikiwa na wadau kama Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 na Sheria ya Utangazaji ya mwaka 1993.


Alisema hadi sasa kuna vituo 40 vya radio nchini, vituo 22 vya televisheni na 18 vinavyounganisha na kurusha matangazo ya vituo vingine. Pia kuna vituo 42 vinavyoendesha shughuli za cable TV. Magazeti ya kila siku yapo 33 na ya kila wiki yapo 187.


Alisema katika mwaka huu wa fedha, Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), litasanifu
istilahi katika uwanja wa diplomasia na uhusiano wa kimataifa na kuchapisha kamusi ya diplomasia na kitabu cha Mwongozo wa waandishi utakaowaelimisha kuhusu mbinu za uandishi sahihi, matumizi ya vituo na istilahi.


Wizara hiyo imeomba kuidhinishiwa Sh 16,021,476,000, kati ya hizo, Sh 11,030,476,000 ni fedha za matumizi ya kawaida na Sh 4,991,000,000 ni fedha za maendeleo.


Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents