Maghembe Na Mgomo Wa Vyuo

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Jumanne Maghembe, amesema idadi kubwa ya wanafunzi wanaogoma kuishinikiza serikali iwapatie mikopo ya elimu ya juu kwa asimilia 100, ni wale wasiokidhi vigezo vya kupata mikopo hiyo.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Jumanne Maghembe, amesema idadi kubwa ya wanafunzi wanaogoma kuishinikiza serikali iwapatie mikopo ya elimu ya juu kwa asimilia 100, ni wale wasiokidhi vigezo vya kupata mikopo hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana kuhusu mgomo wa nchi nzima ulioitishwa na Umoja wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu vya Umma, Profesa Maghembe alisema anashangazwa na migomo ya mara kwa mara ya wanafunzi kuhusu mikopo, wakati sera ya kuchangia elimu ya juu inaeleza wazi juu ya suala hilo.

Alisema kuwa serikali imekuwa ikitoa ufafanuzi mara kwa mara kuhusu wanafunzi wanaostahili kulipwa mikopo hiyo, lakini migomo inazidi kuongezeka, hali
inayoonyesha kuwa kuna ajenda nyingine ya siri iliyojificha nyuma ya migomo hiyo.

“Tumekuwa tukilitolea ufafanuzi suala hili la mikopo mara kwa mara na wanafunzi wamekuwa wakituelewa, lakini mara baada ya muda kidogo utasikia migomo tena, nafikiri kuna watu wanawashinikiza wanafunzi wagome, hapa kuna ajenda ya siri, tatizo siyo mikopo tu,“` alisema Profesa Maghembe.

Waziri huyo aliitisha mkutano huo na waandishi wa habari kufuatia mgomo huo ulioanza jana kwa baadhi ya wanafunzi wa vyuo vikuu vya umma nchini kutoingia madarasani, wakiishinikiza serikali iwapatie mikopo hiyo.

Profesa Maghembe alisema mgomo huo ni batili kwa kuwa umoja wa wanafunzi uliouitisha hautambuliwi na serikali kwa kile alichoeleza kuwa haujaandikishwa kwa mujibu wa taratibu kwani unaotambulika ni ule wa Umoja wa Vyuo Vikuu vya Umma (Tahliso).

“Hiki chama kimejifungia baa na kuibukia TBC1 kutangaza mgomo, chama chenyewe ni batili kwani hakijafuata taratibu zozote za kujiandikisha wala hakina katiba yoyote hivyo wanafunzi nawasihi wasifuate mgomo huo bali waingie darasani kama kawaida,“ alisisitiza.

Akiwa amefuatana na manaibu wake wawili, Mwantumu Mahiza na Gaudencia Kabaka, Maghembe alifafanua kuwa sera ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu inaeleza wazi ni wanafunzi gani na kwa kiwango gani wanastahili kupata mikopo hiyo.

Alisema kwa kutambua umuhimu wa elimu, serikali imetenga bajeti ya Sh bilioni 119 kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na kwamba hadi sasa wanafunzi 60,000 wamepewa mikopo hiyo.

Hata hivyo, alisema kuwa kiwango hicho cha fedha kilichotengwa kwa ajili ya mikopo ni kidogo na kwamba endapo serikali ingeamua kutoa mikopo kwa asimilia 100 kwa kila mwanafunzi basi ni wanafunzi 40,000 tu ndiyo wangenufaika nayo badala ya 60,000.

 

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents