Siasa

Magufuli aandaa risasi kujibu mashambulizi

MGOGORO wa kiwanja namba 951, ilipojengwa Baa ya Rose Garden jijini Dar es Salaam, umechukua sura mpya baada ya mmoja wa viongozi walio katikati ya sakata hilo kuandaa hoja za kujisafisha dhidi ya tuhuma zinazoelekezwa kwake.

Charles Mullinda na Agnes Yamo

 

MGOGORO wa kiwanja namba 951, ilipojengwa Baa ya Rose Garden jijini Dar es Salaam, umechukua sura mpya baada ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, John Pombe Magufuli, mmoja wa viongozi walio katikati ya sakata hilo kuandaa hoja za kujisafisha dhidi ya tuhuma zinazoelekezwa kwake.
Aidha, mgogoro huo ambao taarifa za karibuni zinaonyesha unatafutiwa njia ya kufikishwa kwa Rais Jakaya Kikwete, umeshafikishwa au kuwagusa kwa namna tofauti, Waziri Mkuu, Edward Lowassa na Katibu Mkuu wa CCM, Yussuf Makamba.
Habari kutoka vyanzo kadhaa vya kuaminika zinaeleza kwamba, tayari maofisa wa wizara hiyo wameshaanza kukusanya taarifa mbalimbali ili kujua sababu hasa ya suala hilo linalohusu baa, ifikie hatua ya kugusa hisia za viongozi wa juu kama Waziri Mkuu, Katibu Mkuu wa CCM na Baraza la Madiwani wa Kinondoni.
Kikubwa kinachoanza kutia shaka sasa ni namna Makamba ambaye kabla ya kuwa Katibu Mkuu wa CCM alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuingia kwake moja kwa moja katika suala hilo kwa kiwango cha kutaka mmiliki wa Rose Garden apokonywe kiwanja hicho.
Aidha, kumbukumbu za kimaandishi zinaonyesha kuwa, Makamba alianza kujihusisha na suala hilo kwa karibu kabisa, akisema anafanya hivyo akipata taarifa kutoka kwa watu anaowataja kuwa wasamaria wema (wasiotajwa kwa majina).
Kwa mara ya kwanza Makamba alianza kujihusisha moja kwa moja na suala hilo Juni mwaka 2004 kwa kufanya mazungumzo na uongozi wa Manispaa ya Kinondoni na baadaye mwaka huo huo akaandika barua kwa mkurugenzi wa manispaa hiyo.
Baada ya suala hilo kugonga mwamba na kukosa kumalizwa, Januari mwaka jana tena, siku 12 baada ya Kikwete kuunda Baraza la Mawaziri, aliandika barua ndefu yenye kurasa nne kwenda kwa Magufuli akihoji kuhusu uhalali wa mmiliki wa Rose Garden kuendelea kuwapo hapo kinyume cha sheria.
Katika hali inayoweza ikazusha maswali mengi baadaye, Makamba alituma nakala za barua hiyo kwa Rais, Waziri Mkuu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Waziri wa Miundombinu, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni.
Katika hali ambayo bado haijawa wazi hadi hivi sasa, Makamba huyo huyo tena, katika tarehe na siku isiyojulikana wakati akiwa Katibu Mkuu wa CCM, aliamua kuandika barua kwa Waziri Mkuu akimlalamikia mmiliki huyo wa Rose Garden.
Hatua hiyo ya Makamba kwa nyakati tofauti ilikwenda sambamba na msimamo wa Manispaa ya Kinondoni, moja ya eneo linaloongoza kwa migogoro ya viwanja hapa nchini, wa kutaka kuivunja baa hiyo kwa madai kwamba imejengwa katika eneo la hifadhi ya barabara.
Hata hivyo jitihada hizo za Makamba na za Manispaa ya Kinondoni kwa nyakati tofauti zilionekana kugonga mwamba baada ya Magufuli kuchukua njia tofauti na wao ya kuamua kutumia sheria kumhalalisha Assey kumiliki kiwanja ilipo baa yake, ambacho kabla ya kukitumia kwa shughuli hizo, ilikuwa ni sehemu ya kuuzia maua.
Uchunguzi wa Tanzania Daima umebaini kwamba, kikubwa kilichosababisha suala hilo linaloonekana dogo libadilike sura na kuchukua taswira kubwa hata kuwagonganisha viongozi wa kiserikali, si Rose Garden, bali suala jingine tofauti kabisa.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, kiini cha mgogoro huo ni malalamiko ya ama moja kwa moja au yasiyo ya moja kwa moja ya mmiliki wa kiwanja kilicho nyuma ya Rose Garden (jina tunalo).
Vyanzo vya habari vya kuaminika vinaeleza kuwa, mmiliki huyo ambaye alinunua kiwanja hicho kwa mamilioni ya fedha, anakusudia kuwekeza kwa kujenga kituo maalumu cha biashara kinachojulikana kwa jina la ‘Dar es Salaam Village Centre’.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, mradi huo mkubwa wa mamilioni, umekwama kuanza kutokana na kile kinachoonekana kuwa ni kuwapo kwa Rose Garden mbele yake, jambo ambalo linaweza kukamisha uwekezaji mzima wa kituo hicho cha kibiashara kinachokusudiwa kujengwa.
Kwa sababu hiyo basi, malalamiko ya mmiliki wa kiwanja hicho kilicho nyuma ya Rose Garden ndiyo hasa yaliyoamsha hoja za kuhoji uhalali wa baa hiyo kujengwa hapo, hali inayozuia wamiliki wengine na hatimaye kuzaa mgogoro wa sasa.
Mgogoro huo, ambao umevuta hisia za Watanzania wengi na kuwahusisha baadhi ya viongozi wa juu serikalini, huku ukiibua mvutano baina ya Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni inayoongozwa na Meya Salum Londa kwa upande mmoja na Waziri Magufuli kwa upande mwingine, sasa unaonekana dhahiri unaweza ukapanda ngazi za juu kuchukua sura nyingine.
Habari zaidi ambazo Tanzania Daima imezipata kutoka vyanzo vya kuaminika katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi zinaeleza kwamba, Magufuli amelazimika kuandaa vielelezo vya maandishi na vya kauli kuhalalisha kuridhia kwa uamuzi wa Kamishna wa Ardhi wa kumpa mmiliki wa Rose Garden hati halali ya kumiliki kiwanja namba 951, ilipojengwa baa hiyo maarufu.
Inaelezwa kuwa moja ya vielelezo hivyo ni majibu ambayo Magufuli alimwandikia Waziri Mkuu, Edward Lowassa, akielezea sababu hasa za kummilikisha, Damas Assey, kiwanja hicho.
Ofisa mmoja wa juu wa wizara hiyo aliyezungumza na gazeti hili alisema, Magufuli katika majibu yake hayo, amebainisha kiini cha mgogoro huo kuwa ni mmiliki mwingine wa kiwanja kilicho karibu kabisa na kiwanja ilipojengwa Rose Garden.
Kwa mujibu wa ofisa huyo, uamuzi wa Magufuli kuridhia kupewa hati kwa mmiliki huyo kulichangiwa kwa kiwango kikubwa na ripoti aliyopewa na wataalamu wa wizara hiyo waliokwenda kuchunguza kiini cha malalamiko ya kuonewa yaliyofikishwa hapo na Assey dhidi ya Manispaa ya Kinondoni.
Aidha, majibu ya maelezo hayo yaliyoandaliwa na Magufuli yanaweza kuibua kashfa nyingine ya rushwa ndani ya Wizara ya Ardhi, Manispaa ya Kinondoni na baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wa hapa jijini wanaotajwa kuhusika kwa namna moja au nyingine katika mgogoro huo.
Katika maelezo yake, Magufuli anabainisha jinsi mmiliki wa kiwanja hicho, Damas Assey alivyoomba na kumilikishwa eneo hilo na Kamishina wa Ardhi, Albert Msangi na uongozi wa Manispaa ya Kinondoni kupewa taarifa ya maandishi kuhusiana na suala hilo.
Anaeleza kuwa eneo la Rose Garden liko kwenye safu ya viwanja namba 948, 949, 950 na 951 ilipojengwa baa hiyo, katika eneo la Mikocheni, kandokando ya barabara ya Garden na Mikocheni.
Magufuli anaeleza katika maandishi yake kuwa, viwanja hivyo vilibuniwa katika mchoro wa mipango miji TP.NO 1/518/369 ‘B’ na upimaji kukamilishwa kwa ramani ya upimaji namba ‘E’ 320/224 ya Aprili 16, 2004.
Sehemu ya maelezo hayo ya maandishi ambayo gazeti hili limepata nakala yake, inasomeka kuwa: ‘Aidha ubunifu na upimaji wa viwanja hivi ulikuwa ni muendelezo wa upimaji wa eneo lenye viwanja kati ya 383 hadi 385 kwa ramani namba E 320/74.
“Baada ya upimaji huo kukamilika, mmiliki wa Rose Garden, Damas Assey aliwasilisha maombi ya kumilikishwa kiwanja hiki kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni.
“Taratibu za umilikishaji zilifuatia kwa kuandaliwa nyaraka stahili lakini hazikuweza kukamilishwa kutokana na kuwasilishwa kwa hoja ya kupinga umilikishaji huo kupitia viongozi ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam, na jirani/mmiliki wa kiwanja namba 717/5 kilichopo nyumba ya kiwanja namba 951 baada ya kiwanja hicho kununuliwa na Kampuni ya ZEK GROUP LTD.
“Tarehe 7, Machi 2006, Damas Assey ambaye ndiye mmiliki wa Rose Garden, alileta malalamiko yake kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, akilalamikia kutotendewa haki.
“Waziri aliagiza ufanyike uchunguzi juu ya ukweli wa suala hili na yalibainishwa mambo yafuatayo; ramani ‘E’ 320/224 bado ni hai na haijafutwa,” yanasema maandishi hayo ya utetezi wa Magufuli.
Maandishi hayo ya Magufuli yanavitaja viwanja vingine vilivyobuniwa na ramani hiyo hapo juu kuwa ni, 948, 949 na 950 na vilipimwa kwa ramani namba ‘E’ 320/74 ambavyo ni 383 -385 havilalamikiwi japo vyote vipo kwenye safu moja kando kando ya barabara ya Garden.
‘Wenye viwanja namba 948 na 950 hawabughudhiwi na wanatambulika na mamlaka husika isipokuwa mwenye kiwanja namba 951(Rose Garden).
‘Waziri aliagiza haki itendeke kwa kummilikisha Damas Assey ambaye ni mmiliki wa Rose Garden’.
Aidha, katika maelezo yake, Waziri Magufuli anabainisha kuwa, ubunifu na upimaji wa kiwanja namba 951, ilipo Baa ya Rose Garden, umezingatia sheria, kanuni na sheria za mipango miji na kwamba, eneo hilo halipo kwenye hifadhi ya barabara.
Maelezo haya ya Magufuli yanaondoa shaka iliyopo kuhusu uhalali wa kujengwa kwa Baa ya Rose Garden katika kiwanja hicho na yanaondoa nguvu za msimamo wa madiwani wa Kinondoni wa kutaka baa hiyo ivunjwe kwa sababu yanadhihirisha wazi kuwa, halmashauri hiyo iliridhia kuwepo kwa kwa kiwanja hicho.
Vielelezo vingine vilivyoandaliwa na Magufuli ni pamoja na barua ya Kamishna wa Ardhi ya Juni 21 mwaka jana, yenye kumbukumbu namba LD/247419/9/LMK, inayoridhia kumilikishwa kwa viwanja hivyo na kumtaka mmiliki wa Rose Garden kulipa sh mil. 6,121,200 ndani ya siku 30 ili hatua za kumilikishwa eneo hilo ziweze kukamilishwa.
Katika kuhakikisha maamuzi yake hayaingiliwi wala kutenguliwa na viongozi wakuu ambao wamekwisha kuhoji kuhusu ukweli wa jambo hilo, Magufuli ameshamwandikia Waziri Mkuu Lowassa kumtaarifu kuwa kwa mujibu wa sheria namba 167 ya mwaka 1967 inayohusu hifadhi ya barabara, eneo ilipojengwa Baa ya Rose Garden halipo katika hifadhi ya malipo.
Maelezo hayo ya Magufuli yanajibu barua ya Lowassa ya Agosti 4, 2006, yenye kumbukumbu namba PM/P/1/567/38 iliyotumwa kwa Magufuli ikimtaka kueleza ukweli wa jambo hilo.
Magufuli alipewa siku tano na Lowassa kutoa maelezo kuhusu kuwapo kwa baa hiyo katika eneo hilo baada ya Katibu Mkuu wa CCM, Yussuf Makamba, ambaye amekuwa akimwandikia barua (Lowassa), kuhusu utata wa kujengwa kwa baa hiyo katika eneo hilo.
Alipoulizwa kuhusu mgogoro huo na hatua zinazochukuliwa na Magufuli dhidi ya halmashauri yake juzi, Meya wa Manispaa wa Kinondoni, Salum Londa, alikataa kuzungumza lolote kwa maelezo kuwa suala hilo, sasa linashughulikiwa na viongozi wa juu serikali.
“Siwezi kuzungumza lolote, kama kuna makombora yanaandaliwa dhidi yetu sawa tu, mimi niko kimya, ….andika unavyoona,” alisema.
Londa amefikia hatua hiyo, siku chache tu baada ya yeye na madiwani wenzake wa Kinondoni kutoa msimamo mkali dhidi ya maamuzi ya Magufuli ambaye hivi karibuni alipozungumza na waandishi wa habari alisema bayana kuwa mmiliki wa Rose Garden alikuwa na hati halali za umiliki.
Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents