Habari

Maiti 19 wa ajali ya Buffalo watambuliwa

UTAMBUZI wa maiti wa ajali ya basi la kampuni ya Buffalo umeendelea na hadi jana mchana, maiti 19 walikuwa tayari wametambuliwa na kubaki watatu wasiotambuliwa.

Na Yohanes Mbelege, Moshi


UTAMBUZI wa maiti wa ajali ya basi la kampuni ya Buffalo umeendelea na hadi jana mchana, maiti 19 walikuwa tayari wametambuliwa na kubaki watatu wasiotambuliwa.


Taarifa ya Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro iliyotolewa kwa niaba ya Kamanda wa Jeshi hilo Mkoa, Bw. Lucas Ng’oboko, imewataja waliotambuliwa kuwa ni, Bw. Isaya Mbaga (77), mfanyabiashara wa Kaloleni, Arusha.


Wengine ni Asha Eliasaa (20), mwanafunzi wa sekondari ya kiislamu ya Ilala, Dar es Salaam na mkazi wa Bomang’ombe Kibaoni wilayani Hai, Kilimanjaro na Bw. Isaack Ndanshau (43) mfanyabiashara wa Kiwalani, Dar es Salaam.


Pia Lilian Ahimidiwe (20) mwanafunzi wa kidato cha sita wa sekondari ya Machame, Hai na mkazi wa Kimara Kilugule, Dar es Salaam na Herman Peter (23) mwanafunzi wa Chuo cha Kimataifa cha Wanyamapori Mweka, Moshi Vijijini.


Wengine ni Daniel Dugilo (19) mwanafunzi wa kidato cha tano sekondari ya Kibo, Moshi, Rose Joachim (16) mwanafunzi wa sekondari ya Manungushi na mkazi wa Dar es Salaam na Bw. Evod Kwayu (39) mfanyabiashara wa Kibosho, Moshi Vijijini.


Marehemu wengine ni Bw. Jaffary Ridhiwan (20), aliyekuwa kondakta wa Buffalo, Bw. Noela Moshi (38) Mhasibu wa Hospitali ya Shilela, Arusha, Bw. Ayoub Kimaro (23) fundi cherehani wa Moshi na Stephen Mlemeta (19) mwanafunzi wa kidato cha sita sekondari ya Majengo mjini hapa.


Wengine waliotambuliwa hadi jana ni Bw. Benedict Magufya (48) Mhasibu wa Wizara ya Elimu katika sekondari ya Nshupu, Arusha na ambaye alikuwa mkazi wa Ukerewe, Mwanza.


Wengine ni Upendo Mkanza (14) mwanafunzi wa darasa la saba shule ya Msingi Kimnyaki, Arumeru, Arusha, Bw. Gerison Duguda (40) mwandishi wa habari wa kujitegemea wa Yombo, Dar es Salaam.


Maiti wengine ni Eli Adam (12) mwanafunzi wa shule ya kutwa ya Arusha, Glad Robert (8) mwanafunzi wa darasa la tatu katika shule ya msingi Loruwani, Kelvin Robert mwanafunzi wa darasa la tatu katika shule ya msingi ya Loruwani na Claud Robert (5) mwanafunzi wa chekechea, Arusha.


Naye Glory Mhiliwa anaripoti kutoka Arusha kwamba Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Bibi Margreth Sitta, amesema wizara yake imepata pigo kubwa kwa vifo vya walimu na wanafunzi katika ajali ya basi la kampuni ya Buffalo Aprili 15 ya mwaka huu, Mwanga mkoani Kilimanjaro.


Katika ajali hiyo iliyohusisha basi na lori la kubeba mafuta, watu 22 walikufa papo hapo na wengine zaidi ya 50 kujeruhiwa, wakiwamo walimu na wanafunzi waliokuwa wakirudi shuleni baada ya likizo fupi ya siku kuu ya Pasaka.


Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, Bibi Sitta alitoa pole kwa wazazi na walezi wa wanafunzi na walimu waliokufa kwenye ajali hiyo.


Alisema wizara yake ilimtuma Katibu Mkuu wake mkoani Kilimanjaro kupata majina ya walimu na wananfunzi waliokufa na waliojeruhiwa katika ajali hiyo kutokana na basi hilo kudaiwa kuwa na walimu na wanafunzi wengi.


Aliwataka walimu wakuu wa shule mbalimbali nchini kurudisha utaratibu uliokuwa ukitumiwa zamani wa walimu kusindikiza wanafunzi wakati shule zinapofungwa au kufunguliwa.


Alisema utaratibu huo, utawezesha shule husika, mzazi na wizara kuwa na uhakika wa usalama wa wanafunzi wakati wa kurudi shuleni au kwenda majumbani likizo.


Aidha, hadi sasa bado takwimu kamili za wanafunzi na walimu waliokufa na waliojeruhiwa hazijapatikana, ingawa baadhi ya wanafunzi waliojeruhiwa na walimu waliokufa wametambuliwa.


Waziri Sitta aliwataja waliokufa kuwa ni mwalimu wa sekondari ya Kileo Kilimanjaro, Bw. Adam Ramadhani na Mhasibu wa sekondari ya Nshupu, Arumeru, Bw. Magufya.


Aliwataja wanafunzi waliojeruhiwa ambapo wametambuliwa kuwa ni Athumani Msangi wa sekondari ya Moshi, Michael Mtori wa sekondari ya seminari ya Faraja, Kilimanjaro na mwingine aliyefahamika kwa jina moja la Selestine wa sekondari ya Majengo, Kilimanjaro.


Alisema vifo vya wanafunzi hao ni pigo kwa Taifa kutokana na vijana kuwa nguvu ya Taifa.


Katika suala la usafirishaji abiria, Waziri Sitta alisema vyombo vyenye dhamana vinatakiwa kuwa makini na usalama wa abiria wao, hususan katika suala la madereva kuwa makini.


Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents