Habari

Maiti Dar yakutwa na dawa za kulevya

POLISI jijini Dar es Salaam wamekuta kete 15 kwenye mwili wa marehemu waliyezuia asizikwe Jumanne iliyopita katika makaburi ya Sinza.

Waandishi Wa Habari Leo


POLISI jijini Dar es Salaam wamekuta kete 15 kwenye mwili wa marehemu waliyezuia asizikwe Jumanne iliyopita katika makaburi ya Sinza.


Polisi waliamua kuzuia maziko ya mwananchi huyo aliyekufa katika mazingira ya kutatanisha muda mfupi baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyeyere (JNIA).


Ilielezwa kuwa polisi walizuia maziko ya Leonard Chandika (48) baada ya kuwa na wasiwasi jinsi alivyofariki dunia muda mfupi baada ya kuteremka kwenye ndege akitokea Italia Jumatatu iliyopita.


Katika tukio hilo ambalo liliwaacha waombolezaji wakiduwaa, kundi la Polisi lilichukua mwili huo ukiwa kwenye jeneza nyumbani kwake Sinza Vatican, Jumatatu saa 11. 29 jioni ili kwenda kufanya uchunguzi kubaini sababu za kifo hicho.


Kwa mujibu wa habari hizo, Polisi walifika eneo la msiba na kusimamisha maandalizi ya ibada ya kuuaga mwili wa marehemu kabla ya kwenda kuzikwa katika makaburi ya Makumbusho, wilayani Kinondoni, hivyo kuliacha kaburi wazi.


Baada ya Polisi kusimamisha ibada, Mchungaji aliyekuwa tayari kuiongoza aliondoka nyumbani hapo saa 11.09 jioni kwa gari dogo la kukodi lenye namba za usajili T 293 AGX.


HabariLeo ilishuhudia jeneza lenye mwili wa Chandika likipakiwa katika gari aina ya Toyota Hiace namba T506 ACS ambalo lilisindikizwa na gari aina ya Land Rover 110 lenye namba T 201 AMV lililokuwa na polisi waliovaa kiraia.


Polisi walifika kwenye eneo la msiba muda mfupi baada ya mwili kutolewa Muhimbili Jumatatu asubuhi na walikuta waombolezaji wakijiandaa kuanza ibada ya kumuaga.


Wakati mwili unachukuliwa waombolezaji wengi walikuwa wameondoka kwa kuwa walikwisha kupata taarifa kuwa Polisi walikuwa wamezuia mwili huo usizikwe.


Hata hivyo, habari ambazo hazijathibitishwa na upande wowote zilidaiwa kuwa Chandika alifariki dunia Jumapili usiku akiwa na kiasi kisichojulikana cha dawa za kulevya tumboni.


Kwa mujibu wa habari hizo, hiyo ndiyo sababu iliyowafanya Polisi kusimamisha maziko ili kuufanyia uchunguzi wa kina mwili wa marehemu.


Inaelezwa kuwa baadaye Polisi walipigwa butwaa walipokuta mwili wa marehemu ulikwishapasuliwa, upasuaji ambao hadi jana ulikuwa haujafahamika ulikofanyika.


Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Jamal Rwambow alipotakiwa kuzungumzia suala hilo juzi, alisema angeweza kutoa taarifa kamili jana ambako alithibitisha mwili huo ulikutwa umepasuliwa.
Alisema Polisi wanaendelea kufanya uchunguzi kuwabaini waliohusika.
Habari nyingine zinasema kuwa baada ya Chandika kutua uwanjani, waliompokea walifanya jitihada za kumwahisha katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa vile alikuwa akilalamika kuumwa tumbo.


Inadaiwa magari mawili madogo ikiwamo teksi, yalitumika kuwabeba watu waliokwenda uwanja wa ndege kumpokea.


Walipompokea walimuona hali yake haikuwa nzuri kutokana na kulalamika kuwa alikuwa na maumivu ya tumbo, hivyo waliamua kumkimbiza hospitalini, lakini alifariki dunia kabla ya kufika Muhimbili.


HabariLeo ina taarifa zinazodai kuwa upasuaji huo ulifanyika Jumatatu asubuhi na kwamba wafanyabiashara wakubwa katika mtandao wa biashara ya dawa za kulevya walihusika kufanikisha kazi hiyo iliyofanywa na daktari mmoja.


Kamanda Rwambow alisema juzi kuwa polisi wamemkamata mke wa marehemu ili kumhoji, kwa kuwa wanahisi ni mmoja wa watu waliohusika kufanikisha kazi hiyo ya upasuaji.


Habari zilizopatikana zinasema watu wanne wanaoaminika kuhusika na tukio hilo nao walikamatwa juzi hiyo hiyo ingawa Kamanda Rwambow hakuthibitisha taarifa hizo.


Pia kuna taarifa kuwa baadhi ya ‘wanamtandao’ wa dawa za kulevya walitoroka eneo la msiba walivyoona polisi wanamiminika msibani hapo juzi.


Wakati HabariLeo ikiwa nyumbani kwa marehemu ilikuwapo minong’ono kuwa Chandika alifariki dunia katika hospitali moja maarufu jijini muda mfupi baada ya kurejea nchini kutoka Ulaya.


Kwa mujibu wa madai hayo, taratibu za kuutoa mwili huo katika hospitali hiyo zilifanywa haraka na ukapelekwa nyumbani kwa marehemu Jumatatu asubuhi kwa ajili taratibu za mazishi na maziko.


Juzi Kamanda Rwambow alikiri kuwa polisi walipata taarifa kuwa mtu huyo kabla ya kufa alikuwa amebeba dawa za kulevya hivyo walitaka kuthibitisha madai hayo na kama kweli ulikuwa umepasuliwa ili kutoa dawa hizo.


Kamanda Rwambow alisema baada ya kuuchukua mwili huo kutoka Sinza, Vatican, ulipelekwa katika Hospitali ya Mwananyamala kwa uchunguzi huo.


Souce: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents