Habari

Majadiliano Mkutano wa Hali ya hewa bado kizungumkuti

Majadiliano ya mkutano wa hali ya hewa wa Umoja wa mataifa COP 25, yanaendelea hii leo Jumapili huku wajumbe wakifanya jitihada ya kufikia makubaliano.

Spanien UN-Klimakonferenz 2019 COP 25 l Logo (picture-alliance/dpa/T. Brégardis)

Akiomba majadiliano hayo yaendeleee siku ya Jumapili, mwenyekiti wa mkutano huo na Waziri wa mazingira wa Chile Carolina Schmidt amesema lengo ni kupata muafaka.

Awali katika mkutano huo unaofanyika jijini Madrid, Uispania wanadiplomasia kutoka katika nchi tajiri, mataifa yanayoendelea pamoja na nchi masikini kwa sababu tofauti yalikataa rasimu iliyowasilishwa na nchi mwenyeji wa mkutano huo Chile, katika jaribio la kupata makubaliano ya pamoja.

Huku kukiwa na tahadhari za kisayansi, hali mbaya ya hewa kupindukia inayotokana na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na maandamano ya kila wiki yanayofanywa na mamilioni ya vijana, majadiliano ya mjini Madrid yalikuwa yakikabiliwa na shinikizo la kuonesha ishara kuwa serikali zina nia ya kupambana na mgogoro.

Lakini mazungumzo hayo ya siku 12 ambayo sasa yamepitisha muda wake yalikuwa mbali na kufikia lengo lake siku ya Jumamosi.

Wanaharakati wavunjika moyo kwa makubaliano kuchelewa

Mjumbe maalumu wa  masuala ya hali ya hewa kutoka visiwa vya Marshall Tina Stege alinukuliwa akisema “Inaonekana tunarudi nyuma kutokana na tamaa wakati tunatakiwa kusonga mbele kuelekea upande mwingine”. Mjumbe huyo aliongeza kusema “Nahitaji kwenda nyumbani na kuwaangalia wanangu machoni na kusema tulipata matokeoyatakayowahakikishia maisha ya baadaye , na maisha ya watoto wote.

Waangalizi  wakongwe wa mazungumzo ya hali ya hewa ya Umoja wa Mataifa walishangazwa na hali ya mambo kwa takribani saa 24 wakati majadiliano hayo yalipokuwa yamepangwa kukamilika yaliposhindwa kupata suluhisho. Mmoja wa wanaharakati wa mazingira  Alexandria Villasenor, mwenye umri wa miaka 14 alielezea kuvunjwa moyo na mkutano huo kushindwa kuchukua hatua na kwamba mkutano huo umewaangusha. Kwa mujibu wa makubaliano ya Paris yaliyofanywa mwaka 2015, nchi zilikubaliana kufanya kazi kuzuia ongezeko la joto duniani hadi kufikia kiwango cha chini ya nyuzi joto 2.

Juhudi za kuimarisha mpango wa kupunguza uzalishaji wa gesi ya ukaa, unaongozwa na visiwa vidogo na nchi  masikini pamoja na Umoja wa Ulaya. Mawaziri wa muungano wa zinazojiita ‘nchi zenye dhamira ya juu’  wamezitaka nchi za Marekani, Australia na Saudi Arabia wanazoziona kuwa kizingiti kufanya juhudi zaidi. China na India, ambazo ni namba moja duniani kwa kutoa hewa chafu zimeweka wazi kwamba hazioni haja ya kuboresha mipango yao ya kupunguza kiwango cha utoaji gesi ya ukaaa, mipango ambayo inafanya kazi hadi mwaka 2030.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents