Majambazi wateka kijiji, wapora maduka 20

KUNDI la majambazi wenye bunduki mbili aina ya SMG, mashoka, mapanga na marungu, wameteka kijiji cha Kangeme kata ya Ulowa wilayani Kahama na kupora maduka zaidi ya 20 huku wakiimba nyimbo za kumsifu Rais George Bush

Na Patrick Mabula, Kahama


KUNDI la majambazi wenye bunduki mbili aina ya SMG, mashoka, mapanga na marungu, wameteka kijiji cha Kangeme kata ya Ulowa wilayani Kahama na kupora maduka zaidi ya 20 huku wakiimba nyimbo za kumsifu Rais George Bush wa Marekani.

Majambazi hao waliingia katika kijiji hicho juzi saa mbili usiku na kufyatua risasi angani hali iliyofanya wananchi na wamiliki wa maduka kukimbia ovyo kuokoa maisha yao.

Huku wakiendelea kufyatua risasi majambazi hao walivamia baa moja ambapo walimkuta Diwani wa Kata hiyo, Bw. Kulwa Shinzi na wenzake, wakinywa na kuwaweka chini ya ulinzi huku wakiwapiga mateke na kisha kuwaacha na kufanya wakimbie ovyo.

Baada ya wafanyabiashara hap kukimbia maduka yao waliyavunja na kupora vitu mbalimbali zikiwamo simu za mkononi na fedha taslimu.

Wakati majambazi hao wakiendelea kuvunja maduka na kupora, baadhi ya wananchi walipiga simu Polisi wilayani hapa, umbali wa kilometa 90 kutoka Kahama mjini ili kuomba msaada wa haraka.

Polisi wa Kahama walikwenda kwenye tukio hilo lakini hawakuwakuta majambazi na kuanza kuwafatilia.

Baada ya majambazi hayo kuona gari likiwafuata walijificha, lakini kwa kuwa polisi walikuwa wakitumia gari la kampuni ya tumbaku, majambazi hao walipuuza na kutoka msituni na kuendelea na safari yao.

Baada ya kuona msafara wa majambazi hao wenye pikipiki na baiskeli waliwafyatulia risasi usiku huo na jambazi mmoja kupigwa yisasi mguuni lakini akatoroka na kutupa bunduki aina ya SMG.

Majambazi hao walizidiwa na kuacha pikipiki moja aina ya Sanlg, baiskeli mbili, bunduki hiyo na mwenzao aliyejeruhiwa mguu, lakini majambazi wote walitoroka usiku huo.

Katika hali ya kushangaza, wakati majambazi hao wakifyatuliana risasi na polisi, mwanamke ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja alijifungua ghafla baada ya kushtushwa na milio ya risasi.

Diwani Shinzi, alisema yaliteka kijiji hicho kwa muda wa saa tatu.

Jeshi la Polisi lilithibitisha kuwapo kwa tukio hilo na linaendelea na msako dhidi ya majambazi hao kwa kushirikiana na walinzi wa jadi.


 


Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents