Habari

Majambazi yang’oa mataruma, treni yapinduka

WATU 71 wamejeruhiwa na kulazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Tabora kutokana na ajali ya treni ya abiria iliyokuwa ikitokea Tabora kuelekea Dodoma kuanguka eneo la Cheyo mjini hapa.

na Moses Mabula na Murugwa Thomas, Tabora

 

WATU 71 wamejeruhiwa na kulazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Tabora kutokana na ajali ya treni ya abiria iliyokuwa ikitokea Tabora kuelekea Dodoma kuanguka eneo la Cheyo mjini hapa.

 
Ajali hiyo imetokea katika eneo la Cheyo mjini hapa ikiwa ni kilomita sita kutoka katika stesheni ya mjini Tabora, ambapo injini ya treni na mabehewa manne ya treni, yalianguka na kujeruhi watu hao.

 
Mabehewa yaliyoanguka jana yote yalikuwa ni yale yanayotumika kusafirishia abiria wa daraja la tatu, yenye namba 3627, 3606, 3519 na 3628, ambapo matatu yalitumbikia katika eneo hilo la daraja lililokuwa na maji.

 
Kwa mujibu wa Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Tabora-Kitete, Barnabas Mboje, majeruhi hao walianza kupokewa hospitalini hapo saa saba usiku, ikiwa ni nusu saa baada ya ajali hiyo kutokea.

 
Aliiambia Tanzania Daima kuwa kati ya majeruhi waliofikishwa hospitalini, wanaume walikuwa 42 na wanawake 29, mbapo wote walipatiwa matibabu na hali zao zinaendelea vizuri.

 
Dk. Mboje alisema kuwa, baadhi ya majeruhi hao ambao hata hivyo hawakutajwa majina, wameumia katika viungo mbalimbali mwilini huku baadhi yao wakiwa wameumia kichwani, mbavu, kuvunjika viuno, miguu na mikono.

 
Alisema kuwa uongozi wa Shirika la Reli nchini, ulihakikisha kuwa utatoa dawa kwa majeruhi hao, lakini hospitali hiyo ilikuwa na dawa za kutosha kukabili hali hiyo.

 
Dk. Mboje, alisema kuwa baadhi ya wagonjwa walikuwa wamepigwa (X – ray) kwa ajili ya kuangalia hali zao huku wengine wakiwa wamepelekwa katika chumba cha upasuaji, ili kuokoa maisha yao kutokana na majeraha waliyoyapata kuwa makubwa.

 
Habari zaidi kutoka eneo la tukio zinaeleza kuwa ajali hiyo ilisababishwa na hujuma dhidi ya shirika hilo, kwani kuna watu waliokuwa wamefungua reli kwa lengo la kuangusha treni.

 
Habari hizo zinaeleza kuwa watu hao walifungua treni hiyo kwa lengo la kuiba mizigo inayosafirishwa katika treni za mizigo kutoka Dar es Salaam, lakini hata hivyo treni iliyohusika na ajali hiyo ilikuwa ya abiria.

 
Hata hivyo, baadhi ya abiria waliripoti kuibiwa vitu kadhaa, ikiwamo fedha baada ya ajali hiyo kutokea.

 
Naye Ofisa Mkaguzi wa Shirika la Reli mkoani Tabora, Silivano Chenga, alisema kuwa ajali hiyo ilitokea katika eneo lenye umbali wa kilomita 834 kutoka jijini Dar es Salaam na aneo la ajali likiwa na urefu wa mita 600.

 
Alisema dereva wa treni hiyo aliyemtaja kwa jina moja la Sadiki, alinusurika na kwamba injini ya treni hiyo imeharibika vibaya pamoja na mabehewa hayo manne.

 
Baadhi ya abiria waliokuwa kwenye mabehewa yaliyoanguka, Amina Kassim na Mwanne Hassan, waliliambia gazeti hili kuwa baada ya ajali hiyo watu wengi walivamia eneo hilo na kuanza kupora kwa nguvu mizigo ya abiria na hata wao walipoteza mabegi yao mawili.

 
Walisema kuwa ajali hiyo ingekuwa mbaya zaidi iwapo mabehewa hayo yangetumbukia kwenye daraja lililokuwa jirani na mabehewa yaliyoanguka.

 
Walisema kuwa kabla ya kufika kwenye eneo la tukio, kichwa cha treni kilianza kuyumba na kuanguka, kikifuatiwa na mabehewa manne yaliyoanguka, mawili mkono wa kushoto na mawili mkono wa kulia.

 
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkaguzi wa Masoko wa TRC, Silvan Chenga, ambaye pia ni miongoni mwa abiria waliopata ajali hiyo jana, alisema reli hiyo imeharibika mita 30 baada ya kung’oka reli sita na kusababisha kichwa cha treni chenye namba 8833 kudondoka.

 
Hata hivyo, alisema treni hiyo inatarajiwa kuondoka leo mara baada ya treni ya kutoka Dodoma kwenda Mwanza na Kigoma itakapofika eneo la ajali ndipo abiria watabadilishana na treni iliyokuwa ikitokea Dodoma.

 
Alisema kuwa wale watakaofika na treni ya Dodoma watapanda treni ya Mwanza na wale waliotoka Mwanza na Kigoma watapanda treni ya kurudi Dodoma, kwani eneo la ajali bado halijatengemaa vizuri kutokana na kuwapo maji mengi.

 
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Muhud Mshihiri, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuahidi kulifanyia kazi ili kubaini chanzo cha ajali hiyo.

 
Alisema kuwa kumekuwapo malalamiko mengi kwa abiria kuibiwa mabegi yao ya nguo, viatu na vitu vingine vya thamani, na kuongeza kwamba mengi yamechukuliwa na askari kwa ajili ya usalama, hivyo kutoa wito kwa abiria kufika kituo cha Polisi cha Kati kuangalia mizigo yao.

 
Treni hiyo ya abiria ilikuwa na abiria zaidi ya mia sita ambao wanatoka mikoa ya Mwanza, Kigoma, Mara, Shinyanga, Kagera na Tabora.

 
Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents