Habari

Majambazi yapora milioni 42/-

Watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi, wamevamia duka la kuuza vifaa vya ujenzi la Five Star, lililopo karibu na Kanisa Katoliki la Kristu Mfalme mkoani Kilimanjaro na kupora kiasi cha Sh. milioni 42.

Na Victor Kwayu, PST Moshi


Watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi, wamevamia duka la kuuza vifaa vya ujenzi la Five Star, lililopo karibu na Kanisa Katoliki la Kristu Mfalme mkoani Kilimanjaro na kupora kiasi cha Sh. milioni 42.


Ilielezwa kuwa, majambazi hao walifika katika duka hilo na usafiri wa pikipiki na kumvamia mtunza fedha, Bi.Magreth Lawrence (57) ambaye alikuwa katika harakati za kuingia kwenye gari kupeleka fedha hizo benki.


Kwa mujibu wa Kamanda wa polisi Mkoani hapa, Bi.Hilda Kinabo, alithibitisha kutokea tukio hilo katika kikao na waandishi wa habari mjini hapa jana.


Alisema mtunza fedha huyo alikuwa akipeleka fedha hizo benki pasipo ulinzi wowote, kabla ya kuporwa na majambazi hao ambao walifanikiwa kutoweka na fedha hizo kwa kutumia usafiri wa pikipiki.


Alisema katika tukio hilo, watu watatu wanashikiliwa na polisi ambao ni mtunza fedha wa duka hilo Magreth Lawrent (57), Selestine Mbukwini (34) na Lazaro Aloyce (23).


Wakati huo huo, mwanamke mmoja, Mwajuma Masoud (45), mkazi wa mjini Moshi, alikamatwa akiwa na kete 92 za dawa za kulevya aina ya Heroin.


Kwa mujibu wa taarifa za polisi dawa hizo za kulevya zenye uzito unaokadiriwa kuwa gramu 46, zilikutwa katika mfuko wa nailoni nyumbani kwa mtuhumiwa aliyekamatwa kutokana na taarifa za raia wema.


Mtuhumiwa huyo anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote baada ya upelelezi wa shauri hilo kukamilika.


Katika tukio jingine mtu aliyefahamika kwa jina la Mganyizi Kasharankoro (25), mkazi wa kijiji cha TPC Moshi, alikamatwa na bunduki aina ya Riffle yenye namba 71526034 ikiwa na risasi tatu.


Bi. Kinabo alisema mtuhumiwa huyo alikuwa anamiliki silaha hiyo kinyume cha sheria za umuliki wa silaha, ambapo aliakamtwa kufuatia taarifa zilizotolewa na raia mwema.


Aidha mtuhumiwa huyo aliyekamatwa Desemba 10, mwaka huu naye atafikishwa mahakamani mara baada ya polisi kukamilsisha upelelezi wa tukio hilo.


Jeshi la polisi limetoa wito kwa raia wema katika maeneo yote kuendelea kulisaidia kwa kutoa taarifa mbali mbali za uhalifu hasa katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye sikukuu mbali mbali katika juhudi zake za kutokomeza uhalifu mkoani hapa.


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents