Habari

Majambazi yateka basi, yapora abiria mamilioni

WATU wanaosadikiwa kuwa majambazi wameteka basi dogo la abiria na kupora fedha taslimu zaidi ya sh. milioni 4.7 pamoja na simu za mikononi katika eneo la pori la kijiji cha Doroti, Tarafa ya Itigi wilayani Manyoni.

Na Hillary Shoo



WATU wanaosadikiwa kuwa majambazi wameteka basi dogo la abiria na kupora fedha taslimu zaidi ya sh. milioni 4.7 pamoja na simu za mikononi katika eneo la pori la kijiji cha Doroti, Tarafa ya Itigi wilayani Manyoni.


Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi mkoani Singida Bi. Celina Kaluba kwa vyombo vya habari, tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki iliyopita Novemba 29, saa 10.00 jioni.


Bi. Kaluba alisema basi hilo lilikuwa likitokea Manyoni kwenda kijiji cha Mgandu na kwamba lilipofika eneo la kijiji cha Doroti kwenye daraja linalotenganisha vijiji hivyo, ghalfa lilitokea kundi la majambazi yakiwa na silaha na kulisimamisha kwa kufyatua risasi angani.


Alisema dereva wa basi hilo aliyejulikana kwa jina la Bw. Mohamed Khalfani ilimlazimu kusimama ndipo majambazi hao ambao idadi yao haijajulikana, walianza kuwalazimisha abiria kushuka mmoja mmoja na kusalimisha kila alichokuwa nacho.


Hata hivyo alisema majambazi hao walifanikiwa kupora abiria wote fedha taslimu na simu za mkononi na kutokomea porini na kuwaacha abiria hao eneo la tukio.


Alisema baada ya majambazi hao kutokomea, mmiliki wa basi hilo ambaye naye alikuwepo na kuporwa shilingi laki 2.5 alipiga simu polisi Manyoni na polisi hao kufika mara moja eneo la tukio.


Polisi waliendesha msako mkali na kufanikiwa kuwakamata watu wawili wanaosadikiwa kuhusika katika tukio hilo.


Watu hao walitajwa kuwa ni Bw. Bakari Athumani (26) maarufu kwa jina la Luguli na Japhari Yusuf (46) maarufu kwa jina la Msacha wote wakazi wa Kiyombo Wilayani Sikonge mkoani Tabora.


Kamanda Kaluba alisema mara baada ya kuwafanyia upekuzi mtuhumiwa Luguli alikutwa na bunduki aina ya gobore inayotumi risasi za fataki.


Bi. Kaluba alisema mtuhumiwa Luguli aliweza kutambuliwa na baadhi wa abiria waliokuwa ndani ya basi hilo, hivyo kuwarahisishia polisi kazi ya kumkamata.


Wakati huo huo mtu mmoja mkazi wa kijiji cha utaho, amefariki dunia papo hapo baada ya kugongwa na gari lisilojulikana.


Mtu huyo ametambuliwa kwa jina la Rajabu Shabani (25) mkulima na mkazi wa kijiji hicho, hata hivyo gari hilo lilitoweka baada ya kumgonga na polisi wanafanya upelelezi kulibaini.


Wakati huo huo polisi mjini hapa wamefanikiwa kulikamata jambazi sugu lililotajwa kwa jina la Ramadhani Sadi (41) likiwa na bunduki aina ya SMG, magazine moja pamoja na risasi 27 likiwa safarini kutoka Singida kwenda Karatu mkoani Manyara kwa ajili ya kufanya uhalifu.


Kamanda Kaluba alisema jambazi hilo lilikamatwa mwishoni mwa wiki iliyopita likiwa ndani ya basi la Hajjis lililokuwa likitokea Singida kwenda Hydom wilayani Manyara.


Bi. Kaluba alisema mara baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema, polisi waliweka mtego katika kijiji cha Kijota Tarafa ya Mtinko Singida vijijini kwa kisingizio cha kulikamata basi hilo kutokana na makosa mbalimbali yakiwemo ya usalama barabarani.


Alisema basi hilo lenye namba T 500 AKV, lilipofika Kijota askari walilisimamisha na walipoingia ndani na kuanza kufanya upekuzi, walikuta begi jeusi.


“Askari walilitilia shaka begi hilo na kuanza kuhoji mmiliki wake ndipo abiria, walimtaja mtuhumiwa Sadi kuwa ndiye aliyepanda na begi hilo kituo kikuu cha mabasi Singida, “alisema Bi Kaluba.


Kamanda Kaluba alisema hata hivyo mtuhumiwa alianza kukataa kwamba begi hilo si mali yake ndipo abiria walichachamaa na kudai kuwa ndiye mwenye nalo na hana sababu ya kukataa mali yake.


Alisema hata hivyo silaha hiyo ilikuwa imekatwa kitako huku ikiwa imefichwa na kufukikwa kwa majaketi mawili makubwa.


Alisema polisi bado wanaendelea na mahojiano na mtuhumiwa huyo ili kubaini mtandao wao na kuusambaratisha.


Kamanda Kaluba aliwashukuru wananchi kwa ujasiri wao wakumtaja mtuhumiwa huyo na kwamba endepo wataendelea na ushirikiano huo, polisi jamii inaweza kufanya kazi kwa mafanikio zaidi.


Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents