Habari

Majeruhi wa Lucky Vincent watua Arusha, Tsh bilioni 1.7 zatumika kwa matibabu

Wanafunzi watatu wa Shule ya Lucky Vincent ya Mkoani Arusha waliopelekwa nchini Marekani kwa matibabu kutokana na kupata ajali mbaya wanarejea leo nchini huku matibabu yao ‘yakigharimu’ Sh1.7 bilioni.

Watoto hao ambao ni Doreen, Sadia na Wilson waliokuwa wakitibiwa katika Hospitali ya Mercy, Sioux City, Marekani tayari wamewasili wa ndege ya Samaritan,s Purse wakitokea nchini humo baada ya kupata nafuu.

Mamia ya wakazi wa Arusha, ndugu, jamaa, marafiki na viongozi mbalimbali wa serikali wamefika kwa ajili ya kuwapokea watoto hao. Baadhi ya viongozi hao ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira, Mbunge Lazaro Nyarandu makatibu tarafa wa mikoa na viongozi wa wilaya za mikoa ya Arusha na Kilimanjaro.

Akizungumzia kuhusu ujio wa watoto hao jana, Mbunge wa Singida Kaskazini ambaye pia ni mwenyekiti mweza wa Shirika la Stemm, Lazaro Nyalandu alisema tayari wameondoka Marekani na matibabu na gharama nyingine zikiwamo za usafiri ni zaidi ya Dola 800,000 za Marekani (Sh1.7 bilioni).

“Gharama iliyotumika ni kubwa ila hakuna fedha iliyotolewa kwa sababu kila hatua iliyohitaji malipo wahusika walijitolea, Marekani huwa gharama za daktari, wauguzi na hospitali zinalipwa tofauti. Pia, Doreen baada ya kutakiwa kufanyiwa matibabu ya juu zaidi kwenye Kituo cha Madona, Nebraska kinachoheshimika zaidi duniani gharama zake ni Dola 50,000 (Sh100 milioni) kuingia tu,” alisema.

Nyalandu alisema hata gharama za ndege ya Samaritan Purse inakadiriwa kufikia Dola 300,000 za Marekani (Sh600 milioni) kwa safari ya kutoka Marekani hadi Kia na kurudi, hali inayoonyesha kama ingekuwa kulipia gharama ingekuwa changamoto.

Wanafunzi hao waliondoka nchini Mei 14 kwa ajili ya matibabu kwa usafiri wa Shirika la Ndege la Samaritan Purse linaloongozwa na Mchungaji Franklin Graham wa Marekani, ukiwa ni msaada wa taasisi yake baada ya kuombwa kufanya hivyo.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents