Habari

Maji yakwamisha masomo UDSM

UHABA wa maji uliolikumba Jiji la Dar es Salaam kwa zaidi ya wiki tatu sasa, umesababisha baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, sehemu ya Mlimani kushindwa kuingia darasani.

na Agnes Yamo

 

UHABA wa maji uliolikumba Jiji la Dar es Salaam kwa zaidi ya wiki tatu sasa, umesababisha baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, sehemu ya Mlimani kushindwa kuingia darasani.

 
Wakizungumza na Tanzania Daima wiki iliyopita, baadhi ya wanafunzi wa chuo hicho walisema wanashindwa kuingia darasani bila kuoga kwa sababu hakuna maji chuoni hapo.

 
Walisema tangu tatizo la uhaba wa maji lilipoanza, mahudhurio yao darasani yamekuwa hafifu kwa sababu wanatumia muda mwingi kutafuta maji.

 
Wanafunzi hao ambao hawakutaka majina yao yaandikwe bazetini walisema hawapendi kukosa masomo lakini hali ya ukosefu wa maji chuoni hapo imekuwa mbaya na viongozi wanaonyesha kutokerwa nayo, kwa sababu wanapata maji ya kununua kutoka nje ya chuo.

 
“Hali ni mbaya kuanzia chooni hadi kwenye usafi wetu wa mwili, vyoo vinafanyiwa usafi kila asubuhi lakini kwa sababu hakuna maji ya kusafisha uchafu, baada ya kujisaidia tunaondoka bila kusafisha uchafu.

 
“Wakubwa hawashtushwi na hali hii kwa sababu wanapata maji ya kununua, lakini kwa sababu yakilipuka magonjwa ya kuambukiza itakuwa hatari, kuna watu kupoteza maisha, afya zetu ziko hatarini,” alisema mwanafunzi mmoja wa mwaka wa pili wa kitivo cha sheria.

 
Baadhi ya wanafunzi wanaoishi katika hosteli ya Mabibo, Dar es Salaam waliohojiwa na gazeti hili kuhusu hali hiyo, walisema nao pia wako katika tatizo hilo na wameathirika zaidi kwa sababu wanakaa mbali na chuo.

 
Mwenyekiti wa Chama cha Wanafunzi wanaosoma Sayansi ya Siasa, Herman Edcar, alisema tatizo la maji linawaweka katika hali ngumu wanafunzi wanaoishi katika hosteli hiyo kwa sababu wengi wanaishi kwa wasiwasi wa kukumbwa na magonjwa ya mlipuko.

 
“Leo ni siku ya nne hatuna maji hapa Mabibo, miaka yote tumekuwa tukiletewa maji na magari, wanatujazia katika ‘sim tank’ ingawa huwa hayatoshi lakini yanatusaidia, lakini sasa hayapo kabisa,” alisema mmoja wa wanafunzi wanaoishi katika hosteli hiyo.

 
Alisema kuwa kupungua kwa idadi ya magari yanayopeleka maji chuoni hapo kumesababisha baadhi ya wanafunzi kuamka saa 11:00 asubuhi kwenda nje ya chuo kutafuta maji.

 
“Utakuta magari yanamwaga maji asubuhi katika hayo matanki, ambapo kila ghorofa lina matanki mawili, wanafunzi tunapanga foleni ili kupata maji, ukijipanga foleni saa 12, unapata maji saa 2 au saa 3, ukienda darasani unakuta umeshapitwa na vipindi,” aliongeza mwanafunzi huyo.

 
Alisema mapema Januari Kamati ya Bunge inayoshughulikia Huduma ya Jamii ilitembelea hosteli hiyo na kuelezwa matatizo ya maji.

 
Hata hivyo alisema hawana imani na baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo kwa sababu wanaonekana kutoguswa na tatizo hilo.

 
Alisema wakati wa kikao cha Bunge kilichopita walimsikia Mbunge Amina Chifupa akiuliza swali juu ya tatizo la maji kaktika hosteli ya Mabibo, Mwenyekiti wa kamati alitoa majibu yasiyo na ukweli kuwa tatizo hilo limekwisha na magari hayaleti maji tena kwa kuwa sasa kuna mabomba yanayoleta maji moja kwa moja.

 
“Ukweli ni kwamba jengo hili lina zaidi ya miaka saba lakini halina maji, tangu kuwekwa kwa mfumo wa maji, hayajawahi kutoka, na ukisikia shida ya maji ujue magari hayajaleta maji au yameleta kidogo, kwa kuwa hapa tupo zaidi wa wanafunzi 6,000, hivyo maji ni lazima yasiwe ya kusuasua,” alisema.

 
Pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, maeneo mengine ya Jiji yaliyokumbwa na uhaba wa maji ni Tandika, Magomeni, Tabata, Pugu, Mwenge, Tegeta, Kawe, Mabibo, Manzese, na Changanyikeni.

 
Maeneo mengine ni Mwananyamala, Kijitonyama, Namanga, Mikocheni, Msasani, Buguruni, Temeke, Ubungo, Kinondoni, Gongolamboto, Uwanja wa Ndege, Kiwalani, Mburahati pamoja na Kimara.

 
Taarifa iliyotolewa hivi karibuni na Kampuni ya Huduma ya Majisafi na Majitaka katika Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani (DAWASCO) kwa vyombo vya habari juu ya tatizo la maji, ilieleza kuwa linasababishwa na kuharibika kwa pampu moja ya maji ghafi kutoka katika mtambo wa Ruvu Chini.

 
Taarifa hiyo ilieleza kuwa kutokana na kutokuwapo kwa pampu ya tahadhari, uzalishaji wa maji umepungua kwa asilimia 45.

 
Ilieleza kuwa matengenezo ya pampu hiyo yameanza Februari 12 na yanatarajiwa kumalizika Februari 15, ambapo uzalishaji wa maji unatarajiwa kurejea Alhamisi usiku Februari 15, lakini hadi sasa uzalishaji wa maji bado haujarejea.

 
Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents