Bongo5 Makala

Makala: Beka Flavour, Aslay ni moto umeuchochea na umewaka, kazi kwako kuuzima

Aliyekuwa Rais wa 16 wa Marekani, Abraham Lincoln aliwahi kunukuliwa akisema, “Ninafanya vizuri kwa namna ninavyojua na ninaweza kuwa bora, ninamaanisha nitaendelea kufanya hivyo hadi mwisho”.

Beka na Aslay

Leo August 10, 2017 ninapoandika haya kila mmoja kutoka Yamoto Band anafanya kazi kwa utaratibu wake (solo project) lakini katika vile vichwa vinne Aslay anaonekana kufanya  vizuri zaidi kuliko wenzake. Narudia tena, anafanya vizuri na anayemfutia kwa ukaribu ni Beka Flavour, lakini sidhani kama anastahili kutajwa kuwa ni mshindani wa Aslay ukitazama kazi zake, bali anapata nafasi hiyo kutokana walikuwa kundi moja.

Beka Flavour alipowasha moto

 July 19, 2017 Aslay alitoa video ya wimbo wake Baby, siku kadhaa mbeleni yaani July 25 Beka Flavour kupitia kipindi cha E-Newz cha EATV alisema alikuwa na mpango wa kutoa ngoma mpya lakini kutokana Aslay ametoa yeye amehairisha wiki mbili mbele na kuonya kuwa endapo Aslay atatoa tena hatomvumilia.

“Aendelee kutoa tu. akitoa baada ya wiki mbili mbele hapo siwezi kusubiri na mimi natoa mashine, kwa sababu mimi ndio nimepanga wiki mbili mbele kwa hiyo akitoa tena siyo mbaya zikipambana,” alisema Beka.

Chukua hii, Aslay aliposikia hilo alijibu, “Mfano mdogo Libebe imepita na hata angeamua kutoa ngoma na mimi zingekutana huku mjini na kila shabiki angependa ngoma kwa wakati wake,” alisitiza.

Jibu la Aslay ndani yake kuna chembe chembe za maneno ya Abraham Lincoln, kwani hakutilia mkazo maneno ya Beka Flavour. Naomba kurudia tena, hakutilia mkazo maneno hayo, ndio maana jana August 9, 2017 alitoa ngoma nyingine mpya ‘Likizo’.

Zikiwa ni wiki mbili zimepita tangu atoe wimbo wa Baby, wiki mbili ambazo Beka alitangaza kutoa wimbo mpya kitu ambacho hadi sasa hajafanya hivyo, kumbe alikuwa anachochea moto bila kujua sasa umeweka. Beka Flavour toa wimbo wako ili tuanze kuamini katika maneno yako, pia uweze kuzima moto uliowasha.

Beka Flavour ana safari refu zaidi

Tangu Yamoto Band kuanza kazi za solo project Aslay ametoa nyimbo nyingi kama Angekuona, Usitie Doa, Baby, Likizo, Muhudumu na nyinginezo na zote zinafanya vizuri, wakati Beka Flavour ana wimbo mmoja tu mkononi, Libebe.

Hivyo basi hata endapo Beka akitoa wimbo kwa sasa bado ana mlima mrefu wa kupanda, ingawa mfumo wa Aslay wa kutoa nyimbo nyingi kwa wakati mmoja umekuwa ukikosolewa na baadhi ya watu na wengine kuunga mkono, ila hiyo haitaondoa ukweli kuwa Beka ana kazi ya ziada.

Nayakumbuka maneno ya Ben Stein, kuwa “hatua ya mwanzo na muhimu kupata kile unachotaka katika haya maisha ni kuamua ni kitu gani unataka”.  Hivyo Aslay ameamua kile anachokitaka katika muziki wake ni kutoa ngoma nyingi kwa sasa, huenda malengo yake yanamruhusu kufanya hivyo na malengo ya Beka yanamruhusu kutoa ngoma moja na kuipa nafasi ya kufanya vizuri, lakini nani anaelewa hilo?.

Jana kupitia ukurasa wake wa Instagram, Beka aliweka kipande cha video mpya Aslay ‘Likizo’ na kuandika, “Hayahaya wadau wanamwitaga @aslayisihaka kaja hii safari #likizo suport mziki mzuri @chambusso. Ukija ukasoma comment utaona mashabiki wake kuna kitu wanataka kwa sasa.

dasnipe_walesAah nawew amsha dude maana ulihaidi

samrespect2mainBeka tunataka mzigo mpya achana na hizo habari za Aslay

selestinesilvesterMziki Sio Vita Bali Mziki ni Ubunifu Hongereni Sana @bekaflavour@aslayisihaka Kwa Kuonyesha Mnaweza Hii Ni Changamoto Kwa Vijana wengine Wanao Fanya Mziki Naimani Hamto Weza Kujengeana Chuki Isipo Kua Mtajengeana Changamoto Ya Kufanya Mziki Mzuri Cc Twawapenda Woteeeeeeee.

baby_x_one@bekaflavour tunataka na ww ulituhaidi kuachia nyimbo plssss

johnawaliimremaVp mzee baba mbona yako huachii achia bana sio poa! Team beka tupo tunasubiria mashine!

Mtazamo wa wasanii wengine

Katika mtindo wa wasanii kutoa nyimbo nyingi kwa wakati mmoja kama anavyofanya Aslay kwa sasa, wasanii baadhi yamekuwa na mtazamo tofauti katika hilo, miongoni mwao ni Barnaba, Shetta na Nikki wa Pili.

“Aslay anafanya vizuri kwa sasa, hatumii nguvu, aombi interview, hafanyi interview nyingi sana, ni mtu ambaye amechagua system yake binafsi na ile mimi naita local target in market, I like that. Kitu kibaya ambacho tunafanya wasanii wakubwa tunajisahau, tunafanya commercial kuliko hata kuandika,” amesema Barnaba, hivyo anaunga mkono hilo.

Kwa upande wake Shetta haamini katika kutoa ngoma nyingi kwa kipindi kifupi, “Mimi siamini kwenye kutoa nyimbo nyingi ndio ku-trend, nafikiri kujipanga kwangu ndio huwa kuna sababisha kukaa muda mrefu bila kutoa wimbo”.

Nikki wa Pili naye ana hili, “Drake, Wizkid, Davido, Dj khaled, Major Lazer nawasikia kwenye media mbali mbali hapa nyumbani wakisifiwa kuwa wanakimbiza kwa kuwa wana hits nyingi kwa wakati mmoja.

“Lakini kama msemaji wa Weusi nimekuwa nikihojiwa na media kibao kuwa kwanini mmetoa hits zenu haraka haraka hamuoni mnauwa track zenu wenyewe????? halafu hapo hapo wanakuuliza nini kifanyike ili muziki wa Tanzania ukue???? Kazi itakuwaje kama wafanyakazi wakifanya kazi wanaambiwa wanauwa kazi???,” amehoji Nikki, hivyo anaunga mkono.

Hadi kufikia hapo sina budi kupumzisha kalamu yangu, Beka Flavour uamuzi ni wako kuuzima moto uliouwasha au kuuacha uendelee kuwaka.

By Peter Akaro

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents