Burudani

Makala: Bonta unamuona Jux kwa Weusi?

Ni nyakati pekee ambazo zinaweza kubadili mambo katika ulimwengu huu. Nyakati hufanya yale yaliyokuwa yanavuma kufifia au hata kupotea kabisa. Nyakati pia zina nguvu katika ulimwengu wa burudani, ndio maana alikuwepo R Kelly na leo yupo Justin Beiber. Kwa sasa kundi la Weusi linafanya vizuri kwa ujumla na hata kwa upande wa msanii mmoja mmoja, ni nyakati zao.

Ujio wa Weusi ni muungano wa wasanii kutoka kundi la River Camp Soldiers na Nako 2 Nako Soldiers. Sote tunakumbuka makundi haya yalivyokuwa yanafanya vizuri. Nako 2 Nako walikuwa wanapakua ‘hit’ baada ya ‘hit’, ikafika wakati nyakati zikabadilika maisha hayo yakapita.

Kupungua kwa nguvu ya Nako 2 Nako Soldiers hata kuondoka kwa Ibra Da Hustler, ukawa ni mwanzo mzuri wa kuzaliwa kwa Weusi. Lord Eyes na G Nako ndio pekee walionekana kuwa na nguvu ukilinganisha na Bou Nako. Wakati huo G Nako walikuwa ameshafanya kazi kadhaa na ‘River Camp Soldiers’.

Utakumbuka wimbo kama ‘Pea’ ambao G Nako alifanya na Nikki wa Pili na Joh Makini, pia Kilimanjaro aliyofanya na Joh Makini na Lady Jaydee. Wakati huu Weusi ilikuwa bado haijazaliwa, ila Joh Makini alipenda kuinada ‘Brand’ iliyotambulika kama GMF (Good Music Family).

Ujio wa Weusi

‘Hakuna playlist bila Weusi’. Hiyo ni moja ‘line’ zilizopo katika wimbo ujulikanao kama ‘Ngoma Nzito’ aliyofanya G Nako, Lord Eyes pamoja na Fundi Samweli ambaye pia ni prodyuza wa wimbo hiyo. Mstari huu ulimaanisha hata Lord Eyes na G Nako wanaweza kusimama kama Weusi. Kwa maana hiyo ulikuwa ni mwisho wao wa kutambulika kama Nako 2 Nako Soldiers, tuweke nukta hapo.

Hapo nyakati za Nako 2 Nako zikawa zimefika ukingoni na tukafungua ukurasa mwingine (Weusi). Nyakati hizi Weusi ikatambulika kama Kampuni au kundi la muziki lenye wasanii watano.

Weusi ilikuwa ya Joh Makini na Bonta ambao walikuwa Rivers Camp Soldiers, pamoja na Nikki wa Pili ambaye alikuwa mtu wa karibu wa kundi hilo kama alivyothibitisha Joh Makini kwenye kipindi cha Mkasi 2015. Idadi ya watu watano ikakamishwa na Lord Eyes na G Nako kutoka Nako 2 Nako Soldiers kama nilivyotangulia kueleza.

Kundi hili la vichwa vitano ilikuwa ni vigumu kuwapata ndani kazi moja kama ilivyokuwa kwa makundi kama Tip Top Connection na TMK Wanaume ambao waliweza kukaa wasanii zaidi watano ndani ya ngoma moja. Naikumbuka ngoma yao iitwayo ‘Watoto wa Mungu’ ambayo walifanya pamoja wote. Kama kumbukumbu zangu zipo sawa hii ndio ngoma pekee iliweza kuwaweka pamoja. Lakini hata hivyo ngoma hii haikuwa ‘promoted’ sana kama zilivyo ngoma zao nyingine.

Bonta alijaribu kuwaleta pamoja katika wimbo wake alioupa jina la ‘Pigeni Mawe’ ambao walifanya wote isipokuwa Lord Eyes. Maisha yakaendelea na nyakati hizo zikapita.

Tabaka kati yao

Kadri siku zilivyozidikwenda kulianza kuonekana makundi mawili ndani ya kundi moja (Weusi). Kundi la kwanza ni la Joh Makini, Nikki wa Pili, na G Nako. Kundi lingine ni la Bonta na Lord Eyes.

Kazi walizokuwa wanatoa kundi la kwanza na hadi sasa zinaonekana kufanya vizuri kuliko la kundi la pili. Bonta mara nyingi amekuwa na muziki wake pekee ambao kiuhalisia hauendani na kundi la kwanza, hilo lakini halikuwa tatizo kwao. Tabaka lilionekana wazi lilipokuja suala la Lord Eyes. Mara kadha alikuwa akisimishwa ndani ya kundi kwa kile kilichoelezwa ni kwenda kinyume na taratibu za kundi/kampuni.

Mwishoni akawa nje kabisa ya kundi hilo hadi pale tuliposikia amesainiwa kuwa chini ya usimamizi wa msanii Barakah The Prince. Kitendo cha yeye kuwa chini ya usimamizi huo kinaweza kutafsiriwa kama hayupo tena pamoja na Weusi. Hivyo kundi hilo linabakia kuwa na ‘member’ wanne tu.

Kuibuka kwa Jux

Kwa mara ya kwanza kumsikia Jux katika kundi la Weusi ni pale alipopewa shavu na Nick wa Pili katika wimbo wa ‘Safari’. Wimbo huu ulikutanisha ‘vichwa’ kama Joh Makini, G Nako, Vanessa Mdee, Nahreel na Aika (Navy Kenzo).
Baada hapo Jux alikuwa karibu sana na Weusi, na hii ni kutoka alikuwa na kazi zake binafsi studio kwa Nahreel (The Industry) ambapo ilikuwa ni ngome kuu ya Weusi.

Chini ya ngome hiyo (The Industry) Jux ameshatoa nyimbo mbili ambazo ni One More Night na Looking For You aliyompa shavu Joh Makini. Hapa Jux alianza kuwa ‘mtiifu’ wa kundi hilo kwani hata kwenye baadhi ‘show’ wamekuwa wakifanya pamoja.

Kama hiyo haitoshi Jux na G Nako wamekuwa na muunganiko (chemistry) ambao unaweza kuifanya ngoma yoyote ile kuwa ‘hit’ na ndio si ajabu kuona wanapewa shavu pamoja katika ngoma moja. Bila shaka unaijua ngoma ya Quick Rocka ‘Hapo’. Ngoma hii waliikutana wote na kutoa burudani ya kukata na shoka. Pia kumbuka remix ya ngoma ya Belle 9 ‘Movie Selfie’ wawili hawa walikuwepo pamoja na wakali kama Izzo Bizness, Maua Sama na Mr Blue, weka nukta hapo.

Kilichonihamasisha kuandika ujumbe huu, ni pale niliposikia ngoma waliyofanya pamoja G Nako na Jux ‘Go Low’. Ngoma hii ni ‘level’ nyingine kwa wote wawili na kundi la Weusi kiujumla. Ni wazi ukaribu wa Jux kwa kundi hilo unaonekana kuwa na nguvu kuliko hata ule wa Bonta na Lord Eyes. Lakini hilo halina tatizo kwa pande zote ilimradi lengo linafikiwa. Lengo la kutoa burudani na kufanya biashara pia.

Kwanini Bonta

Bila shaka unajiuliza kwanini nimetangulia kumtaja Bonta katika makala haya. Bonta akiwa kama mtu wa nne au wa mwisho katika kundi, ni kwamba nafasi yake inaonekana kuchukuliwa na Jux. Huu ni mtazamo wangu unaweza kuukubali au kuupinga pia. Nyakati zimemuacha nyuma Bonta ndani ya kundi na wenzake wanakazana kuendana na wakati uliopo. Wakati ambao unahitaji kutengeneza muziki wa kibiashara na kuwekeza muda na fedha.

Mambo haya mawili yamemshinda Bonta. Kwanza yeye anaamini katika aina yake ya muziki ambao anaufanya. Muziki kwa ajili ya watu wake wa mtaani, kushikilia msimamo huo ni moja ya sababu za mwezake kumuacha nyuma. Jambo la pili ni uwekezaji wa fedha na muda. Sote tunaona jinsi lile kundi la kwanza nililotangulia kulitaja jinsi linamwanga fedha katika kutengeneza nyimbo na video zao, suala hilo limeshinda kabisa Bonta, video anazotoa zimekuwa za kawaida sana na hata hajitoi sana kuutangaza (promotion) muziki wake.

Pia niligusia uwekezaji wa muda katika muziki wake, hili kwake limekuwa ligumu kutokana na majukumu alinayo ya kuitumikia jamii nje muziki. Bonta ni daktari hivyo muda mwingi anakuwa amejikita katika kazi yake, weka nukta hapo pia. Kutokana na sababu hizo nilizotangulia kuzieleza hapo juu. Bonta anaweza kuitafakari nafasi yake ndani ya Weusi na ukaribu wa Jux katika kundi hilo.

Faida na hasara kwa Jux

Ukaribu wake na Weusi unaweza kuwa na faida kwake kibiashara na kundi hilo pia. Lakini jinsi ambavyo Bou Nako anavyoumia kuona ‘member’ wenzake walivyondoka Nako 2 Nako Soldiers na kwenda kunzisha Weusi, ndivyo hivyo kundi la Wakacha linavyojiuliza kwa Jux.

Jux ni ‘member’ wa kundi la Wakacha ambao linaundwa na yeye pamoja na Cyril na Gigga Flo. Ni wazi hasara itakuwa kwa kundi hilo ambalo kila mara limekuwa likitangaza ujio mpya lakini hawafanyi hivyo.

Imeandika na Peter Akaro
Author Professional: Journalist.
Contact: 0755 299596.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents