Tupo Nawe

Makala: Darassa unasinzia na fegi, utachoma kibanda (+Audio)

Si Darassa pekee, yeyote mpenda muziki wa nchi hii ukimuuliza wimbo mkubwa kutoka kwa rapper huyo ni lazima atataja ngoma ya muziki iliyotoka November 2016. Ni wimbo ambao ulimuweka katika ramani nyingine kabisa kimuziki, pia ulimuwezesha kufanya show nyingi zaidi na kubwa, hivyo kuna uwezekano mkubwa pia ngoma hiyo ilimuingizia fedha nyingi zaidi.

Licha ya wimbo huo hadi sasa kufikisha views zaidi ya Milioni 12 katika mtandao wa YouTube na kuwa wimbo wa kwanza kutoka kwa Darassa kufanya hivyo, bado ni vigumu kuelezea ukubwa wake kwa lugha rahisi yenye kueleweka na wengi.

Rais Jahmuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli akiwa katika ziara mkoani Mtwara wakati akihutubia alinukuu maneno kutoka kwenye wimbo huo. Nanukuu; ‘Mkiambiwa changanya kama karanga ndio mnachanganyikiwa kabisa’.

Baada ya Rais Magufuli kumaliza sentensi hiyo kilichofuata ni shangwe la aina yake utasema Darassa mwenyewe ndiye anatumbuiza katika uwanja aliokuwa akihutubia Rais. Hivyo basi, hadi Rais Magufuli kuzungumza hivyo ina maana anaujua wimbo huo na pia aliupenda kwa namna moja au nyingine. Huo ndio ukubwa wa ngoma hiyo.

Twende Na Muziki

Katika wimbo wa Muziki kuna mstari Darassa anasemma; ‘Sinzia na fegi uchome kibanda’. Ni mstari wenye maana pana zaidi, rapper huyo aliandika mstari huo kwa ajili ya kulikumbusha kundi fulani katika jamii kuwa makini na yale watendayo ila katika makala haya mstari huo ni maalum kwa Darassa mwenyewe.

Fegi ya Darassa kwa sasa ni ukimya wake katika muziki, kibanda chake ni mashabiki wake waliokuwa naye beka kwa beka kwa kipindi kirefu. Hivyo, akiendekeza fegi atachoka kibanda; maana yake ni kwamba, akiendelea kuwa kimya atapoteza mashabiki wake.

Toka alipotoa wimbo ‘Hasara Roho’ May 2017 hajatoa wimbo mwingine wowote, hata hajasikika katika wimbo wowote alioshirikishwa na wasanii wengine. Mbaya zaidi toka August 12, 2018 hajaposti chochote katika kurasa zake za mitandao ya kijamii, this is too much.

Kutotoa wimbo mpya sio ishu kuna wasanii wengi wanakaa hata miaka miwili na baadaye wanarudi vizuri tena sana katika muziki.

Mfano mzuri ni Alikiba, tangu alipotoa wimbo wa Aje alikaa kimya zaidi ya mwaka mmoja bila kutoa wimbo hadi pale alipokuja kutoa wimbo uitwao Seduce Me. Kipindi cha ukimya wake aliweza kushirikishwa na wasanii kama Nuh Mziwanda, Baraka The Prince, Abby Skillz na Mr. Blue, pia alikuwa anajichanganya na kuonekana katika matukio mbali mbali lakini ni tofauti na Darassa.

Ukichoma kibanda!; Is Too Much

June 30, 2016, Darassa alikuwa na mkutano wa waandishi wa habari katika ukumbi wa Habari Maelezo Posta Dar es Salaam. Wakati huo alikuwa akifanya vizuri na nyimbo zake mbili ambazo ni Heya Haye aliomshiriksha Mr. Blue na ule aliomshirikisha Rich Mavoko uitwao Kama Utanipenda.

Nitakupa mambo mawili kutoka kwenye mkutano huo, mosi; alizungumzia ujio wa ngoma yake inayokwenda kwa jina la Too Much, pili; ni ujio wa label yake, Classic Music Group (CMG) ambayo alieleza kuwa itaanza kusimamia wasanii.

Wimbo wa Too Much ukaja kutoka Jully 15, 2016 na kufanya vizuri lakini katika label bado hakuna chochote kilichofanyika kama alivyoeleza. Binafsi, nafikiri kipindi hiki ambacho amekuwa kimya ndio ulikuwa wakati wa kuwatoa wasanii kutoka kwenye label yake.

Moja ya sababu alizotaja Diamond Platnumz kutochaguliwa kuwania tuzo za BET kwa mwaka 2017, alieleza hakutoa ngoma nyingi kali kwa sababu alikuwa akitoa nafasi kwa wasanii walio katika label yake, WCB wapate kusikika, ndicho namaanisha kwa Darassa.

Hata hivyo Darassa ameamua kusinzia na fegi, yaani kuwa kimya, huku akielekea kuchoma kibanda, yaani kipoteza mashabiki wake, na ikishakuwa hivyo suala la label litafanikiwa vipi?. Ikishafika hatua hiyo tunasema is Too Much maana atakuwa si msanii wa kwanza kutoa ahadi kama hiyo na kutoitimiza. Twende bila haraka.

Vipi hizi stori mbaya kuhusu yeye baada ya kusinzia na fegi ingawa hakuna uthibitisho wa moja kwa moja kuhusu hilo lisemwalo?. Kama ni kweli itakuwa is Too Much maana si msanii wa kwanza wa Bongo Flava kuhusishwa/kuwa katika ishu kama hizo, chonde chonde Darassa usichome kibanda nafasi yako bado ipo wazi katika Bongo Flava. Shukrani.

Related Articles

Back to top button
Close
Bongo5

FREE
VIEW