Promotion

Makala: Jinsi Vodacom ilivyosalimu ‘Amri’ kwa Yanga, TFF, kamati ya ligi zikizodoka

Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Laurence Mwalusako akizikagua jezi walizopewa na mdhamini wa ligi Vodacom

Baada ya mtifuano na malumbano ya takriban wiki tatu tangu ligi kuu ya Vodacom kuanza hatimaye jambo ambalo halikutegemewa kutokea likatokea. Tunazungumzia Yanga kupewa jezi zenye matakwa yao kwa maana logo ya Vodacom isiyokuwa na doa jekundu.

Hapa tunakutana na mtihani ambao kwa mtazamo wa haraka haraka unakupa ishara ya kuwa kuna walakini kwenye uendeshaji wa ligi ambao unatokana na asilimia kubwa busara kutotumika kwa ukamilifu wake.

Kwa namna ambavyo mgogoro huu ulivyoanza na namna ambavyo TFF ambao ndio walezi wa timu na ligi pamoja na kamati ya ligi ambayo inasemekana ipo kama msimamizi wa ligi ilishughulikia jambo hili, basi kuna siku huko mbele ya safari makubwa yatatokea.

Mengi yameshasemwa kuhusiana na namna ligi ya msimu huu ilivyoanza, hayumkini, kwa taasisi ya mpira wa miguu na wahusika wake wote wanaotengeneza ligi kufanya mambo kwa maslahi binafsi bila ya kuangalia maslahi mapana ya mchezo wenyewe ndio tatizo kubwa katika maendeleo ya jumla.

Kwa nini tunasema hivyo, ni kwa sababu kuna kosa kubwa limeshatendeka lakini kwa kulinda heshima na hadhi ya baadhi ya watu wakaamua kuficha ukweli. Kama tulivyoandika hapo juu dalili zinaonyesha kuna mapungufu ambayo kama mkataba ukitolewa na kuwekwa wazi basi kuna watu wataumbuka.

Ukiona mtu aliyezoeleka kuonekana wazi wazi ghafla anaanza kujificha asionekane wazi wazi mithili ya mtu anayetembea ndani ya baibui au hijab wakati alizoeleka kuonekana bila kificho, basi ujue nyuma ya kificho hicho kuna jambo.

Yote kwa yote ukipita mitaani kwenye viunga vya wapenda mpira wa kitanzania utakuta namna ambavyo wapenzi na wadau hao wanavyoelezea kuhusu matukio hayo ya ligi Tanzania. Jaribu kukatiza maeneo ya Mtoni Mtongani, Mwembe Yanga (Temeke ), Ubungo maeneo ya kituo kikuu cha basi, Kariakoo sokoni na mitaa ya Msimbazi mpaka shule ya Uhuru ndipo utaelewa janga lililopo huko mbele siku za usoni.

Hili la jezi za Yanga ni moja ya mtihani ambao umepatiwa ufumbuzi lakini kuna mashaka mengi ambayo yanarudi upande wa TFF na kamati ya ligi ambao kauli zao zinaonyesha kuna kitu..haiwezekani wewe ukawa ndio ulioingia mkataba kwa niaba ya klabu ambao nao hawajui nini kimo ndani alafu inapotokea mgogoro wa logo ya mdhamini msimamizi ambaye kwa muda wote unasimama na kuipinga Yanga, unatoa nafasi kwa Yanga waende wakaongee na Vodacom kama wataweza kuruhusiwa kutumia logo isiyo na doa jekundu na baada ya muda baada ya mikwara mingi tena ya wazee wa Yanga Vodacom inasalimu amri na kutekeleza matakwa ya Yanga.

Swali la kujiuliza, Je kama TFF walishindwa kuitetea Yanga kwa Vodacom na pia wameshindwa kuitetea Vodacom kwa Yanga wataaminiwa vipi na klabu au wapenzi na wadau wa mpira?

Mathalani timu kama Yanga itakapopata mgogoro wowote mwingine na TFF au kamati.

Je yanga hawatatumia udhaifu huu wa kamati na TFF wa sakata la jezi kukaidi maagizo yao? Majibu yako ni kama yetu.

TOa maoni yako hapa na kupitia mitandao yetu ya kijamii.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents