Makala

Makala: Magari na majumba ya kifahari tumeshayaona, wasanii wana lipi jipya kwenye video zao?

Miaka ya hivi karibuni tumeshuhudia mabadiliko makubwa kama sio mapinduzi katika soko la muziki wa kiafrika hasa kwenye upande wa video za muziki. Tumeona ongezeko kubwa la wanamuziki kuandaa video zenye ubora kuanzia kwenye muswada wa video (script), ubora wa picha, (lighting, frame rate, shutter speed, props nk), uwekezaji wa kifedha na muda, kutafuta maeneo mazuri ya kufanyia video (location) na kadhalika.

French Montana kwenye video ya Unforgettable iliyofanyika nchini Uganda

Mabadiliko au mapinduzi yamekuja na faida nyingi ikiwemo kuongeza mapato ya wasanii kutokana na mauzo yatokanayo na kutazamwa YouTube lakini pia kuwaweka kwenye ramani ya muziki wa ndani na nje kwa kuwafanya na wao waonekane ‘wamo’. Mapinduzi haya yametokea  wakati sahihi kwa Afrika ambako kabla ya hapo tulizoea video za muziki kama kitu cha ziada tu, na wasanii walitengeneza namna walivyotaka bila kuzingatia hasa mahitaji na soko linakwendaje na mashabiki wao wanataka nini.

Lakini tunapozungumzia mapinduzi katika sekta ya video za muziki, tukubali kuwa yamekuja na changamoto. Changamoto hii sio tu kutumika kwa gharama na nguvu kubwa katika uzalishaji na promo za kazi zetu bali changamoto kubwa ni muziki wetu kupenya kwenye soko la kimataifa hususani barani Ulaya na Marekani.

Bila shaka yoyote wasanii wa Waafrika wanafanya kila juhudi kupenya katika soko la dunia huku wakiendelea kulazimisha ladha yao ya kiafrika kubaki kama ilivyo. Katika hili, tumejiandaa? Wasanii wamepanga kufanya muziki tofauti na video tofauti?bila shaka hapa ndiyo kunatatizo.

Unapozungumzia kushindana na wenzetu wa magharibi ili kupenyeza katika soko la dunia, halafu kwenye video ya wimbo wako ukaweka magari na majumba ya kifahari utakuwa unawavutia kwa lipi hadi wakutazame au wavutiwe na kazi yako?

Kwa msingi huo, kwa mashabiki duniani hakuna ambacho bado hawajakiona kutoka katika video za wasanii wakubwa tunaowafahamu leo hii kwenye viwanda vya muziki. Hii imewafanya hata wao wakahama kutoka kutengeneza video za magari na majumba na kuhamia kutengeneza video za kibunifu na maudhui ya pekee.

Tufanye nini? Tunapojaribu kupenyeza katika soko la kimataifa lazima tuwaoneshe mashabiki mambo ambayo hawakutarajia au hawakuwahi kuyaona katika video za muziki ambazo zimekwishakufanyika na wasanii wakubwa duniani au hata Afrika. Ni muhimu tukapima kila mara na kuangalia mahitaji kuliko kufanya kwa mazoea zaidi.

Mathalani, video ya muziki ya Unforgettable ya French Montana imepata mrejesho mzuri kutoka katika pande zote za dunia, imefanyika Afrika, nchini Ugand, French Montana na muongozaji wa video walikuwa na jicho la kipekee kuona fursa katika sehemu ambayo watu hawajaishtukia, wasanii wa Uganda wanaimba mbele ya Cadillac Escalade huku wakishindwa kutumia fursa ya kuonesha uhalisia wa maisha ya jamii zao.

Barani Afrika, tumejaliwa maeneo na vitu vizuri na vya kuvutia ambavyo tunaweza kuvitumia kuuza video za muziki wetu kwa mashabiki kutoka kila kona ya dunia. Mfano, badala ya msanii kuonekana akiwa na gari na nyumba ya kifahari huku analia umasikini, ingekuwaje kama angefanya hiyo video kwenye landscape ya kiafrika, lakini video yake ikawa na viwango bora kabisa vya picha na kuweka uwekezaji uleule ambao tunautumia kwenye kukodi magari na majumba ya kifahari.

Jaribu kutafakari Diamond Platnumz ni Morani wa Kimasai yupo Ngorongoro anaenda kuoa binti wa kimasai katika boma jirani akisindikizwa na Morani wenzake wakiwa wamevalia mavazi yao ya kimasai wakipiga stori mbili tatu (japo mistari miwili ya kumezeshwa yenye subtittle) halafu anafika anakuta binti ameshaozeshwa kwenye familia nyingine waliotoa ng’ombe nyingi, kisha akaanza kuimba UKIMUONA akieleza machungu yake kwa rafiki wa binti, aina hii ya video lazima ipenye kimataifa kwani kuna utajiri wa kitamaduni ambao mataifa mengine yanataka kuuona na bahati mbaya wasanii wa hapa nyumbani hawatumii hiyo fursa.

Video ya namna hii ingeuza zaidi kwasababu wenzetu (mashabiki kutoka magharibi) hawajawahi kuona. Ni muhimu wasanii hasa waimbaji wakajikita katika kuuza uhalisia wa maisha ya waafrika na watu wa  mataifa yao kwasababu huo ndio ukweli wao, na wanaotizama video hizo ndicho wanachotaka kukiona.

Kwangu msanii kulenga soko la kimataifa kwa kuweka Lamborghini au Ferrari na mabinti machotara (lightskined) naona ni sawa na kufungua saluni ya kunyoa Jamaica au kuuza biblia Macca.

Ulishawahi kupata bahati ya kusoma maoni chini ya Video ya Salome ya Diamond Platnumz na Rayvanny? Wengi wa watu wa nje waliotizama video ile pamoja na kutoelewa kabisa kinachoimbwa, wamesifia mavazi na kuzungumzia muonekano wa wahusika huu ni mfano pata picha wasanii wetu wangewekeza kwa wingi kwenye kusimamia video kama hizo? bila shaka tungekuwa na muelekeo mzuri.

Wanamuziki wakubwa duniani wamewekeza kwenye vitu kadhaa kwenye video zao;

i. Visuals and Graphics kwa lengo la kuifanya video isichoshe kuangalia mfano video ya muziki ya Kendrick Lamar- Humble na The Weeknd- I feel it coming.

ii. Kutumia watu maarufu wengine mbali na wao kwenye video ili kuongeza mashabiki kutoka kwenye tasnia nyingine mfano, Jay Z kwenye album yake ya sasa 4:44 amemtumia Lupita Nyon’go ili kuongeza mashabiki ambao pengine wanavutiwa na filamu za Lupita.

iii. Video kuwa na vituko na vichekesho mfano PSY- Gungnam style hii huvutia zaidi wapenda vichekesho na kuwavuta wale ambao wamechoka kutizama video za kufanana.

iv. Kuchanganya tamaduni ili kuifanya video ivutie kwenye tamaduni mbalimbali. Baadhi ya wanamuziki wakubwa wanafanya hii kwakuwa hawana kipya cha kuonesha ulimwengu toka kwenye mataifa yao mfano, Omarion-Distance, French Montana- Unforgetable. Pia Jay Z, Rihanna na Nas wao wamekuwa wakichanganya sana utamaduni wa Jamaica katika video zao.

Sasa si lazima wasanii wa kitanzania kwenda moja kwenye niliyoyataja hapo juu ila kutumia tamaduni zetu za kiafrika kwenye video zao ni muhimu kwani kuna mengi ambayo dunia inataka kujua kutoka Afrika na sio majumba na magari ya kifahari kila siku.

Imeandikwa na Kennedy Mmari na Alpha Wawa

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents