Makala

MAKALA: Miaka mitano ya kifo cha Ngwear, bado kilio cha ‘Ghetto Langu’ kinawatesa wasanii Tanzania

Inaandikwa na Kennedy  Mmari

Pengine ghetto linalowachengua ‘maduu’ si tu ndoto ya kila kijana Tanzania na duniani kote, lakini imeendelea kuwa ndoto kwa kila msanii anayechipukia na hata msanii mkubwa nchini Tanzania.

Tarehe kama ya leo miaka mitano iliyopita moja ya Rappers mahiri  zaidi kuwahi kutokea nchini Tanzania, Albert Mangwear a.k.a Ngwear alifariki dunia nchini Afrika Kusini.

Ngwear anakumbukwa kwa uwezo wake mkubwa wa utunzi wa mashairi na uwezo wake wa kufokafoka kwa mitindo huru (freestyle) lakini pia zaidi kwa mchango wake katika kuukuza na kuusambaza muziki wa Bongo Fleva nje ya mipaka ya Tanzania.

Wachambuzi wa muziki nchini wamekua wakiitaja album yake ‘A.K.A MIMI’ kama miongoni mwa album bora ya muziki wa kizazi kipya, pamoja na uwezo huo Ngwair alifariki pasipo kufanikiwa kuishi maisha ya ndoto zake hata kwa kile kilichoonekana kwamba kwa aina ya kipaji na uwezo alipaswa kukimudu (Ghetto/Nyumba ya hadhi).

‘Ni ghetto langu tu linalowachengua maduu, linalonipa chati za juu, Kigogo mpaka East Zoo. Ghetto langu, utadhani majuu, ndilo linalonipa hadhi ya juu. Nimesota mpaka kulipata’

Ni moja ya mashairi inayopatikana katika wimbo ‘Ghetto’ ambao unajirudia rudia kuashiria uhalali wa ndoto hizi kwa wasanii walio wengi.

Ngwear alifariki wakati ambao bado yupo katika kilele cha umashuhuri kimuziki lakini bado hakuwa anamiliki ‘ghetto’ lillowachengua ‘maduu’.

Marehemu Ngwear ni mfano mmoja tu wa wasanii na watu maarufu ambao hawajafanikiwa kupata mafanikio wanayostahili kulingana na ukubwa wa majina yao kimuziki.

Ingawa bado kiwanda cha sanaa na muziki Tanzania ni kidogo na kinakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo uvamizi wa viwanda vya nje hasa vya Nigeria na Magharibi, lakini bado mafanikio yanayotokana na Sanaa yetu kwa wasanii yanazalisha maswali mengi kuliko idadi ya majibu.

Kwa mfano, kwa miaka mingi wasanii wa nchi jirani mathalani wa Kenya na Uganda wameendelea kufurahia mafanikio kutokana na biashara ya muziki kama vile kumiliki majumba makubwa na ya kisasa, biashara kubwa na magari ya kifahari kuliko wasanii wa Tanzania ingawa kwa ufananisho, kiwanda cha Sanaa cha Tanzania ni kikubwa kuliko katika nchi hizo.

Wasanii kama Jose Chameleone kutoka Uganda na Jaguar wa Kenya wameonekana kuwa na matumizi makubwa yanayotokana na muziki, na hata kama si mapato ya sanaa pekee waliyonayo, basi sanaa ndiyo imekuwa daraja la wao kuvuka na kupata mafanikio hayo.

Kwa kipindi kirefu pia hali imekuwa tofauti kwa wasanii wenzao wa Tanzania hata kwa wale wenye majina makubwa. Wengi wao wamekuwa maarufu zaidi kuliko hata mafanikio ya kawaida kama kumiliki biashara, nyumba na magari yenye hadhi.

Tukubaliane kuwa wasanii wa Tanzania bado hali zao haziendani na ukubwa wa majina yao, na hali zao kwa sasa huwezi ukaziona kwa macho ya kawaida ila mpaka kutokee tatizo ndio utajua ukweli wa maisha.

Mtizamo huu unaacha maswali ya msingi kwetu sote, ni nani anawakwamisha wasanii wa Tanzania? Ni wao wenyewe, sisi mashabiki wao au serikali?.

Ulale mahali pema peponi Ngwear, ni kweli pengo lako bado halijapata wa kuliziba.

IMEHARIRIWA NA PETER AKARO & GODFREY MGALLAH

_______________________________________________________________________________________________

Kwa sasa unaweza kupata habari zetu zote sehemu moja kwa kupitia App yetu ya Bongo5. Pakua sasa kupitia Play Store kwa kubonyeza link hii – https://bit.ly/2J2Argw

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents