Bongo5 Makala

Makala: Miwani yangu ilivyowasoma Harmonize na Mr Nice

Nimeangalia kwa umakini video mpya ya Harmonize ambayo ndani yake yupo Mr Nice ambaye kwa asilimia zote amejivika uhalisia wa ngoma hiyo.

Ndiyo, ni yule Mr Nice aliyeitangaza vema Bongo Flava Afrika Mashariki na kutoa hits song kibao kama Kikulacho, Rafiki, Fagilia, Kidali, Kuku Kupanda Baiskeli na nyinginezo kibao. Kiujumla ni video nzuri ambayo macho yako hatachoka kuitazama.

Hawa ni wasanii wa aina mbili wamekutana na kila mmoja ana uzito wake ila muda ndio unawatofautisha. Kutokana na hilo nimeona ni vema kuandika mambo machache sana kuhusiana na kazi yao kama nilivyoitazama.

Pande mbili za Harmonize

Wasanii wa WCB hasa Diamond wamekuwa na aina mbili za ngoma wanazotoa kwa kuangalia ni wapi wanataka ngoma husika ifike, sidhani kama umenielewa.

Kabla ya Diamond kutoka wimbo wake mpya wa sasa ‘ENEKA’, alikuwa ametoa nyimbo mbili kwa siku moja ambazo ni I Miss You na Fire aliyomshirikisha Tiwa Savage kutoka Nigeria. Kwa nini nyimbo mbili kwa siku moja?, jibu ni kwamba I Miss You ni kwa ajili ya soko la nyumbani na Fire kwa ajili soko la kimataifa.

Harmonize na naye pia anafuata mtindo huu wa Boss wake, wakati alipotoka na ngoma yake ya Iyola kisha kutoa ‘Bado’ aliyomshirikisha Diamond alitoa wimbo uitwao Matatizo. Ngoma hii ya tatu ililenga soko la ndani pekee, hivyo basi, alipotoa nyimbo kama Niambie na Show Me aliyoshirikiana na Rich Mavoko nilijua dhihiri hawezi kuwasahau watu wake wa nyumbani.

Wimbo wa Sina hauna tofauti yoyote na ule wa Matatizo katika kufikisha ujumbe, lakini kuna utofauti ujumbe huo ni kwa ajili ya nani na kwa muda gani.

Wimbo wa Matatizo unagumsa kila mtu na lengo la Harmonize ni kumfanya mwananchi wa kawaida anayeishi Tandale ajione na yeye ana sehemu yake katika muziki wa Harmonize.  Kwani tungo za mapenzi au starehe mara nyingi huishia kupendwa na matineja pekee lakini kuna kundi la watu wazima wanahitaji kujifunza kitu kutoka kwenye Bongo Flava.

Ngoma ya Sina anawalenga zaidi wasanii na mfumo wa maisha ambao wamekuwa wakiuishi kila siku. Kuna baadhi mifumo imekuwa inaaminika kuwapoteza wasanii wengi na hata kupelekea kuyumba kimaisha licha ya kuwa na umaarufu mkubwa.

Miongoni mwa wasanii ambao wamekuwa wakilaumiwa kwa kushindwa kutumia umaarufu waliokuwa nao kujinufanisha kimaisha ni Mr Nice. Pindi inapoibuka hoja ya wasanii kuwekeza pale wanapokuwa na biashara nzuri katika muziki ili baadae wasije kujutia, ni mara chache sana kulikosa jina la Mr Nice kutumika kama mfano.

Hivyo basi katika upande huu wa pili Harmonize aliona ujumbe wake utafika kwa haraka zaidi iwapo mhusika mwenyewe atakuwepo katika lengo kuu lake.

Mr Nice atarudi WCB wakiamua

Nakumbuka kipindi cha nyuma kulikuwa na uvumi kuwa Q Chillah angesainiwa na label ya WCB baada ya kuoneka kuwa karibu na Diamaond na hata uongozi wa label hiyo. Watu wengi waliamini Q Chillah angesanishwa WCB na kufanikiwa huku kungekuwa mwanzo wake mpya wa kufanya vizuri tena.

Siku hazigandi, muda una safiri mbio kama mwanga kwenye chumba cha giza. Mwaka huu Diamond akamtambulisha msanii mpya ndani ya label hiyo ambaye ni Lava Lava na ngoma yake ikatokea ‘Tuachane’ ambayo inafanya vizuri kwa sasa na maisha mengine yakaendelea.

Waliovumisha uvumi huu waliamini kabisa iwapo Q Chillah angeingia WCB angeweza kurudi katika nafasi yake kimuziki kutokana na ushawishi mkubwa ulionao label hiyo kwa sasa.

Kutotimia kwa hilo ni suala ambalo hakuna anaweza kutoa majibu ya kuridhisha zaidi ya wahusika wenyewe.

Hivyo basi baada ya video hii ya Harmonize ni lazima taarifa ziwe nyingi na maswali lukuki, je Mr Nice naye atasainiwa WCB? au tayari ameshasainiwa?.

Vyote vyote itakavyokuwa, twende mbele twende nyuma, binafsi bado naamini zaidi kwa Mr Nice kuliko Q Chillah, sababu ni moja tu. Ipo hivi, Mr Nice hajawahi kupewa nafasi kubwa kama aliyowahi kuipata Q Chillah chini ya Management ya QS ambayo ilibainisha kuwa ilitumia zaidi ya Tsh. Milioni 200 bila faida.

Iwapo wataamua kufunga macho na kuwekeza kwake walau kwa nyimbo mbili au tatu na ushawishi mkubwa walionao katika muziki huu bila shaka watafanikiwa. Naamini hivyo kwa sababu kiu ya wengi ni kutaka kumsikia Mr Nice baada ya kupotea kitambo kirefu katika muziki, vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

  Remix ya ngoma husika

Wakati wote fursa zipo kila sehemu, jifunze kuziona na kuzitengeneza, kama alivyoamini mfanyabiasha kutoka Uholanzi, Jacob Geit Dekker.

Bila kupepesa Harmonize ameishi katika fikra za mfanyabiashara huyu, kitendo cha kuamini Mr Nice anaweza kubeba uhalisia mkubwa katika video yake hiyo ni zaidi ya kuvumbua fursa kwani wapo wasanii wengi walikuwa maarufu sana kipindi cha nyuma na sasa hawasikiki.

Kile anachoimba Harmonize kwa namna moja au nyingine kinagusa maisha ya Mr Nice na ndio sababu ya yeye kuwepo katika video ya ngoma hiyo ili ujumbe uliokusudiwa uweze kuwafikia walengwa kwa haraka zaidi.

Kwa upande wangu naona iwapo na yeye angeimba walau verse ya pili ingeongeza ukubwa wa ngoma hiyo. Sababu ya kuamini hivyo ni kwamba kuna wale wasio na tv au uwezo wa kuingia katika mtandao wa YouTube kuitazama video. Kundi hii litafaidi melody na ujumbe wa ngoma husika ila maudhui makubwa katika picha/video ambayo pengine yangekuwa na faida zaidi kwao wameyakosa.

Sasa basi kundi tajwa hapo juu ili liweze kupata ujumbe uliokusudia bila ubaguzi ni wimbo huu kufanyiwa remix.  Iwapo hilo litafanikiwa itakuwa imempa Mr Nice key start iwapo atataka kusikika tena katika muziki wa Bongo Flava. Hadi kufikia hapa naomba nivue miwani yangu kisha tuendelee kufurahia muziki mzuri kutoka kwenye Bongo Flava yetu

By Peter Akaro

 

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents