Bongo5 Makala

Makala: Ni muda sasa wa Tanzania kuwa na record labels za uhakika

Record label ni nini? Ni kampuni inayosimamia wasanii ama brand, kuratibu utengenezaji wa nyimbo ama video, usambazaji, masoko, promotion na mambo mengine. Record label pia hufanya misako kupata wasanii wapya na kuwaendeleza.

2000px-Warner_Music_Group_logo_svg

Katika nchi zilizoendelea, wasanii waliofanikiwa wameendelea kutegemea zaidi record label kuongeza wigo wa kazi zao, kunadi albam zao na pia kufanyiwa promotion kuhakikisha wanasikika kwenye radio na kuonekana kwenye TV kwa msaada wa watu maalum waliojariwa kuwasaidia kuhakikisha kazi zao zinapatikana kwa wakati na sehemu husika.

Hata hivyo internet imeongeza kuwa njia mpya ya baadhi ya wasanii kuepuka gharama za kujitangaza na njia ya kupata mashabiki wapya.

Kuna aina tatu kubwa za label, major label (music group, label binafsi (indie) na sublabel (label zilizo ndani ya label kubwa).

Major labels, ni label kubwa zenye label zingine ndani kulingana na aina ya vipengele ama maeneo zilipo. Kwa sasa kuna label nne (Big Four) duniani ambazo ni pamoja na Universal Music Group, Sony Music Entertainment, Warner Music Group na EMI. Kwa uzoefu wa nchi zilizoendelea, record label huwa chini ya uongozi wa kampuni kubwa zaidi inayojulikana kama ‘music group’

UNIVERSAL_MUSIC_GROUP-copy

Labels mara nyingi huingia mkataba ‘exclusive’ wa kurekodi na msanii kumarket kazi yake kwa kumlipa mirahaba kutokana na kazi yake inavyoingiza faida.

Mkataba unaweza ukawa ule wa msanii kutoa kazi zake zilizo rekodiwa tayari ama kampuni kulipia na kusimimia kazi ya kurekodi nyimbo upya. Kwa msanii aliye na historia ya kurekodi, label huhusika katika kuchagua watayarishaji wa muziki, studio za kurekodi, wasanii wa nyongeza na nyimbo za kurekodi na wakati mwingine husimamia mpaka shughuli za kurekodi. Kwa wasanii wazoefu, label huhusika mara chache sana kwenye mchakato wa kurekodi.

Hapa Tanzania, zipo record label chache japo kutokana na uchumi, hazifanyi kazi kama zilivyo label kubwa za kimataifa. Hiyo ni kwasababu kuwa na record label kunahitaji mtaji mkubwa. Record label ni kampuni inayohitaji kuwa na wafanyakazi kama zilivyo kampuni zingine ambao wanatakiwa kulipwa mishahara kila mwisho wa mwezi.

Na ndio maana zile zinazoitwa record label nchini ni zile zinazopatikana kwenye studio husika ya kurekodi muziki. Kwa mfano Izzo Bizness, Shaa na Quick Rocka wapo chini ya label ya MJ Records. Mabeste na Gosby wapo chini ya B’Hits Music Group. Wapo pia wasanii mfano AY na kampuni yake ya Unity Entertainment iliyowachukua kwa mfano hio wa record label wasanii kama Feza Kessy na Stereo, kampuni ya Mwana FA Life Line Inc inayomsimamia Maua Sama nk.

Hata hivyo kwa mfano wa record labels katika nchi zilizoendelea, Tanzania bado haina kampuni yenye sifa hizo. Kuanzishwa kwa record label ya mfano wa zile za nje, kunahitajika mtaji mkubwa. Hii ni kwasababu record label inatakiwa kuwa na watu wa kusimamia kila hatua muhimu katika biashara ya muziki na msanii yeye akibaki kuhusika na upande wake wa kurekodi tu. Umuhimu wa kuwa na record label kwa msanii ni kuwa hujikuta akipunguziwa mambo mengi kama kusambaza nyimbo, kupanga interview, kufanya mipango ya kushoot video, mipango ya safari za tour na mambo mengine muhimu.

Kama kukiwepo na record label kubwa hapa nchini na zikafanya kazi zake inavyotakiwa, vipaji vingi vya muziki vitafanikiwa kimuziki huku pia kampuni hiyo ikipata faida. Kukiwepo record label za aina hiyo, wasanii watakuwa hawahangaiki kuzunguka kila radio ama TV kujipromote wenyewe.

Record label kubwa hutumia kiasi kikubwa cha fedha kwenye promotion ili kuhakikisha kuwa wasanii wao wanasikika na kuonekana kwenye kila radio, TV, majarida na magazetini. Hizi ni sehemu kubwa zinazotumika kutangaza kazi za msanii ili ziuze.

Sio rahisi kwa msanii peke yake kufanya promotion ya uhakika kwakuwa inahitaji gharama kubwa. Ni rahisi sana kwa record label yenye mtaji wa kutosha kufanikisha hili.

Kwa muda mrefu muziki wa Tanzania umekuwa na kasoro kwenye video zake. Sababu ni kuwa ili kufanya video nzuri, ni lazima pesa nyingi itumike. Ni wasanii wa kuhesabu wanaoweza kumudu gharama za kufanya video zenye muonekano wa kimataifa kama wazifanyazo wanaijeria. Hii itawezekana kwa wasanii wengi kama kukiwepo na record label zenye mtaji mzuri ambazo zitagharamia gharama zote huku zikifanya promotion ya uhakika kuhakikisha zinarudi na kila mmoja apate faida.

Kihistoria uchezwaji wa nyimbo kwenye radio umekuwa ni kitu muhimu zaidi wakati wimbo unapotoka. Wasikilizaji wa radio za mkondo mkuu (mainstraim radio station mf. Clouds FM, East Africa Radio, RFA, Kiss FM, Magif FM, Times FM na zingine) husikiliza radio kutaka kusikia nyimbo wazipendazo na pia huzitegemea zaidi kufahamu nyimbo mpya.

Kufanya kampeni ya radio nchi nzima kwa wimbo wa msanii hutumia pesa, muda, jitihada na uhusiano mzuri na watangazaji ama madj wa radio husika. Label nyingi hata zile kubwa kabisa duniani, huwapa kazi hii mapromoter wanaoweza kufanya kazi hii kwa ufasaha na wakafanikiwa kwakuwa huwa wana uhusiano mzuri na watangazaji ama wahusika wakuu kwenye vituo hivyo vya radio.

Kwa Tanzania kazi hiyo yote hufanywa na msanii mwenyewe na wasanii wengi hushindiwa hapo. Kwa uzoefu wa Marekani, promoter wa kufanya kazi hiyo huweza kutoza hadi dola 40,000 kufanya kazi hiyo kwa wimbo mmoja na baada ya wiki nane kazi hiyo hukamilika. Kwa kuangalia uchumi wa Tanzania, kazi hiyo inaweza kufanyika kwa gharama nafuu zaidi. Wapo watu wachache Tanzania wanaofanya kazi kama hiyo, mfano akiwa ni Babu Tale.

Ni muda sasa wa inatakiwa ajitokeze mdau mkubwa wa muziki mwenye mtaji wa kutosha na mwenye mapenzi ya dhati na muziki wetu pamoja na uelewa, kuanzisha record label kubwa. Hatua hiyo itaonesha njia ya jinsi biashara ya muziki inavyoweza kuwa chanzo cha ajira kwa watu wengi wenye sifa stahili na hatimaye kuupelekea muziki wetu hatua za mbele zaidi.

Makala imeandikwa na Fredrick ‘Skywalker’ Bundala (Bongo5 Head of Content)

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents