Bongo5 MakalaBurudani

Makala: Nyimbo hizi 10 za Kibongo zingefika mbali kama…..

Na Wynjones Kinye

Nadhani hakuna changamoto kubwa kama ya kum”kwachu” shabiki pindi uwapo msanii. Kama huna moyo wa kustahimili mapokeo ya kile unachotoa, nadiriki kusema kuwa unaweza ukabwaga manyanga kwakuwa shabiki ni “nazi ngumu kuvunja”.

headphones

Niko na washkaji kadhaa maskani tunazungumza kishabiki na topic inayofanya sauti zetu zipae ni nyimbo ambazo hazikutendewa haki na wasanii pamoja na uongozi mzima wa wasanii husika. Tunazungumzia nyimbo ambazo kwa kuzisikiliza ni nzuri sana lakini hazikuwafikia watu wengi kwasababu tu jitihada za kufikishwa kwao hazikuwa za kuridhisha. Tumezungumza kiujumla sana, hapa nalazimika kuzungumzia nyimbo kumi tu ambazo endapo zingefanyiwa video nzuuuuri, basi zingewafikisha mbali sana wenye nyimbo hizo.

1. PUNCHLINE-Nikki Mbishi Ft. Grace Matata

Nani wa kupinga kwamba wimbo huu uliistua hiphop tz? Leo tunashuhudia kizazi kilichojaa watu wa kufanana kimitambao, mimi nasema chanzo ni PUNCHLINE na nitakuwa na wengi wa kuungana name kimawazo.

Hili lilikuwa toleo la kipekee kwa Mbishi. Production ilikuwa nzuri sana na chorus ya kitofauti aliyofanya Grace Matata ndio usiseme. Ila wimbo huu kiukweli haukuwafikia watu wengi, naamini wapo mashabiki wa Nikki wa hii leo wasiojua wimbo huu, hususan wale ambao hawakubahatika kupata nakala ya Sauti ya Jogoo. Mimi na wenzangu tunasema Punchline ingepata video basi Nikki angekuwa mbali zaidi ya alivyo hivi sasa.

2. BINTI MALIKIA-Fid Q Ft. Nuruelly

Ukizungumzia nyimbo bora za mapenzi za Hiphop zilizowahi kutokea kwenye ardhi ya Tanzania basi hutauacha wimbo huu. Binafsi nauita bora wa nyakati zote content wise. Ukiacha uzito wa mistari ya Fid kwenye wimbo, jinsi anavyomuimbia kisela binti malikia kunafanya wimbo huu udumu kuwa mzuri. Nao ulihitaji video nzuri na kwa wakati ule bado uwezekano wa kufanya video nzuri ulikuwepo.

3. RAHISA-TID Ft. Mwanafalsafa

Wakati huo TID alikuwa hashikiki…sikuyaelewa mazingira ya kutoka kwa wimbo huu, si kama alivyoachia Zeze, Siamini na nyinginezo. Ni kama aliuchukulia poa lakini nadiriki kusema kwamba huu haukuwa wimbo wa kuchukuliwa poa. Naamini ungemuweka sehemu nzuri zaidi kutokana na kumshirikisha FA ambaye pia alikuwa vizuri mno kinyota.

4. PETE-Ben Pol
Wimbo huu ulikuwa wa maana sana kwa mashabiki, ndio tayari Ben alikuwa ameshahit kwa matoleo mengine, lakini toleo hili lilikuwa muhimu sana. Pete ni toleo la kwanza la Ben akiwa nje ya Mlab, kwa mashabiki pale tulikuwa tunasubiria kwa hamu mno. Naamini kwa uzuri wa Pete kama ingepata video nzuri kwa wakati ule basi iko wazi kuwa kibiashara Ben angekuwa mbali zaidi ya alivyo hivi sasa.

5. BOSI-Ferooz Ft. Nature & Solo Thang

Si music video pekee, ila Bosi ya Ferooz ingetoa story nzuri sana ya movie na hatimaye kuwanufaisha zaidi hawa mabwana watatu. Ilikuwa na bado ni miongoni mwa nyimbo kali kuwahi kutokea kwenye tasnia hii hapa tz. Ulalamikaji wa Ferooz kisauti na kipicha kingeipa nguvu video, uchale wa Nature na ustaarabu wa Solo vyote kwa pamoja vingeunda kitu kizuri, kwa wakati ule video ile ingepambwa na waigizaji maarufu wa tamthilia wenye kusadifu nafasi za wahusika kwenye wimbo basi tungekuwa tunazungumzia mambo mengine hivi sasa kwenye wimbo huu na kwa Ferooz.

[soundcloud url=”https://api.soundcloud.com/tracks/128457520″ params=”color=ff6600&auto_play=false&show_artwork=true” width=”100%” height=”166″ iframe=”true” /]

6. NIKUPE- Man Dojo na Domo Kaya

Kati ya wasanii wa Tanzania waliotakiwa kuwa kimataifa sasa hivi ni Mandojo na Domokaya. Walikuwa na kila sababu ya kutusua kimataifa, uimbaji wao unaosindikizwa na chombo kipendwacho na wengi “guitar” ulikuwa ni silaha kubwa sana kwao kufika mbali. Nadiriki kusema kukosekana kwa video ya debut song yao “nikupe” kumezaa mjukuu huyu. Nikupe ilitakiwa kuwafikisha mbaaali sana, na kote huko kungefikika kama ingalikuwapo video.

7. WANOKNOK- Man Dojo na Domo Kaya ft. Lady Jaydee

Yote niliyoyasema kwenye Nikupe yanazama humu lakini yapo ya nyongeza. Jay Dee kushambulia wimbo huu na hawa mabwana ilikuwa ni kitu kimoja mahiri sana, ukichanganya na mpishi wa mlo huu mzungu Miika Mwamba basi Wanoknok ingekuwa hatari zaidi kama ingebarikiwa kichupa. Najiuliza na sipati jibu la kwanini huu wimbo haukuwa na video ikiwa wakati huo hawa mabwana walikuwa na support kubwa ya Jay Dee ambaye tayari yeye wakati huo kila toleo lake lilikuwa na video, na kumbukumbu zangu zinasema Executive Producer wa album ambayo Wanoknok inapatikana alikuwa ni JayDee.

8. BARUA-Daz Nundaz

Wangeamua kusimama kama kundi mpaka leo basi Afrika Mashariki Sauti Sol wangekuwa chini ya hawa mabwana. Uwezo wao ulipitiliza kwakweli. Barua kwangu mimi ni wimbo wa tatu mzuri wa masimulizi kuwahi kutokea Tanzania. Moja na mbili natoa kwa Bosi na Starehe za Ferooz. Lakini Barua ilizitangulia zote hizi, video ya Barua ingewaweka pazuri sana Daz Nundaz.

9. SITAKI DEMU-Juma Nature

Nature ni kama yuko allergic na videos, huwa hatoi videos na akitoa huwa ni mbaya…sasa sijui ni maandalizi yake ama ni directors wanaofanya nyimbo zake ndio wanashindwa kumfitisha. “Dance with Me” ndio video ambayo kidoooogo Juma Nature “alitokelezea”.

Sitaki Demu ni moja ya nyimbo bora kabisa za Nature. Audio ilimpa faida kubwa sana kibiashara, ni kama aliridhika na mafanikio yale akasahau kufanya video yake. Angetumia wachekeshaji wa Kaole kipindi kile kuipamba video basi Sitaki Demu ingekuwa inaishi mpaka leo naamini.

10. ANAISHI NAYE-Belle9 & Ben Pol

Haukuwa wimbo wa kiwango cha hawa mabwana wawili, lakini kwasababu mashabiki walikuwa wakisubiri kwa hamu duet yao basi wimbo ulipokelewa vizuri japo haukutiliwa nguvu sana. Mimi ningekuwa na sauti katika kuwaamulia basi ningewagongesha kichupa cha wimbo huu hivyo kusababisha kila mmoja kuvua mashabiki katika dimbwi la mashabiki wote.

Mimi na wewe tunajua kuwa kuna nyimbo nyingi ambazo zilistahili video kutokana na uzuri wake katika audio. Nyingine labda zina kila haki ya kuwa ndani ya kumi hizi lakini na mimi ni shabiki na nina mapokeo yangu, naendeshwa na moyo wangu na nyoyo za wengine katika majadiliano yetu.

Unaweza kumfollow Kinye kwenye Twitter @kinye42 au kumtumia email: [email protected]

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents