Bongo5 MakalaBurudaniDiamond Platnumz

Makala: Sababu tano kwa nini nawakubali AY na Diamond (+video)

Kwa wakati huu unapotaka kuzungumzia mafanikio ya muziki wa Bongo Fleva katika ngazi ya kimataifa, huwezi kuepuka kuyataja majina ya Ambwene Yessayah ‘AY’ na Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’.

AY na Diamond

Tulimfahamu AY kupitia wimbo ‘Ni Raha Tu’, na Diamond kupitia ngoma yake ‘Kamwambie’. Wasanii hawa wamekuwa wakipambana sana kuhakikisha muziki huu unafika mbali zaidi na kupata dhamani kubwa kwenye mataifa mengine na hilo wamefanikiwa kwa asilimia kubwa.

Kabla ya kufika mbali unaweza kutazama video ya makala nzima hapa chini

Binafsi nimekuwa nikivutiawa sana na wasanii hawa, sasa leo kupitia Bongo5 Makala ningependa kukushirikisha hizi sababu tano kwa nini nawakubali wasanii hawa.

  1. Kuitangaza Bongo Fleva Afrika

AY alianza kufanya kazi na wasanii wa Kenya na Uganda kitu kilichoipa Bongo Fleva nguvu katika nchi hizo, alifanya kazi na wasanii kama Prezzo na Maurice Kirya ambao walikuwa na nguvu kubwa ya ushawishi kwa wakati huo na ukawa mwanzo wa Bongo Fleva kupewa heshimu Afrika Mashariki akishirikiana wasanii wengine kama Lady Jaydee na Prof Jay, tuachane na hilo.

Kama kumbukumbu zangu zipo sawa huenda AY ndiye msanii wa kwanza kutoka kwenye Bongo Fleva kufanya kolabo kubwa na wasanii kutoka Nigeria. Wakati kundi la P Square linafanya vizuri na nyimbo zake kama Temptation na Dome walikuja Tanzania kufanya show, ndipo AY alipoona kuna uwezekano wa kufanya kazi na kundi hilo ambalo lilianza kuiteka Afrika kimuziki.

Kundi la P Square

Bila kupoteza muda wakaingia studio B Hit’s kwa Prodyuza Hermy B na kutoa wimbo uliokwenda kwa jina ‘Freeze’ ambao ulishangaza wengi na kujiuliza AY amewezaje?. Wakati huo wana-Nigeria walikuwa wanafanya vizuri katika movie kuliko muziki ndio maana baada ya AY ilichukua muda kwa msanii mwingine kutoka Tanzania kufanya hivyo.

Ilichukua zaidi ya miaka minne kama sio mitano hadi pale Diamond alipokuja kumshirikisha Davido, hiyo ilikuwa mwaka 2013 kwa pamoja walitoa wimbo uitwao ‘My number One’ ikiwa ni remix ambayo ilimleta Diamond mpya kwenye Bongo Fleva.

Kazi ilifanyika studio za Burn Records kwa prodyuza Shed Clever, licha ya wimbo huu kumtambulisha Diamond kimataifa pia ulimtambulisha Shed Clever na kumuwezesha kuwania tuzo za Afrimma Dalas Texas Marekani, ingawa hakushinda.

Ni vema kujua hili

AY hakuishia kwa P Square tu bali alikuja kufanya kazi na wasanii kama Goldie Harvey ambapo walitoa wimbo uitwao ‘Skibobo’ uliotoka mwaka 2012. Goldie Harvey ambaye kwa sasa ni marehemu alikuwa mwakilishi wa Nigeria katika shindano la Big Brother Africa (BBA) kwa mwaka 2012 ambapo alianzisha uhusiano wa kimapenzi na msanii wa Kenya, Prezzo.

Kama hiyo haitoshi mwaka 2013 AY pamoja na Mwana FA walimpa shavu J Martins kwenye wimbo uitwao ‘Bila Kukunja Goti’, chini ya prodyuza Marco Chali. Diamond nae alizidisha mashambulizi kwa kufanya kazi na wasanii kama Iyanya aliyempa shavu kwenye wimbo ‘Bum Bum’. Mr Flavour alichukua nafasi kwa kupewa shavu kwenye wimbo wa ‘Nana’ uliopikwa na prodyuza Nahreel.

Ili kudhibitisha ubora wake mwaka jana Diamond alidondosha ngoma aliyowashirikisha P Square ‘Kidogo’, hivyo kufanya AY na Diamond kuwa wasanii pekee kutoka Tanzania kufanya kazi na kundi hilo bora barani Afrika.

  1. Hadi Marekani

Diamond na AY si watu wa mchezo kabisa, wote wawili wanaingia katika vitabu vya kumbukumbu kwa kufanya kazi na wasanii kutoka nchini Marekani. AY alianza kwa kumshirikisha Miss Trinity kwenye wimbo uitwao ‘Good Look’.

Mwaka 2014 aliachia nyimbo mbili kwa mpingo ambazo alifanya na wasanii wa Marekani. AY alimshirikisha Sea Kingston kwenye wimbo uitwao ‘Touch Me’. Pia alimshiriksha tena Miss Trinity na Lamiya kwenye wimbo wa ‘It’s going down’. Video za nyimbo hizi zilifanyika Marekani na AY anakiri ni miongoni mwa video alizowekeza fedha nyingi zaidi.

Sea Kingston na AY

Tukihamia kwa upande wa Diamond, wimbo aliofanya na Msanii wa Marekani ni Marry You ambao amemshirikisha Ne-Yo, msanii aliyetamba na nyimbo kama, So Sick, Because of You, Miss Independent na nyinginezo kibao. Wimbo huo uliosimamiwa na prodyuza Shed Clever iliwalazimu kusafiri hadi Nairobi Kenya ambapo wakati Ne-Yo alikuwa anafanya show huko.

Ne-Yo na Diamond
  1. Uwezo wao binafsi

AY alimshirikisha Diamond kwenye remix ya wimbo wa ‘Zigo’ ambao ulitoka takribani mwaka mmoja kabla, hivyo hiyo remix ilifanya wimbo huo kukaa katika media rotation kwa miaka miwili. AY alikaririwa akisema kama asingempata Diamond katika wimbo huu basi angemshirikisha msanii Wizkid kutoka Nigeria.

Kwa kujiamini AY alieleza umefika wakati kwa wasanii wa Tanzania kutengeneza muziki mkubwa bila kushirikisha wasanii wa nje. Katila hilo wamefanikiwa kwa asilimia kubwa kwa kuwa tuliona wimbo huu ukifanya vizuri na kuingia katika chati za muziki za vituo vikubwa vya televisheni vya Afrika na Ulaya pia.

Video ya wimbo huu hadi sasa katika mtandao wa YouTube umetazamwa na watu zaidi ya milioni 8.9 tangu utoke Januari 22 mwaka jana, hivyo kuufanya kuwa katika Top 10 ya nyimbo zilizotamwa zaidi mtandaoni Bongo.

Tumalize hivi, kutambua ukubwa wa hii kolabo, AY anawakutanisha maprodyuza watatu ambao ni Nahreel, Marco Chali na Hermy B kunogesha mdundo wake, hiki ni kitu ambacho hutokea mara chache sana katika Bongo Fleva.

  1. Kusimamia wasanii

Utamaduni wa wasanii kusimamia wasanii wengine (lebo) ulikuwa umpotea kabisa Bongo au ulikuwa haupo. AY alianzisha kama sio kurudisha utamaduni huo pale alipoanzisha utaratibu wa kusimamia wasanii pale alipoanzisha Unity Entertainment.

Unity Entertainment aliweza kusimamia wasanii kama Ommy Dimpoz na Stereo na kuweza kutoka fursa kwa Ommy Dimpoz kufanya kazi na J Martins wa Nigeria na Stereo kutoa wimbo na Victoria Kimani kutoka Kenya.

AY, Victoria Kimani na Stereo wakati wa kurekodi wimbo ‘Wako’ (Never Let You Down) chini ya Unity Entertainment.

Katika hilo Diamond hakua nyuma ndio maana mwaka 2015 alitambulisha rasmi lebo yake ya WCB ikiwa na msanii mmoja tu ambaye ni Harmonize. Kadiri siku zinavyodi kusonga mbele ndivyo na WCB inazidi kukua hadi sasa imeweza kusimamia wasanii watano ambao ni Harmonize niliyetangulia kumtaja, Rayvanny, Rich Mavoko, Queen Darleen na Lava Lava aliyetambulishwa mwaka huu.

WCB

Ujio wa Unity Entertainment na WCB ni kama umeleta muhamko kwa wasanii wengine kufanya hivyo kwani hapo awali waliokuwa wanasimamia wasanii mara nyingi ni maprodyuza na watu wenye mapenzi na muziki lakini sasa wasanii kama Fid Q, Ommy Dimpoz, Vanessa Mdee na wengineo wanasimamia wasanii wao lakini chimbuko ni kwa AY na Diamond.

  1. Kumiliki biashara

Hivi majuzi P Diddy alitajwa na Forbes kuwa namba moja kati ya mastaa watano wa Hip Hop wenye fedha nyingi zaidi duniani. P Diddy anamiliki utajiri wa dola milioni 820 ambazo zinatokana na biashara zake ikiwemo Ciroc Vodka, Revolt TV, na ziara yake iliyoanza mwaka jana ya “Bad Boy Family Reunion Tour.

Hii inaonyesha ili msanii kuendelea kuwa bora uwekezaji ni kitu cha muhimu zaidi kuliko kwenda studio na kurekodi. AY na Diamond nawaona kama wasanii wenye mtazamo huo.

Sote tunafamu AY ni mmoja ya wamiliki wa Mkasi Tv (Mkasi Production), ilikuwa tv show na hadi Ngaz kwa Ngaz. Mkasi kilikuwa kipindi cha aina yake kutokea nchini kutokana na ubunifu wake kitu kilichopeleka kushinda tuzo mbili ‘Tuzo za Watu’.

Enzi ya kipindi cha Mkasi

Katika wimbo wa El Chapo aliomshirikisha Jokate, sauti ya mrembo huyo inabainisha kuwa AY ni msanii pekee wa Tanzania kufanya kitu kama hicho, pongezi kwake.

Kwa upande wa Diamond ambaye naweza kusema anamtama AY kama role model wake kama  umenifuatilia vizuri kuanzia mwanzo, yeye mwaka huu ameingiza sokoni manukato yake ‘Chibu Perfume’ kitu ambacho naamini kitamuweka sehemu nzuri zaidi kiuchumi.

Kibwagizo

Ukijua kutafuta fedha ni lazima ujue pia na kuzitumia, bila hivyo wewe utakuwa mtumwa. Sasa sikia hii, AY aliwahi kuweka meno ya gold, siku moja Diamond alipomuona nayo naye akamuambia na mimi naenda kuchukua ya kwangu na kweli akafanya hivyo. Hivi ni vitu vya kujifurahisha tu lakini kama unajua kutafuta fedha si mbaya kufanya hivyo.

By Peter Akaro

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents