BurudaniDiamond PlatnumzMakala

Makala: Saida Karoli amewachambua kama karanga Belle 9, Diamond na Darassa  

Mwaka 2001 msanii wa muziki wa asili, Saida Karoli alitoa albamu yake ya kwanza ‘Maria Salome’ ambayo ilipata mafanikio makubwa na kuingia katika vitabu vya kumbukumbu vya muziki wa kitanzania.

Albamu hiyo iliyochota vionjo tele vya kabila la Kihaya, mashabiki wengi waliipachika jina la ‘Chambua kama Karanga’ kutokana na maneno yanayopatikana katika wimbo wa Maria Salome ambao umebeba jina la albamu.

Inaelezwa miezi mitatu baada ya kutoa albamu hiyo, Saida Karoli alipata mwaliko wa kuimba nchini Uganda ambapo Kabaka wa Buganda alimwalika katika sherehe ya kiutamaduni, pia kumfanya kuwa mwanamuziki wa mwaka katika sherehe hiyo.

Pia albamu hiyo ilifuatiwa na ziara kubwa alizofanya katika nchi za Burundi, Rwanda, Uganda na Kenya ambapo alipata mafanikio makubwa na Saida kujikuta akibatizwa na kupewa jina la malkia wa nyimbo za asili.

 Karibu Diamond, Darassa na Belle 9

Septemba 18 mwaka jana Diamond Platnumz alitoa wimbo uitwao Salome akiwa amemshirikisha Rayvanny. Wimbo ukiwa umekopa beat, melody na baadhi ya maneno kutoka kwenye wimbo wa Maria Salome wa Saida Karoli.

Wimbo huu uliotengenezwa na prodyuza Lizer kutoka Wasafi Records na video yake kuongozwa na Nocorux kutoka Afrika Kusini, watu wengi walihoji juu ya uhalali wa Diamond kutumia vionjo wa wimbo wa Saida Karoli, lakini uzuri ni kwamba pande zote mbili zilikuwa tayari zimeshahafikiana.

Baada ya Diamond kufanya vizuri sana na wimbo huo, haikuwa ajabu November 23 mwaka jana kuona rapper Darassa akitumia baadhi ya vionjo kutoka kwenye wimbo wa Maria Salome katika wimbo wake ‘Muziki’ aliomshirikisha Ben Pol.

Muziki ni hit sing iliyoweka historia katika maisha ya muziki ya Darassa akipata baraka kutoka kwenye mikono ya prodyuza wa watatu, Mr Vs, Abbah na Mr T Touch.

Wakati watu wakiruka madebe na ngoma ya Muziki na Salome, huku wakijikumbushia mwanzoni mwa miaka ya 2000 walivyolirudi na ngoma ya Maria Salome, mkali wa muziki wa RnB, Belle 9 anadondosha ngoma yenye vionjo sawa na hizi mbili za mwanzo.

Belle 9 alikuja na wimbo uitwao Give It To Me, hiyo ikiwa ni December 17 mwaka jana. Wimbo huu alimshirikisha mkali wa chorus kutoka Weusi, G Nako chini ya prodyuza Luffa.

Saidi Karoli awachambua kama karanga

Wiki hii Saida Karoli ameamua kuvunja ukimya kwa kuachia wimbo uitwao Urugambo. Wimbo huu tunaweza kusema ameamua kijilipa fadhila kwani amechukua baadhi ya maneno kutoka kwenye nyimbo zote tatu nilizozielezea hapo juu.

Akiwa anaimba kiswahili na kikabila (kihaya) kama ilivyo kawaida yake, ameweza kuchanganya nyimbo zote tatu na kutoa kitu kimoja cha kipekee sana ambacho kila upande utakielewa. Najua hujanielewa, namaanisha mashabiki walioanza na Saida Karoli hawatochoka kuusikiliza, na kizazi cha sasa cha Bongo Fleva kitapenda kuusikiliza pia.

Katika wimbo huu wenye dakika 3 na sekunde 58, Saida Karoli ananza kuchambua ngoma ya Darassa Muziki kwa kusema, “Nikamuuliza baba yangu, akasema utafute ule mpaka Dar es Salaama… Nimesimama wima x 2…. Maisha na muziki, acha maneno weka muziki x 2”.

Kisha anaendelea na wimbo wa Belle 9 ‘Give It To Me’, “Nikaenda Dar es Salaam nikakuta wazangu, wanaongea kizungu na mimi nikaimba kizungu, ‘Baby give it to me, ahaaa!! x 6”. Wakati akichanganya lugha mbili anaendele na wimbo wa Diamond ‘Salome’.

“Nikaeenda Dar es Salaa nikashanga ‘majumba’,….  “Wanakodoa kodo wanakodoa!! (macho kodo) (wale kodo) x 2”. Kisha chorus fupi yenye melody ya aina yake, watoto wa mjini wanasema amazing, “Baby nimekuweka moyonii, usije ukaniacha nitaumia”.

 Ni faida kwa Bongo Fleva

Bila shaka leo katika vitu 10 ambavyo Fid Q anajivunia katika muziki wake, hawezi kuweka kando mafanikio ya kufanya kazi na wasanii wa zamani kama Zahir Zorro na Bibi Kidude.

Pia tumeona mwaka huu Kassim Mganga akitoa wimbo na Killimanjaro Band (Njenje) ambapo pia Mwana FA alishatoa nao ngoma. Hii maana yake nini?, wasanii wa zamani na wa Bongo Fleva wanapokuwa karibu na kufanya kazi, maana kuna vitu wanaleta katika muziki wa sasa na pengine huko mbeleni tutakuja kupata utambulisho (ID) ya muziki wa kitanzania ambao umekuwa ukisemakana haupo.

By Peter Akaro

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents